Sh651 bilioni zinahitajika kuiokoa Tazara isifilisike

Muktasari:

Matokeo ya ushindani huo kiwango cha mizigo inayosafirishwa na reli hiyo kimepungua na mapato yameporomoka huku gharama za uendeshaji zikizidi kupanda.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya marais wa Tanzania na Zambia kukutana jijini Dar es Salaam na kukubaliana kubadili sheria iliyounda Mamlaka ya Reli ya Tazara, imebainika hali ya kifedha ni mbaya na zinahitajika Dola za Marekani 300 milioni (Sh651 bilioni) kuokoa isife.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwananchi katika makao makuu ya mamlaka hayo Dar es Salaam na Lusaka, Zambia unaonyesha mapato ya Tazara yamekuwa yakipungua baada ya kukimbiwa na wafanyabiashara wengi. Nchi washirika zinatakiwa kuchangia kiasi hicho ili kurekebisha miundombinu.

Tazara imekuwa na hali mbaya tangu miaka ya 1990 kutokana na sababu tofauti. Kwanza uhaba wa mtaji wa uendeshaji ulijitokeza tangu ilipoanzishwa. Pili, sera ya ubinafsishaji wa mashirika iliyoikumba Zambia, wamiliki wapya wa migodi ya shaba hawakuona ulazima wa kusafirisha biashara zao kwa reli hiyo.

Sababu ya tatu ni kwamba baada ya Zimbabwe na Namibia kupata uhuru pamoja na kumalizika utawala wa kibaguzi Afrika Kusini, wamiliki wa migodi na wafanyabiashara wa mataifa hayo walianza kutumia Bandari ya Durban, Afrika Kusini badala ya Bandari ya Dar es Salaam.

Pia, hadi sasa wafanyabiashara wengine husafirisha mizigo yao kwa malori ambayo imeelezwa yanatumia muda mfupi kufika eneo husika kuliko reli. Hivyo, Tazara ilianza kushindana na malori kusafirisha mizigo.

Matokeo ya ushindani huo kiwango cha mizigo inayosafirishwa na reli hiyo kimepungua na mapato yameporomoka huku gharama za uendeshaji zikizidi kupanda.

 

Anguko la Tazara

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa kipindi mwaka 1986/87 usafirishaji ulifikia kiwango cha tani za mizigo 1.2 milioni wakati matarajio yalikuwa tani milioni tano kwa mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na mamlaka hiyo, kuanzia mwaka 2010 hadi 2016 imesafirisha mizigo ambayo haifiki hata wastani wa tani milioni moja kwa mwaka, kwani imeshuka kutoka tani 533,679 mwaka 2010/11 hadi tani 128,105 mwaka 2015/16.

Mwaka 2014/15 ndiyo ulikuwa mbaya zaidi katika historia ya Tazara baada ya kuambulia tani 87,860 tu za mizigo wakati mwaka 1994 ilisafirisha tani 600,000.

Mwenendo wa takwimu hizo unafanana na zile za Ofisi ya Takwimu za Taifa (NBS) licha ya kuwa zinatofautiana kidogo na zile za Tazara. Katika ripoti ya takwimu muhimu za mwaka 2015, NBS inaeleza kuwa mizigo ya Tazara imeshuka kutoka tani 540,000 mwaka 2010 hadi tani 130,000 mwaka jana.

Pamoja na rekodi kuonyesha Zambia, mshirika mkuu wa reli hiyo, imeagiza mizigo ya tani 1.9 milioni kutoka nje kwa mwaka huu lakini ni sehemu ndogo imesafirishwa kwa Tazara, huku wafanyabiashara wengi wakitumia usafiri wa barabara.

Takwimu kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), zinaonyesha mizigo inayobebwa kwa Tazara kutoka bandarini imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 2.69 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 0.18 mwaka 2015.

Pia, kwa mizigo iliyobebwa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) ilikuwa asilimia 0.64 mwaka 2011 na mwaka 2015 ilikuwa asilimia 0.12.

Aidha, malori ambayo yanabeba sehemu kubwa ya mizigo yameendelea kuongeza kiwango cha uchukuzi; mwaka 2011 ilikuwa asilimia 96.67, mwaka 2014 asilimia 99.8 na asilimia 99.7 mwaka 2015.

Kwa upande wa abiria, wamepungua kutoka 786,759 mwaka 2010/11 hadi abiria 414,746 mwaka 2015/16.

 

Mapato chini

Kutokana na kupungua kwa mizigo, mapato nayo yamekuwa yakishuka huku vitabu vya kifedha vya Tazara vikionyesha kuwa ndani ya miaka minne mapato ya mamlaka hiyo yalishuka mara tatu kutoka Sh48.53 bilioni mwaka 2012 hadi Sh15.4 bilioni mwaka jana.

