Thursday, March 9, 2017

Sh70 milioni zachangia mafunzo Mbeya

 

Mbeya. Halmashauri saba zimetoa Sh10 milioni kila moja hivyo kukusanya Sh70 milioni kulipia mafunzo ya wafanyabiashara na wajasiriamali wanaosindika bidhaa ili waziboreshe zipate alama ya msimbomlia (barcode).

Mafunzo hayo yanatolewa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kuziagiza halmashauri zote kutoa kiasi hicho cha fedha ili kuwalipia wafanyabiashara na wajasiriamali wao wafundishwe jinsi ya kuboresha bidhaa na kupata alama hiyo kwa uratibu wa Kampuni ya GS1 TZ National.

Akizungumzia mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi mkoani hapa anayeshughulikia kilimo, Chibagu Nyasebwa aliwataka wajasiriamali katika kila halmashauri kujitokeza kwa wingi kwenye mafunzo hayo.

“Wajasiriamali wanachotakiwa ni kufika kwenye kumbi za mafunzo hayo kwani yameshalipiwa na halmashauri zao,’’ alisema.

Nyasebwa alisema Halmashauri ya Chunya ilikuwa ya kwanza kutoa fedha hizo na kwamba, wafanyabiashara na wajasiriamali wake ni wa kwanza kupata mafunzo yaliyoanza jana hadi Machi 11.

Kati ya Machi 14 na Machi 16, mafunzo kama hayo yatafanyika Kyela na baadaye Rungwe, Busokelo, Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Mbeya.

Meneja Masoko wa Kampuni ya GS1 TZ National, Oscar Ruhasha alisema wamejipanga kuwafundisha wajasiriamali zaidi ya 200 kwa kila halmashauri.

Ruhasha alisema wajasiriamali hao watafundishwa mambo mbalimbali kutoka kwa maofisa wa TFDA, Sido, TRA, TBS, TCCIA, Tirdo, Tantrade, PPF na Benki ya CRDB. “Tumewaita wadau hao ili watoe elimu na mwisho tunawafundisha jinsi ya kupata barcode,’’ alisema.

-->