Shahidi Wambura asema muhtasari kubadili watia saini TFF ulighushiwa

Muktasari:

  • Wambura, shahidi wa pili wa upande wa mashtaka alieleza hayo jana mahakamani akitoa ushahidi akiongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro katika kesi inayomkabili aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wanne.

Dar es Salaam. Ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura (49), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa muhtasari wa Juni 5, 2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za benki za TFF zilizopo Stanbic ni wa kughushi.

Wambura, shahidi wa pili wa upande wa mashtaka alieleza hayo jana mahakamani akitoa ushahidi akiongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro katika kesi inayomkabili aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wanne.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alidai anaeleza hayo kwa sababu alikuwapo kwenye kikao cha Juni 5, 2016.

Alidai hapakuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.

Wambura alidai Masoud alikuwa mkurugenzi wa fedha na utawala TFF lakini sasa ni marehemu. Alifariki dunia mwaka jana.

Alidai mchakato ulitakiwa kupelekwa kama ajenda ukieleza sababu za kutaka kufanya mabadiliko ya watia saini katika kamati ya utendaji ambayo ikiridhia mabadiliko hufanyika.

Awali, Wambura ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka alidai akiwa ofisa mtendaji mkuu wa bodi ya ligi tangu Juni 2015, majukumu yake yalikuwa kusimamia shughuli za ligi. Pia, ni mjumbe wa sekretarieti ya TFF ambayo inawezesha vikao vya kamati ya utendaji kufanyika.

“Mwaka 2016 kamati ya utendaji ilikuwa na wajumbe wasiopungua 20 na wasiozidi 24, utaratibu wa ufanyaji vikao kinaitwa na mwenyekiti na kuwapelekea ajenda wajumbe,” alieleza Wambura.

Alidai nyaraka za ajenda zinaandaliwa na sekretarieti chini ya katibu mkuu na rais ambaye ndiye msimamizi wa sekretarieti.

Wakati vikao vikifanyika, alisema sekretarieti chini ya katibu mkuu huchukua muhtasari ambao huwasilishwa kikao kinachofuata kwa ajili ya kuthibitishwa na kusainiwa na mwenyekiti ambaye ni rais wa TFF au makamu wake. Alisema mwaka 2016 aliyekuwa mwenyekiti ni Malinzi.

Wakili Kimaro alimuonyesha Wambura muhtasari wa Juni 5, 2016 ukionyesha yeye ni miongoni mwa wajumbe wa sekretarieti waliohudhuria kikao.

Baada ya kuupitia muhtasari huo aliokabidhiwa, Wambura alidai umeghushiwa na haufahamu kwa sababu alikuwapo kikaoni na hapakuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa TFF.

Akihojiwa na mawakili wa utetezi alidai wakati Malinzi akiwa rais wa TFF, alikuwa akilipwa mshahara wa Sh2 milioni na baada ya kuondoka madarakani sasa analipwa Sh7 milioni.

Alieleza hayo akihojiwa na wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza iwapo aliwahi kupeleka maombi ya kuongezwa mshahara kwa Malinzi.

Sehemu ya mahojiano kati ya Rweyongeza na Wambura ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Ulipeleka maombi upate Sh7 milioni kwa mwezi kwa Malinzi akakukatalia?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Ni kweli wakati Malinzi akiwa madarakani alikataa nyongeza hiyo?

Shahidi: Si kweli.

Wakili: Sasa hivi ni kweli unapata Sh7 milioni kwa mwezi?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Hizi Sh7 milioni zimeidhinishwa na rais wa sasa wa TFF baada ya kutoka Malinzi madarakani?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Kwa mantiki ya kawaida chini ya rais wa zamani na wa sasa wewe upo vizuri zaidi?

Shahidi: Nipo vizuri kikazi.

Wakili: Mshahara wa katibu mkuu wa TFF unaufahamu?

Shahidi: Siufahamu?

Wakili: Bodi ya ligi ipo chini ya TFF, nikisema katibu mkuu wa TFF ni mkubwa kwako?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Una habari unamzidi mshahara?

Shahidi: Sina habari.

Wakili: Unaweza kutaja nyadhifa ulizopitia TFF 2011 na 2013?

Shahidi: Ofisa habari na mawasiliano wa TFF, TMS meneja, mkurugenzi wa mashindano na niliwahi kukaimu ukatibu mkuu wa TFF, Novemba 2013 hadi Desemba 31, 2013.

Wakili: Wakati huo nani walikuwa watia saini wa TFF.

Shahidi: Boniface Wambura, Jamal Malinzi, Wallace Karia na Yonaza Seleki wakati nakaimu ukatibu mkuu TFF.

Wakili: Kamati ya utendaji ni kikao gani ilikaa kuwateua ninyi kuwa watia saini wa TFF?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Na wewe ndiye ulikuwa katibu na mtia saini na wenzako?

Shahidi: Ni kweli nilikuwa katibu wa vikao vyote.

Wakili: Wewe ndiye uliyejaza fomu za kwenda benki kubadilisha mtia saini wa benki kama katibu mkuu wa TFF?

Shahidi: Sikumbuki.

Kesi imeahirishwa hadi Mei 28 na 29 kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Malinzi (57), Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine (46) na mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27), meneja wa ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na karani wa TFF, Flora Rauya.

Wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 wakiwa na mashtaka 30 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha.