Wednesday, February 14, 2018

Shahidi wa 20 awapa wakati mgumu mawakili

Wakili wa utetezi wa watuhumiwa wa mauaji wa

Wakili wa utetezi wa watuhumiwa wa mauaji wa Bilionea Erasto Msuya, Majura Magafu (kushoto) akiwafafanulia waandishi wa habari kuhusu vifungu vya sheria, kwenye chumba cha Mahakama Kuu kanda ya Moshi, kabla ya kesi ya mauwaji hayo haijaanza kusikiliza jana. Picha na Dionis Nyato 

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Shahidi wa 20 wa upande wa mashtaka, Celestine Mtobesya, jana aliwapa wakati mgumu mawakili wa upande wa utetezi katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Erasto Msuya, wakati wa kujibu maswali.

Hali hiyo ilimlazimu Jaji Fatma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, kuingilia kati mara kwa mara ama kutoa ufafanuzi wa aina ya swali aliloulizwa au kumlazimisha kujibu maswali ya mawakili hao.

Shahidi huyo ambaye ni kiongozi wa mawakala wa kusajili laini za Airtel Kanda ya Kaskazini alikuwa akitoa ushahidi wake kuhusiana na laini nne za simu zinazodaiwa kusajiliwa kinyume cha taratibu.

Laini hizo zilizokuwa na majina ya Kimasai ndizo baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka waliotangulia wanadai zilisajiliwa kwa maelekezo ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed.

Namba za simu ndizo zinazodaiwa kutumika wakati wa mipango ya mauaji ya bilionea Msuya na baada ya mauaji hayo laini hizo zilikoma kutumika.

Kwanza shahidi huyo alianza kutoa ushahidi wa msingi kwa kuongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana, lakini hali ilibadilika wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi, Majura Magafu.

Katika ushahidi wake, alisema utaratibu wa kusajili laini za simu ulikuwa ni lazima mteja afike mwenyewe kwa wakala (in person) akiwa na vitambulisho vilivyoidhinishwa kwa usajili.

Shahidi huyo ambaye alisema amesomea ufundi wa umeme katika Chuo cha Ufundi Arusha kati ya mwaka 1992-1995, alivitaja vitambulisho hivyo kuwa ni cha mpiga kura, leseni ya udereva na pasi ya kusafiria.

Vitambulisho vingine kwa mujibu wa shahidi huyo, ni cha mwanafunzi na cha mkazi, lakini akasema laini hizo nne hazikusajiliwa kwa kufuata utaratibu huo. Shahidi huyo alizitaja laini hizo na majina yakiwa kwenye mabano kuwa ni 0788-275697 (Motii Riria), 0682-010119 (Motii Ndoole) na 0788-276417 na 0788259036 zilizosajiliwa kwa jina la Noldonyo Lolibon.

Alisema Agosti 15,2013 aliitwa polisi na alikutana na Koplo Seleman (shahidi wa 11) aliyemueleza kuwa laini hizo zilikuwa zimesajiliwa kinyume cha taratibu kwa vile hazikuwa na fomu za usajili.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, wakati akiitwa na kufika polisi tayari mawakala wawili waliosajili laini hizo ambao aliwataja kuwa ni Aneth Pius na Hamisa Kassim walikuwa tayari wamekamatwa.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake ndipo mmoja wa mawakili wa utetezi, Majura Magafu alipomtaka aeleze kama katika ofisi ya kanda ya Airtel iliyopo Arusha naye ana ofisi yake.

Hata hivyo, shahidi huyo badala ya kujibu swali hilo, alisema tu kuwa “huwa naripoti kwa bosi wangu”, lakini wakili Magafu akasisitiza shahidi ajibu swali hilo ili jaji aweze kuandika.

“Kwa hiyo shida ni mahali pa kukaa? Mimi naweza kuingia ofisini kwa bosi wangu kuna viti viwili nikafanya shughuli zangu. Saa nyingine sioni sababu ya kukaa,” alisema shahidi huyo. Alipoulizwa fomu za usajili huwa zinafanywa nini, shahidi huyo alisema huzikusanya za mikoa yote minne na kuziwasilisha ofisi za kanda na baadaye hutumwa makao jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakili Magafu alirejea tena swali lake kuhusu ofisi za shahidi huyo kwa kumuuliza kama anaposikia mtu anakwenda ofisini huwa anamaanisha nini, swali ambalo hakupenda kulijibu. “Unaponiuliza ana maana gani napata shida sana na hilo swali,” alijibu shahidi huyo na ndipo Majura akamuuliza mawakala huwa anakutana nao wapi, barabarani au nyumbani kwake.

“Naomba niwe huru kujibu. Kwa hiyo kama swali liko nje ya mazingira ni sawa nisipolijibu?” Alihoji shahidi huyo na kuibua kicheko kwa ndugu, jamaa na hata mawakili waliokuwepo mahakamani.

Jaji Maghimbi aliingilia kati kwa kusema, “Shahidi umeapa hapa mahakamani kusema ukweli. Sawa? Hii kesi si yako, wewe ni shahidi tu naomba useme ukweli kama ulivyoapa kusema ukweli.”

