KESI YA MAUAJI YA BILIONEA MSUYA-Shahidi: Mahabusu Moshi ni ‘Self Contained’

Mawakili wa upande wa utetezi  wakifunga nyaraka za ushahidi mbalimbali baada ya kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya kuahirishwa jana. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

Mbali na kauli hiyo, Kapusi ambaye ni mkaguzi wa polisi, alisema kila gwaride aliloliendesha kati ya magwaride matatu dhidi ya mshtakiwa wa saba, Ally Mussa maarufu Mjeshi, alitumia sekunde 60.

Moshi. Msaidizi wa mkuu wa upelelezi wilaya ya Moshi (OC-CID), Bernard Kapusi, ameieleza mahakama kuwa chumba cha mahabusu ya kituo kikuu ni “self contained” akimaanisha kina choo ndani yake.

Mbali na kauli hiyo, Kapusi ambaye ni mkaguzi wa polisi, alisema kila gwaride aliloliendesha kati ya magwaride matatu dhidi ya mshtakiwa wa saba, Ally Mussa maarufu Mjeshi, alitumia sekunde 60.

Kapusi ambaye ni shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya, alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu maswali ya mawakili wa utetezi.

Shahidi huyo alikuwa akihojiwa na mawakili wa utetezi kutokana na ushahidi wake alioutoa jana na juzi, alieleza kuwa wakati gwaride linafanyika, mshtakiwa alitokea katika mahabusu hiyo.

Jopo la mawakili wa utetezi wanaowatetea washtakiwa saba, linaongozwa na John Lundu anayesaidiana na Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Aloye Kamara na Emmanuel Safari.

Kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi, inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi huku jopo la upande wa mashtaka likiundwa na wakili wa Serikali mkuu, Peter Maugo anayesadiana na wenzake watatu.

Akijibu maswali ya wakili Magafu, shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa siku hiyo ya gwaride Oktoba 7, 2013, mshtakiwa alichanganywa na washiriki tisa na kufanya jumla ya waliopangwa kuwa 10.

Shahidi huyo aliendelea kuwa washiriki wa gwaride hilo walikuwa na wajihi, umbo, sura, mavazi na umbo vilivyokuwa vikiendana na mshtakiwa, ambaye wakati huo alitolewa kutoka mahabusu.

“Katika hili gwaride la utambulisho, hao washiriki walitoka sehemu mbalimbali. Wengine walitokea lock-up (mahabusu) kama mshtakiwa na wengine walikuwa ni wapita njia tu,” alieleza.

Wakili Magafu alimuuliza shahidi huyo kama kabla ya kuanza kwa gwaride aliwahi kuzungumza na mshtakiwa huyo na kumuuliza kama alikuwa amekaa mahabusu muda gani na kama alikuwa ameoga.

“Sikumuuliza kama amekaa muda gani mahabusu wala sikumuuliza kama ameoga siku hiyo, lakini ninachojua washiriki waliendana na mshtakiwa na bahati nzuri choo chetu ni self contained,” alidai shahidi huyo.

“Kule (mahabusu ya kituo kikuu Moshi) hatutunzi watu wachafu na ana nafasi ya kuoga. Chumba chetu ni self contained (kina huduma ya choo ndani), kwa hiyo alifanana na washiriki,” alisisitiza.

Shahidi huyo alidai kuwa mashahidi watatu walimtambua mshtakiwa kuwa alifika na kuzungumza na marehemu katika hoteli yake ya SG Resort ya jijini Arusha, siku moja kabla ya kuuawa kwake.

Alipoulizwa na wakili Magafu kama maelezo hayo ya utambuzi aliyaandika katika fomu namba PF 186, ambayo ni rejista ya polisi ya gwaride la utambulisho, alieleza kuwa hakuyaandika maelezo hayo.

Hata hivyo, maswali ya wakili Magafu na wenzake yalijikita katika muda wa kufanya magwaride yote matatu, ambayo yalionekana kufanyika na kukamilika chini ya sekunde 60.

Gwaride la kwanza kwa mujibu wa fomu hiyo PF 186, lilifanyika na kukamilika saa 10:55 alasiri, la pili likafanyika na kukamilika saa 11:00 alasiri na gwaride la tatu likafanyika na kukamilika saa 11:19.

“Hili gwaride la kwanza lilianza saa 10:55 na ndani ya muda huo huo likakamilika. Yaani lilianza sekunde 00 na ilipofika sekunde ya 55 likakamilika. Hayo mengine ni ndani ya dakika moja.

