Shahidi wa aliyekuwa mhasibu Takukuru atoa ushahidi

Muktasari:

Gugai na wenzake wanakabiliwa na  makosa 43, kati ya hayo 19 yakiwamo ya kughushi, utakatishaji fedha na  kumiliki mali zilizozidi kipato halali akiwa kazini

Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato chake, inayomkabili aliyekuwa  Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na mwenzake, ameieleza mahakama kuwa jumla ya Sh989 milioni zilikuwa ni mshahara na posho kwa kipindi cha miaka 15, alichokuwa kazini.

Shahidi huyo, Boniface Sechuma kutoka Takukuru Makao Makuu, Dodoma, amesema hayo leo, Oktoba 15, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akati akitoa ushahidi wake dhidi ya Gugai

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Pius Hila mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, shahidi huyo amedai kuwa kiasi hicho cha fedha ni mshahara na posho alizozipata Gugai tangu alipoajiriwa na Takukuru mwaka 2001 hadi 2016, ambapo ajira yake ilikoma.

Sechuma ambaye ni Mchunguzi Mkuu na Mhasibu, alidai kuwa Gugai aliajiriwa  Takukuru mwaka 2001 kama mchunguzi daraja la tatu na mwaka 2004 alihamishiwa mkoa wa Manyara na kuwa mkuu wa Takukuru wilaya ya Hanang.

Shahidi huyo alidai kuwa Agosti 2006, Gugai alihamishiwa makao makuu akawa mmoja wa washauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru na Desemba mwaka huo,  alihamishiwa Kitengo cha Uhasibu na  Januari  2007 aliteuliwa kuwa Kaimu Mhasibu Mkuu wa Takukuru.

"Nilimfahamu Gugai kama mtumishi mwenzangu na bosi wangu kwani mwaka 2009 aliteuliwa kuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, kazi aliyoifanya hadi mwaka 2016, ambapo utumishi wake ulikoma baada ya Takukuru kupata taarifa kuwa anamiliki mali nyingi zisizoendana na kipato chake halali," amesema  Sechuma.

Amesema baada ya Takukuru kupata taarifa hiyo, mkurugenzi mkuu aliunda timu ya kufuatilia tuhuma hizo, ambapo timu hiyo ilibaini ni kweli Gugai anamiliki mali nyingi ambazo hazilingani na kipato chake halali.

"Baada ya timu kukamilisha uchunguzi, iliwasilisha taarifa yake kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru " amesema

Mkurugenzi huyo baada ya kupitia taarifa hiyo, alitoa maelezo ya kuundwa kwa shauri la nidhamu.

Katika shauri hilo la nidhamu, timu iliwasilisha mapendekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, kuwa Gugai afukuzwe kazi.

" Baada ya mapendekezo hayo,  Takukuru ilichukua hatua za kumfukuza kazi Gugai," amesema.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16, 2018 itakapoendelea na ushahidi.

Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka, Ayoub Akida(52) ambaye ni Ofisa Utumishi Mkuu kutoka Takukuru, ameshatoa ushahidi wake dhidi ya Gugai.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Decembea 2015.