VIDEO-Sh1.5 trilioni bado mtihani mzito

Muktasari:

Na hasa mtihani mzito ni hoja ya Sh1.5 trilioni ambazo ni tofauti ya fedha zilizokusanywa na Serikali kwa mwaka huo wa fedha na zile zilizotumika na kukaguliwa na CAG.

Kama kuna wakati ambao Serikali ya Awamu ya Tano, Bunge la Kumi na Moja, Mawaziri, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na wadau wengine wamewahi kuwa na mtihani mzito, basi ni hoja za ripoti ya ukaguzi ya 2016/17.

Na hasa mtihani mzito ni hoja ya Sh1.5 trilioni ambazo ni tofauti ya fedha zilizokusanywa na Serikali kwa mwaka huo wa fedha na zile zilizotumika na kukaguliwa na CAG.

Tangu ripoti hiyo ilipokabidhiwa bungeni Aprili 11, kumekuwa na mtukio tofauti ndani na nje ya Bunge yanayoashiria uzito wa hoja zilizoibuliwa katika ukaguzi huo wa kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Tofauti na miaka mingine, mawaziri wamekuwa wakijitokeza mbele ya waandishi wa habari kujaribu kuzijibu, hali kadhalika wabunge ambao pia wametumia ripoti hiyo kujenga hoja zao bungeni.

Pia katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alijitokeza hadharani kujibu hoja iliyoibuliwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuhusu Sh1.5 trilioni.

Na juzi, Rais John Magufuli alizungumzia kidogo wachambuaji wa ripoti hiyo, akionyesha kuwa haijataja kwamba kuna wizi wa Sh1.5 trilioni, na kuiachia kamati za Bunge kufanya kazi yake.

Rais alizungumza hayo muda mfupi baada ya Serikali kutoa kauli yake bungeni kuhusu fedha hizo ambazo CAG hakuzikagua.

Hoja hiyo iliibuliwa na Zitto alipozungumza na waandishi wa habari kutoa taarifa ya uchambuzi wa chama chake wa ripoti hiyo ya CAG, na kujikita zaidi katika tofauti hiyo ya mapato na matumizi, akiitaka Serikali kueleza zilikokwenda fedha hizo.

Pamoja na Serikasli kutoa maelezo, Zitto ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, ameendelea kushikilia msimamo wake, akiitaka Serikali kuacha vitisho na kujibu hoja alizoibua na kwamba yuko tayari kukamatwa na kushitakiwa mahakamani.

Mpaka sasa Serikali inaonekana kujibu hoja moja tu ya kutoeleweka kwa matumizi ya Sh1.5 trilioni mbali ya hoja alizoibua Zitto.

Bunge kwenye mtihani

Tayari hoja hiyo imeshaanza kulitingisha Bunge ambalo linatakiwa lijadili ripoti hiyo kwa kutumia kamati zake za Hesabu za Serikali (PAC) na ya Serikali za Mitaa (LAAC).

Lakini kamati hizo za Bunge zitakuwa katika wakati mgumu kujadili kasoro hizo baada ya mawaziri kujitokeza kuzijibu na baadaye kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua iwapo zitathibitika.

“Taarifa ya CAG ina utaratibu wake wa kuijibu na si humu bungeni. Majibu ya CAG yanatakiwa kutolewa katika kamati ya PAC na CAG kuthibitisha na kisha kuletwa bungeni kujadiliwa,” alisema mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara bungeni wiki iliyopita.

Mbunge wa CCM (Morogoro Kusini Mashariki), Omary Mgumba alitoa maoni kama hayo.

“Hili si jambo la kupuuza, ni jambo lililozungumzwa na CAG katika ripoti yake ambayo sisi wabunge na Watanzania ndiyo jicho letu. Kwa hiyo tunapoona Sh1.5 trilioni hazina maelezo ya kutosha, tunapata mashaka,” alisema Mgumba.

Lakini mbunge wa viti maalum, Fatma Hassan Toufiq alisema: Naibu Waziri amefanya jambo sahihi, Kwa sasa kinachotakiwa ni watu kushikamana kwa pamoja.”

Hata hivyo, makamu mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillal aliondoa hofu hiyo ya kamati kutoweza kufanya kazi yake vizuri baada ya majibu hayo ya mawaziri.

