Shahidi adai saini za marehemu zilighushiwa

Kiwanja ambacho kimeingia katika mgogoro kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Taasisi ya Mawenzi Sports Club ambapo wadhamini wawili wa taasisi hiyo wameshitakiwa kortini kwa madai ya kugushi saini za marehemu ambazo zilisaidia kutwaliwa kwa kiwanja na ofisi za Serikali ya Kata ya Mawenzi katikati ya mji wa Moshi.

Muktasari:

  • Shahidi huyo, Fikiri Temakunji ambaye ni mtaalamu wa maandishi kutoka Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi, anakuwa shahidi wa tatu baada ya Mbunge wa Moshi mjini, Jaffar Michael kutoa ushahidi wake mwezi uliopita.

Moshi. Shahidi wa upande wa mashitaka katika kesi ya kughushi saini za marehemu waliokuwa wadhamini wa taasisi ya Indian Sports Club, ameiambia mahakama uchunguzi wa kimaabara ulithibitisha saini hizo kughushiwa.

Shahidi huyo, Fikiri Temakunji ambaye ni mtaalamu wa maandishi kutoka Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi, anakuwa shahidi wa tatu baada ya Mbunge wa Moshi mjini, Jaffar Michael kutoa ushahidi wake mwezi uliopita.

Michael, ndio kiini cha kuanzishwa uchunguzi wa sakata hilo mwaka 2015 wakati huo akiwa Meya wa Manispaa ya Moshi, baada ya kuziandikia mamlaka za uchunguzi akizitaka kuchunguza sakata hilo.

Kughushiwa saini hizo za kuanzia mwaka 1970 hadi 2007 ndiko kunakodaiwa kulisaidia kukamilishwa mchakato wa kutwaa kiwanja cha Serikali kilichopo katikati ya mji wa Moshi, eneo la kibiashara.

Kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi wa Moshi, inawahusu wafanyabiashara wawili mashuhuri mjini Moshi, Hitesh Solan na Amratlal Pattni wanaokabiliwa na mashitaka 75 ya kughushi nyaraka.

Solan na Pattni ambao ni wadhamini wa Taasisi ya Mawenzi Sports Club ambayo zamani ilijulikana Indian Sports Club, wanadaiwa kughushi nyaraka hizo za kuanzia mwaka 1970 hadi 2007.

Saini wanazodaiwa kughushi ni za wadhamini wa zamani wa taasisi hiyo, Devchand Shah aliyefariki dunia mwaka 1979 na Mohamed Shariff, aliyefariki mwaka 1998.

Kiwanja hicho namba LO 9850 chenye hati namba 10660 ambacho kilikuwa ofisi ya Serikali Kata ya Mawenzi kwa zaidi ya miaka 20, kilichukuliwa na baadaye kuuzwa kwa mfanyabiashara tajiri wa Moshi.

Akitoa ushahidi juzi mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Jullieth Mawolle, Koplo Fikiri alisema uchunguzi ulibaini nyaraka za taasisi hiyo zilizopelekwa kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) ziligushiwa.

Alisema alipolinganisha nyaraka hizo, aligundua saini zilizopo kwenye nyaraka bishaniwa kwa maana za 1970 hadi 2007 ni tofauti na saini za watu hao walizozisaini kati ya 1961-1965.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Kassim Nassir, shahidi huyo alisema uumbaji herufi (letter formation) na mwandiko (writing skills), zinatofautiana katika saini hizo.

Awali shahidi wa pili katika kesi hiyo, Peter Kimaro ambaye ni Diwani Kata ya Rau (Chadema), alisema Desemba 31, 2013 waliletewa taarifa kuwa kuna watu wanataka kuchukua kiwanja hicho.

“Hatukujua ni nani hasa wanaokitaka hicho kiwanja na jengo ambalo Serikali ilikuwa inalitumia kwa karibu miaka 30 mfululizo. Tulimshauri Meya aunde kamati ndogo ya kufuatilia,” alisema.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, yeye ni miongoni mwa wajumbe walioteuliwa kuingia katika kamati hiyo na Januari 22, 2015 Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi liliridhia kamati ianze kazi.

Alisema katika utafiti walioufanya, waligundua kuwa anayekitaka kiwanja hicho ni taasisi iitwayo Mawenzi Sports Club, hivyo alitumwa Rita jijini Dar es Salaam kutafuta uhalali wake.

Shahidi huyo alidai Februari 9, 2015, aliwasilisha barua Rita ya kuomba nyaraka za taasisi hiyo na alikabidhiwa nyaraka zote ambazo aliziwasilisha kwenye kamati

“Tulipopitia nyaraka hizo tuligundua hiyo taasisi ilijianzisha kama Indian Sports Club mwaka 1950 ikiwa na wadhamini waliotajwa kuwa ni Devchand Shah na Mohamed Ladak”.

