VIDEO-Mazishi ya Akwilina kugharimu Sh80 milioni

Muktasari:

Kifo cha Akwilina kilitokea Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji jijini Dar es Salaam.


 Ndugu wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline wamesema mazishi ya mwanafunzi huyo yatagharimu Sh80milioni.

Akizungumza na MCL Digital leo Februari 20, 2018 msemaji wa familia, Festo Kavishe amesema baada ya kukaa kikao cha familia pamoja na viongozi wa Serikali wamepitisha kiasi hicho cha fedha.

“Bajeti ya mazishi itakuwa Sh70milioni hadi Sh80milioni. Familia ilikaa na katibu mkuu wa wizara ya elimu na mkuu wa wilaya ya Ubungo,” amesema Kavishe.

Amesema pia walijadili ratiba ya mazishi hayo, ikiwemo ratiba ya kuaga mwili wa mwanafunzi huyo Februari 22, 2018 katika viwanja vya chuo cha NIT.

Kavishe amewatahadharisha watu mbalimbali kutochanga fedha kwa ajili ya msiba huo katika mitandao mbalimbali, kuwataka kufika nyumbani kwa ndugu wa marehemu eneo la Mbezi Louis ambako ndiko unakofanyika msiba ili kuwasilisha rambirambi zao.

Hayo yamezungumzwa leo baada ya Serikali na ndugu wa marehemu kufanya kikao cha pamoja kujadili kuhusu taratibu za mazishi na gharama zake.

Kufuatia gharama hizo, Serikali imesema inakwenda kujadili kuhusu gharama hizo na jioni watarudi kwa familia kuleta mrejesho kuhusu gharama hizo.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo amesema wanakwenda kujadiliana kuona namna wanavyoweza kuchangia gharama hizo.

"Mpaka sasa tumekubalina na familia tutaaga mwili wake Alhamisi katika chuo cha NIT saa saba mchana na kusafirishwa nyumbani kwao kwaajili ya maziko," amesema Dk Akwilapo.

Amesema makubaliano hayo bado hayajafikia tamati na wanazidi kuwasiliana na taasisi nyingine za kiserikali ili kuweza kufanikisha msiba huo.

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.