“Serikali kuleta taarifa bungeni sio mbaya, lakini kwetu kamati ukaguzi uko palepale. Kamati itamuita katibu mkuu wa Wizara ya Fedha atoe ufafanuzi kwenye kamati na CAG akiwepo,” alisema Aeshi.

Serikali matatani

Pamoja na Bunge kuwa na mtihani, wapo wanaoona kuwa ripoti hiyo inaweka mtihani mkubwa kwa Serikali ambayo imeonekana kuwa na kasoro kadhaa licha ya maelezo hayo ya Sh1.5 trilioni.

“Ukaguzi una hatua kuu nne; kwanza CAG huwatuma wakuguzi wake kwenye maeneo husika, kisha wanamletea ripoti ya awali ikionyesha upungufu kadhaa,” alisema mtaalamu wa maendeleo, Dk Marcosy Albanie alipozungumza na Mwananchi jana.

“(Halafu) Anawatuma tena kwa mara ya pili kukagua upungufu ulioonekana, wasiporidhika wanakagua kwa mara ya tatu, kisha waandika ripoti na kuipeleka kwenye taasisi zinazokaguliwa, wanapewa siku 21 za kuweka vielelezo.

“CAG akipata vielelezo ndiyo anatoa ripoti ya nne ambayo huikabidhi kwa Rais na Bunge. Sasa kama Serikali iliyokaguliwa ilipewa siku 21 kwa nini haikuweka huo utetezi?”

Akikosoa taarifa ya Serikali bungeni, Dk Albanie alisema utaratibu wa bajeti unaotumika Tanzania ni wa kupata fedha kwanza ndipo zitumike.

“Huwezi kutumia fedha kama bado hujazikusanya, labda kama tungekuwa tunatumia utaratibu wa focus budgeting. Ukiona mpaka hatua ya nne ya ukaguzi imefika ujue hawakupeleka au walishindwa kumshawishi CAG,” alisema.

“Serikali haipaswi kutuambia sisi, bali imwambie CAG kwa sababu yeye ndiye jicho letu. CAG siyo Polisi, wala Mahakama (kiasi cha) kusema kuna wizi, ila ameuliza fedha ziko wapi?”

Hoja kama hiyo ameiona mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda.

“Hii ripoti inakuwa moto kwa Serikali kwa sababu utaratibu haukufuatwa. Tuliona tawala zilizopita mawaziri wakihangaika kulishawishi Bunge kuhusu bajeti zao, lakini siku hizi, ni tofauti,” alisema Dk Mbunda.

“Hiyo ni wake up alarm (wito wa kuamsha) kwa Serikali irudi kwenye utaratibu. Tunajua Serikali ni mpya, mawaziri wengi ni wapya, lakini wajifunze sasa.”

Katika taarifa yake, Naibu Waziri wa Fedha Dk Ashatu Kijaji alisema tofauti hiyo ilitokana na mfumo mpya unaotumiwa na TRA kukusanya mapato, fedha ambazo zilikuwa zinatarajiwa kuiva za hati fungani na fedha ambazo Serikali ilikusanya kodi kwa niaba ya Zanzibar.

Ofisi za ubalozi zafanya matumizi mabaya

Wakati mjadala huo ukiendelea, ripoti hiyo inaonyesha pia ofisi nane za umma zilifanya matumizi nje ya bajeti kwa zaidi ya Sh3 bilioni ndani ya ripoti ya CAG.

Ofisi ya ubalozi wa Tanzania jijini New York imeongoza orodha hiyo baada ya kuzidisha matumizi kwa Sh2.48 bilioni.

Ubalozi wa Tanzania, Japan ulizidisha Sh154.1 milioni na Comoro Sh26.29 milioni. Ubalozi wa Misri ulizidisha Sh5.76 milioni.

“Jambo hili lisipokomeshwa huweza kusababisha uharibifu wa shughuli zilizopangwa,” ameshauri CAG.

Ukiacha matumizi yakizidi kwenye ofisi hizo, Mhasibu wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Joyce Moshi alifanya ubadhirifu wa mamilioni mwaka huo.

Ukaguzi umeonyesha katika kipindi hicho, Sh332.85 milioni (Dola 150,000 za Marekani) zilihamishwa kutoka akaunti ya ubalozi kwenda ya ofisa huyo.