Seth wa IPTL aruhusiwa kuzungumza na mkewe

Muktasari:

  • Ruhusa hiyo imetolewa leo Juni 21, 2018 na hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma  Shahidi baada ya upande wa utetezi kudai kuwa Seth hajapata nafasi ya kuonana na mkewe na kumpa pole, baada ya kufiwa na mama mzazi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeruhusu mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habinder Seth  kuongea na mkewe, mahakamani.

Ruhusa hiyo imetolewa leo Juni 21, 2018 na hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma  Shahidi baada ya upande wa utetezi kudai kuwa Seth hajapata nafasi ya kuonana na mkewe na kumpa pole, baada ya kufiwa na mama mzazi.

"Nikisema waongelee ndani ya chumba hiki cha mahakama nitakuwa nakiuka haki ya mshtakiwa kwa sababu hawa ni watu wazima, hawatakuwa huru kuongea," amesema Shahidi.

Shahidi amesema mshtakiwa ana haki ya kupewa nafasi ya kuonana na kuongea na mke wake, kwa sababu hajatiwa hatiani.

“Naomba mshtakiwa huyu apewe nafasi ili aweze kuongea na mke wake, hivyo watu wa magereza muangalie utaratibu wa kumruhusu mke wa Seth aongee na mumewe hapa mahakamani kabla mshtakiwa hajarudishwa mahabusu" amesema.

Mbali na Seth, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara, James Rugemarila, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 katika Mahakama hiyo.

 

Awali, wakili wa Seth, Chuma John alidai kuwa mteja wake hajapewa kibali cha kuongea na mke wake gerezani na hata  mahakamani, licha ya mahakama hiyo kuruhusu kuonana na mke  gerezani.

“Mpaka sasa mke wa Seth, hajapata kibali cha kumuona mumewe gerezani wala hapa mahakamani" alidai John

Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya  uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi.

Pia, wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola 22 milioni za Marekani na Sh309.46 bilioni