Sh600 mil kudhibiti Ukimwi

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu , Jenista Mhagama akizungumza wakati wa kukabidhi fedha zilizotolewa na wahisani kwa  Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF), jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Waziri wa  Tamisemi,  Selemani Jaffo. Picha na Said

Muktasari:

  • Waziri wa Afya amesema msaada wa fedha za kukunua dawa za Waviu umetolewa kwa wakati muafaka

 Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF), ikishirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), imetoa Sh600 milioni kwa Wizara ya Afya kununua dawa za kupambana na magonjwa nyemelezi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya wahisani kujitoa kununua dawa hizo muhimu kwa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Waviu).

Alisema lengo la kununua dawa hizo ni kuziba pengo la gharama za kudhibiti Ukimwi kama malengo ya ATF yanavyoelekeza.

Pia, alikabidhi hundi ya Sh200 milioni kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kusaidia kujenga Kituo cha Afya Mererani.

“Licha ya Mkoa wa Manyara kuwa na idadi ndogo ya maambukizi ya Ukimwi, lakini katika eneo la Mererani ambako kuna mwingiliano wa watu kutokana na uwapo wa madini, hali ni mbaya.

“Kituo hicho mbali na kusaidia kuboresha afya za wananchi wote wa eneo hilo, kitatoa pia huduma kwa Waviu, ” alisema Mhagama.

Pia, alisisitiza wananchi kuchangia katika mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi kwa kuzindua namba maalumu, ambayo ni 909090.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema msaada huo wa fedha umetolewa wakati muafaka.

Alisema mahitaji ya fedha za kununulia dawa aina ya septrin ambayo inasaidia kupunguza magonjwa nyemelezi ni Sh2.8 bilioni kwa mwaka, hivyo fedha hizo zitasaidia kupunguza mzigo huo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini dhidi ya Ukimwi, Godfrey Simbeye alisema,“Hakuna familia inayoweza kujipambanua kuwa haijaguswa na janga la Ukimwi, hivyo kuchangia katika mfuko huo ni jukumu la kila mmoja.”