Shafii Dauda apandishwa kizimbani, aachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Dauda na mwenzake wanadaiwa  kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Shafii Dauda,   kinyume cha sheria  kutuma maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)

Dar es Salaam. Benedict Kadege  na mtangazaji Shafii Dauda wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kutumia maudhui mtandaoni bila kuwa na kibali.

Wamepandishwa kizimbani leo mchana Jumatatu Septemba 24, 2018.

Wakili wa serikali Mkuu,  Tumaini Kweka akishirikiana na mawakili Mutalemwa Kishenyi na Mwanaamina Kombakono wamewasomea shtaka hilo washtakiwa hao mbele ya hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina.

Akisoma shtaka hilo wakili Kombakono amedai  kati ya Juni 14  hadi Septemba, 2018 jijini Dar es Salaam kwa kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Shafii Dauda,   kinyume cha sheria  walitoa maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa hao walikana na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo,  wakili Jebra Kambole anayewatetea washtakiwa hao ameomba wateja wake wapewe dhamana kwa sababu shtaka linadhaminika.

Kweka amedai hawapingi kutoa dhamana ila kama mahakama itaridhia kutoa dhamana izingatie kifungu cha 148 (6)(7) cha sheria ya makosa ya jinai.

Akitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao,  Hakimu Mhina alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili kwenye vitambulisho vya kuwatambulisha na barua ambazo zinatambulika.

Pia,  kila mdhamini alitakiwa kusaini bondi ya Sh15milioni na kutoruhusiwa kusafiri nje ya Tanzania bila kupata kibali cha mahakama huku wakitakiwa Oktoba 8, 2018 kuwasilisha mahakamani hati zao za kusafiria.

Washtakiwa hao wamepata dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi  Oktoba 8, 2018 itakapotajwa tena.