Sh48 milioni za vicoba zilivyoyeyuka Dar

Muktasari:

Wakizungumza jana, wanavikundi hao walisema fedha hizo zimeibwa katika mazingira ya kushangaza wakidai walitegemea milango, madirisha au nyumba zilimokuwa kuvunjwa lakini haikuwa hivyo.

Dar es Salaam. Utata umegubika wizi wa zaidi ya Sh48 milioni zinazodaiwa kuibwa kwenye vikundi vya Migombani Vicoba vinavyojumuisha vikundi vitatu vilivyopo Segerea jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza jana, wanavikundi hao walisema fedha hizo zimeibwa katika mazingira ya kushangaza wakidai walitegemea milango, madirisha au nyumba zilimokuwa kuvunjwa lakini haikuwa hivyo.
Mmoja wa wanakikundi, Mwanaisha Abdallah alisema walikuwa na vikundi vitatu vya vicoba ambapo fedha zote zimeibwa.

Alisema mojawapo wa kicoba kilikuwa cha mwaka mmoja na nusu ambacho kilitakiwa kivunjwe Septemba 2, kikikuwa na wanachama 30.
Mwanaisha alisema kicoba cha pili cha miaka miwili walikuwa wamekwishachangia wiki 60 na walitegemea kukivunja Februari, 2019 kikiwa na watu 30 na cha mwisho cha miaka mitatu walishachangia wiki 60 na wako watu 40.
Alisema Septemba 2 walipigiwa simu saa 10 alfajiri na mwenye nyumba zilimokuwa fedha zao, Ally Mfaume ambaye alikuwa mweka hazina akiwafahamisha kuwa wezi wamevunja nyumba yake na kuiba fedha zilizowekwa kwenye masanduku matatu.
Alisema baada ya kuelezwa hivyo, baadhi yao walielekea kwenye eneo la tukio ambapo cha kushangaza hawakuona sehemu iliyovunjwa kama ilivyodaiwa.
“Tulipofika kwenye eneo la tukio hatukuona kitu ambacho kilichovunjwa matokeo yake mwenye nyumba alidai hao majambazi waliingia ndani na kumtishia kumuua kwa kisu kama hajaonyesha masanduku matatu ya fedha yalipofichwa, ndipo aliwaonyesha wakayachukua na kukimbia nayo huku wakielekea kwenye gari lao na wengine walipanda pikipiki,” alisema Mwanaisha.
“Mimi ni mfanyabiashara wa matunda huwa nachukua Iringa na kuyauza hapa Dar es Salaam, nilikuwa na ndoto ya kununua gari aina ya Noah kwa ajili ya kufanyia biashara na nilikuwa nishaelewana na mtu tayari, basi ndoto zangu zimeshakufa.”
Alisema alikuwa anacheza majina matatu ambapo kila hisa moja ilikuwa Sh10,000 na kila wiki alikuwa anawasilisha Sh105,000.

Mwanaisha alisema alilipa hivyo kwa mwaka mmoja na nusu na alitegemea siku ya kuvunjwa kwa vicoba kupata Sh15 milioni.
Mwanakikundi mwingine, Alex Savin alisema alishangaa kusikia siku ya tukio kuwa vikundi vyao havikuwa na akaunti benki kwa kuwa ilishafungwa wakati kila walipokuwa wakikutana mwalimu wao alikuwa anawaeleza kuwa fedha zao zinahifadhiwa benki.
Mratibu wa mafunzo ya vicoba hivyo, Habiba Mgomba alisema mazingira ya kupotea kwa fedha hizo yanatatanisha.
Mgomba alisema kama mratibu anayehudhuria baada ya mwezi, alikuwa anaangalia fedha hizo zinakusanywa na kuwekwa kwenye sanduku na baadaye kupelekwa benki.
Alipotafutwa mratibu wa mafunzo ya vicoba vilivyo chini yao taasisi ya Pidcoda, Riziki Njavike alisema suala hilo limefunguliwa kesi polisi na kwa kuwa mazingira ya wizi yanatatanisha wanaendelea kufuatilia.
Njavike alisema wanakikundi hao alikutana nao juzi kwa lengo la kutaka kujua kwa nini vicoba vya Migombani hawana akaunti na inakuwaje kila mwanakikundi hana akaunti benki.
Alisema kwa maelezo ya mwalimu wa vicoba hivyo walishawahi kuwa na akaunti, lakini walifungiwa na aliwashauri kila mmoja awe na akaunti yake.
“Hairuhusiwi kukaa na hela nyingi nyumbani kwa mtu na mwalimu hilo analijua huwa tunawaelekeza wanapokutana, na wanavikundi wanatakiwa awaelekeze kuwa na akaunti kila mmoja haitakiwi fedha kuwekwa kwenye masanduku,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema tukio hilo la kuvunjwa nyumba na kuiba fedha pamoja na watuhumiwa wamekamatwa.
“Ushahidi ukipatikana wa kutosha wote waliohusika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, bado tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Hamduni.