Baada ya kauli hiyo ya jaji, wakili Magafu alirudia tena swali lake akitaka kujua shahidi alikuwa akikutana wapi na mawakala, lakini shahidi huyo akamtaka katika swali lake aondoe neno ‘barabarani’.

Wakili Magafu akasema kwa vile hataki kujibu swali hilo, basi amwambie kule Arusha Technical College alipata cheti gani, badala ya kujibu shahidi huyo akamtaka wakili arudi kwenye swali lake la awali.

Hali hiyo ilimfanya Jaji Maghimbi kuingilia tena kati na kumtaka kujibu maswali ya mawakili kwa sababu amefika mahakamani kutoa ushahidi, ndipo aliposema alipata cheti cha umeme. Baada ya kujibu hivyo, wakili Magafu alirudia tena swali la awali la mahali anapokutana na mawakala ndipo shahidi huyo akajibu kuwa ni kwenye maeneo yao ya kazi wanapoweka miavuli na meza.

Shahidi huyo alisema katika utaratibu waliokuwa nao Airtel walikuwa hawaonyeshi laini namba ngapi hadi ngapi ilikuwa imeuzwa kwa wakala gani kati ya mawakala wao zaidi ya 20.

Jibu hilo lilimfanya wakili Magafu amuulize ilikuwaje akajua laini alizozitaja awali zilikuwa zimesajiliwa kwa majina aliyoyataja, akasema hilo alielezwa na shahidi wa 11, Koplo Seleman.

Akiendelea kujibu maswali ya wakili huyo kama kiongozi wa mawakala wa kusajili laini aliwahi kuwaona watu wenye majina aliyoyataja, alisema hakuwahi kuwaona. Akijibu swali la Wakili John Lundu aliyetaka kufahamu ni nani kati ya mawakala wawili (Hamisa na Aneth) aliyeuza laini hizo, shahidi huyo alisema sio waliouza na wala hatambui nani aliyeuza.

Katika hatua nyingine, shahidi wa 21 wa upande wa mashtaka, Flotea Mmasi aliieleza mahakama kuwa ndiye aliyeuza pikipiki mbili aina ya Toyo namba T316 CLB na King Lion yenye namba T751 CKB. Pikipiki aina ya Toyo ndio ambayo shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Mrakibu wa Polisi (SP), Joash Yohana alidai ilitelekezwa na watuhumiwa wa mauaji hayo huko Sanya Juu wakati wakitoroka.

Wakati Toyo ikikutwa imetelekezwa, pikipiki aina ya King Lion ilipokelewa kama kielelezo mahakamani Alhamisi iliyopita ikidaiwa kuwa ni mali ya mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo, Sadick Jabir. Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Jaji Maghimbi, shahidi huyo wa 21 wa upande wa mashtaka alisema Toyo aliiuza kwa Sh1.7 milioni wakati King Lion aliiuza kwa Sh1.65 milioni.

Akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na Wakili wa Serikali, Kassim Nassiri, shahidi huyo alisema Agosti 3, 2013 akiwa dukani kwake jijini Arusha alifika mteja kwa lengo la kununua pikipiki.

Alisema mteja huyo alitaka pikipiki aina ya King Lion na alimueleza bei kuwa ni Sh1.7 milioni, lakini aliomba ampunguzie bei ambapo alikubali na kumpunguzia Sh50,000 na hivyo kumuuzia kwa Sh1.65 milioni. “Tulikubaliana kwa bei ya Sh1,650,000 na niliruhusu mafundi watoe pikipiki kwa ajili ya kuifanyia matengenezo. Tukiwa hapo simu yake iliita na akatoa nje kuzungumza,” alisema shahidi huyo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, kama baada ya dakika tano, mtu huyo alirudi akiwa amefuatana na mtu mwingine ambaye baada ya kuingia dukani wakasema wanahitaji pikipiki mbili.

“Safari hii walitaka pikipiki ya Toyo na mimi sikuwa nayo, hivyo niliagiza kwa jirani yangu anaitwa Salvatory Thomas Luka ambaye alikuwa akiiuza kwa Sh1,700,000,” alisema shahidi huyo.

“Waliomba punguzo lakini nilishindwa kuwapunguzia kwa sababu Toyo ni ghali zaidi. Yule mtu aliyekuja wa pili alilipia pikipiki zote mbili.”

Shahidi huyo alisema alipowauliza aandike majina gani katika pikipiki hizo, walipiga simu kwanza kwa mtu mwingine na baadaye wakamwambia aandike Motii Ndoale Mollel.

Akiendelea kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alisema alipowauliza pikipiki hizo zilikuwa zinapelekwa eneo gani walisema ni Mirerani wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.

Alisema wakati wakiwa hapo, waliingia vijana wengine wawili na hivyo kufanya jumla ya waliofika kwa ajili ya pikipiki hizo kufikia wanne, lakini akasisitiza kuwa hawezi kuwakumbuka kwa sura.

Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee vitabu vya stakabadhi alivyovitumia kuandika risiti kwa ajili ya pikipiki hizo kama kielelezo cha kesi hiyo na mahakama ilikubali na kuvipokea.

Kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed na Ally Mussa itaendelea kusikilizwa leo.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro.

-->