“Baadaye mwaka 1964 walimuongeza mtu anayeitwa Mohamed Shariff kuchukua nafasi ya Ladak ambaye alifariki. Tuligundua hawakuwasilisha returns (taarifa) Rita tangu mwaka 1965.

“Returns za 1970 hadi 2007 zikiwa ni jozi 14 zikapelekwa zote kwa mkupuo mwaka 2012 na kupokelewa na maofisa wa Rita na zote zikagongwa muhuri wa kupokelewa wa Novemba 22, 2012”.

Shahidi huyo alisema katika kuzipitia nyaraka hizo waligundua pia sahihi za wadhamini hao zilisainiwa kwa lugha ya kigujrati tofauti na zile zilizosainiwa na wadhamini mwaka 1961-1965.

Aliiambia mahakama taasisi ya Indian Sports Club na baadaye Mawenzi Sports Club ilishakufa na hawakuwa na uhalali wa kupewa kiwanja ambacho halmashauri ilikitumia kwa miaka zaidi ya 20.

Kutokana na viashiria hivyo vya kuwapo kwa jinai, walimuagiza Meya wa wakati huo ambaye sasa ni mbunge, Jaffar Michael kulipeleka suala hilo polisi ili waweze kufanya uchunguzi wao.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, mawakili Caessar Shayo anayemtetea Solan na Colman Ngallo anayemtetea mshitakiwa wa pili, Pattn) walimhoji shahidi huyo kama ifuatavyo:

Wakili Shayo: Ulishawahi kumuona Mohamed Ladak?

Shahidi: Sikuwahi kufahamiana naye.

Wakili Shayo: Tunaomba uiambie mahakama kama uliwahi kufahamiana na Shah.

Shahidi: Sikuwahi kumfahamu.

Wakili Shayo: Kwa hiyo kwa kuwa hukuwahi kuwafahamu, huwezi kusema hizi ni saini zao?

Shahidi: Siwezi kusema.

Wakili Shayo: Umesema mlijadili hili jambo kwenye kamati. Kwenye hivyo vikao huwa kuna maelekezo au muhtasari?

Shahidi: Kunakuwa na minutes (mihtasari).

Wakili Shayo: Kuna minutes zozote umeleta kuthibitisha uliteuliwa kuwa kwenye kamati? Pia, Kuna ushahidi wowote kama tiketi ya basi umeleta hapa kuthibitisha ulifika Rita tarehe 9.2.2015?

Shahidi: Sijaleta.

Wakili Shayo: Ni kweli hizi nyaraka zilizofanyiwa uchunguzi na polisi na hawa (washitakiwa) wakashitakiwa nyie ndio mliwapatia polisi?

Shahidi: Ndio ni sisi tuliwapatia polisi.

Wakili Shayo: Ukiwa unahojiwa na wakili wa Serikali unasema taasisi hii haipo, kwani ulishawahi kufanya kazi Rita?

Shahidi: Sijawahi kufanya kazi Rita.

Wakili Shayo: Wewe kama diwani, unaweza kusema hii taasisi ipo au haipo?

Shahidi: Hapana.

Wakili Shayo: Mna ushahidi wowote kuwa manispaa inamiliki eneo hilo?

Shahidi: Hatuna documents (nyaraka). Baadaye ilifika zamu ya Wakili Ngallo kuuliza maswali ya kuhoji.

Wakili Ngallo: Unasema uliagizwa uende Rita, zile returns (taarifa) za mwaka 1965 kurudi nyuma uliziona?

Shahidi: Ndio niliziona.

Wakili Ngallo: Zilikuwa zimesainiwa na nani?

Shahidi: Kuanzia 1950 hadi 1965 zilisainiwa na Shah na Ladak.

Wakili Ngallo: Zile za 1970 hadi 2007 ni nani alikuwa amesaini?

Shahidi: Zilikuwa zimesainiwa ki Gujrati mimi na wewe hatuwezi kufahamu.

Wakili Ngallo: Mtu anayefahamu ki Gujrati anaweza kufahamu?

Shahidi: Angeweza kusoma.

Wakili Ngallo: Wewe hizi returns ulizikuta Rita. Kwa maana nyingine Rita walizikubali hizo nyaraka ndio maana wakazipokea.

Shahidi: Mimi nilizipokea tu kama nyaraka.

Wakili Ngallo: Uliweza kuwauliza Rita katika kipindi hicho ni nani walikuwa wadhamini?

Shahidi: Sikuuliza kazi yangu ilikuwa kuchukua documents (myaraka).

Katika kesi hiyo namba 386/2017 yenye mashtaka 75, washitakiwa wanadaiwa kughushi na kuwasilisha nyaraka za kughushi ofisi ya Rita kwa ajili ya marejesho (returns) za kila mwaka.

Nyaraka hizo za kuanzia mwaka 1970 hadi 2007 zinadaiwa zilighushiwa saini za wadhamini wa taasisi hiyo ambao ni marehemu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Oktoba 23, ambapo upande wa mashtaka unakusudia kuita mashahidi watatu kutoa ushahidi wao.