“Huu muda wa dakika moja wa gwaride ni kuanzia shahidi anafika, anajitambulisha, ninawauliza washiriki kama wana pingamizi au shaka, anazunguka kuwakagua na kumtambua mshtakiwa,” alieleza.

Alipoulizwa na wakili Magafu kama anataka kuishawishi mahakama iamini hayo yote aliyafanya ndani ya dakika moja na si kwamba gwaride halikufanyika na fomu aliijazia ofisini, alidai kuwa muda ulitosha.

Akihojiwa na wakili Emmanuel Safari, shahidi huyo alidai katika eneo alilokuwa akifanyia gwaride hilo ambalo ni uani mwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, hakuna mtu aliyekuwa katika jengo la ofisi.

“Katika eneo nililokuwa nafanyia hakuna mtu aliyekuwa ofisini. Shughuli zote zilisimama kwa muda huo. Wala hakuna mtu aliyekuwa anaweza kuona hata akiwa ofisini kwa vile kuna mapazia,” alieleza shahidi huyo na kuongeza:

“Watu wote waliondolewa kwenye eneo hilo lililokuwa limeandaliwa kwa gwaride la utambulisho. Hali ya afya ya mtuhumiwa ilikuwa njema kabisa na wala hakuwa na jeraha lolote.”

Wakili Safari akamrejesha kwenye ushahidi wake kuwa kati ya sekunde 00 hadi sekunde ya 60 gwaride lilikuwa limekamilika, hivyo akamuuliza kama ana stop watch (saa) akadai hakuwa nayo.

Kwa upande wake, wakili John Lundu alimuuliza shahidi huyo kama si kwamba gwaride halikufanyika na rejista hiyo aliijaza tu ofisini na kubadilisha nafasi aliyosimama mshtakiwa, alikanusha madai hayo.

Pia, shahidi huyo alikanusha madai ya wakili huyo ya kuwapo uwezekano wa kuwasiliana kwa simu na mashahidi na kuwaelekeza mtu wa kumtambua, akisisitiza mashahidi walimtambua pasipo na shaka.

Hata hivyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula alipopata nafasi ya kumuuliza shahidi wake maswali ya ziada, shahidi huyo alikanusha vikali madai kuwa gwaride hilo halikufanyika.

Shahidi huyo alidai kuwa Kanuni za Polisi (PGO), hazijaweka sharti la lazima linalomtaka aandike muda wa kuanza na kumaliza gwaride na alichokiandika kwenye PF186 ni muda gwaride lilipofanyika.

Kuhusu mawakili wa utetezi waliohoji sababu za watu walioshiriki gwaride hilo hawakubadilishwa kila baada ya gwaride, shahidi huyo alieleza hakuna kifungu cha PGO kinacholazimisha jambo hilo.

Shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi wake hiyo jana na leo upande wa mashtaka utaita shahidi mwingine kuendelea kutoa ushahidi kujenga kesi ya upande wa mashtaka.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa kesi wakili wa Serikali mkuu, Peter Maugo anayeongoza jopo la waendesha mashtaka, alieleza kuwa shahidi wao mwingine aliyekuwa atoe ushahidi wake jana ni mgonjwa.

Maugo alimweleza Jaji Maghimbi kuwa ingawa shahidi huyo, mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP), Vincent Lyimo alikuwa tayari kutoa ushahidi wake ni vyema akaruhusiwa kuondoka hadi siku nyingine.

Wakati wakili huyo akitoa maelezo hayo, shahidi huyo alikuwa amesimama mbele ya Jaji, huku mkono wake wa kulia ukiwa na kifaa maalumu (canula) cha kupitisha dawa kwenda kwenye mishipa ya damu.

“Tungeiomba mahakama imruhusu na kumpa siku nyingine ingawa amesema yuko tayari kutoa ushahidi wake, lakini kwa tatizo hilo la afya aweze kutoa keshokutwa (Alhamisi),” aliomba wakili Maugo.

Jaji Maghimbi alikubali ombi hilo na kumuonya shahidi huyo kuwa awepo hiyo kesho kwa vile tayari kumbukumbu za mahakama za kesi hiyo, zimeshaingia kuwa atatoa ushahidi siku hiyo.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kwa kutumia bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi inawakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed na Ally Mussa.