Mbali na kushuka kwa mapato, Tazara inakabiliwa na madeni lukuki na hadi Juni mwaka huu, gazeti la The Citizen lilieleza kuwa takriban Sh94 bilioni kutoka kwa taasisi mbalimbali zikiwemo TRA na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Ili Tazara ijiendeshe kwa faida inahitajika isafirishe mizigo kati ya tani 650,000 hadi tani 700,000 kwa mwaka lakini sasa haizidi hata tani 150,000.

Mkurugenzi Mkuu wa Tazara, Bruno Ching’andu aliyechukua nafasi ya Ronald Phiri alikiri kushuka utendaji wa Tazara lakini akasema kwa sasa wameanza kufanya marekebisho ya miundombinu ya reli na treni ili kupunguza muda unaotumika safarini.

“Tumebadilisha mambo kadhaa hapa. Kwa mwaka uliopita utendaji wetu umekuwa mzuri. Kwa mfano, zamani ungechukua siku 30 kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Kapiri Mposhi, lakini sasa tunachukua siku nne hadi saba. Haya ni mafanikio makubwa na wateja wameanza kurudi. Kwa treni ya abiria iliyokuwa ikichukua siku saba, sasa inachukua saa 48,” alisema.

Alisema mafanikio hayo ni mara saba ya utendaji uliokuwapo awali ambapo treni ilikuwa ikichukua muda mrefu kutokana na ubovu wa reli.

“Kulikuwa na vikwazo 52 vya mwendo, sasa tumevipunguza hadi 19 na mwisho wa mwaka huu tutafikisha vikwazo 13. Katika vikwazo hivyo treni ilikwenda kwa mwendo wa kilometa 10 kwa saa kutokana na ubovu wa reli,” alisema.

Ching’andu alisema kuwa wamepunguza muda wa upatikanaji wa mabehewa ya kubeba mizigo kwa wateja kutoka wiki mbili hadi saa 24 hadi 48.

Akizungumzia ushindani uliopo kati ya Tazara na wasafirishaji wengine hasa TRL na wamiliki wa malori, Ching’andu alisema huo ni ushindani wa kawaida na kwamba Tazara ilikuwa ikipoteza wateja wake kutokana na gharama za usafiri zilizosababishwa na ongezeko la kodi, lakini kwa sasa wamepunguza gharama.

“Kwanza Tazara isichukuliwe kuwa kama njia pekee ya usafirishaji wa mizigo na abiria. Inapambana na kampuni nyingine za usafirishaji. Wafayabiashara wanachagua njia ya usafiri kulingana na gharama za usafirishaji. Kuna wakati Tanzania ilionekana kuwa ghali kwa sababu kodi zilikuwa juu, lakini sasa tumepunguza baada ya kuangalia mwenendo wa kodi, sasa zinaeleweka,” alisema.

 

Kurudi Wachina

Kuhusu hatua ya Serikali ya China kuifufua Tazara, Mkurugenzi alisema kuwa Wachina wamekuwapo katika mamlaka hiyo kwa muda wote wa uhai wake na sasa kuna majadiliano yanaendelea ili kuona wataiokoaje isife kabisa.

“Kama ni Wachina wamekuwa hapa muda wote, wamewekeza mitaji yao hapa muda wote, kuna itifaki 15 kati yetu na China kwa miaka zaidi ya 30 ya shirika hili. Hakuna kitu kipya,” alisema.

“Ngoja niweke sawa. Kuna majadiliano kati ya China na nchi hizi mbili kuhusu uendeshwaji wa shirika hili. Majadiliano bado hayajafikia mwisho ili kujua ni ushirikiano gani utakaokuwa. Unaweza ukawa wa ushirikiano, unaweza kuwa wa kiutawala, unaweza ukawa wa maridhiano. Majadiliano yakiisha tutajua.”

 

Marais wa Tanzania, Zambia

Februari 2015 Rais mstaafu Jakaya Kikwete alikwenda Zambia kwa majadiliano na Rais Edgar Lungu kuhusu namna ya kufufua shirika hilo. Wiki hii kilifanyika kikao kingine kati ya Rais John Magufuli na Lungu jijini Dar es Salaam kujadili, pamoja na mambo mengine suala la Tazara.

Katika taarifa yao ya pamoja, Rais Magufuli alisema nchi mbili hizo zimekubaliana kuifumua menejimenti ya Tazara ili kuruhusu watu wengine wenye uwezo kutoka nje kufikiriwa katika nafasi ya menejimenti.