Wednesday, September 13, 2017

Shambulio la Lissu lilivyowaponza wabunge

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea (mbele) na mdogo wake Mbunge wa Singida Mashariki, Tindu Lissu wakiingia  katika Kanisa la Ufufo na Uzima, Ubungo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Ibada maalum ya kumuombea Tindu Lissu iliyoendeshwa na Askofu wa Kanisa hilo Josephat Gwajima jumapili iliyopita. Picha na Ericky Boniphace 

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Wakati sakata la kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu likimtia matatizoni mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema ni suala la muda tu kabla ya watu waliomjeruhi Lissu hawajafahamika.

Lissu alijeruhiwa kwa risasi tano kati ya 32, Septemba 7 mwaka huu, nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na kupelekwa hospitali ya mkoa wa Dodoma kabla ya kuhamishiwa hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi anakoendelea na matibabu.

Kubenea, ambaye ni mbunge wa Ubungo (Chadema), ameingia matatani kutokana na kauli aliyoitoa akimtuhumu Spika Job Ndugai kwamba alidanganya idadi ya risasi alizopigwa Lissu.

Jana, Ndugai aliagiza kutafutwa kwa namna yoyote kwa Kubenea na leo afikishwe kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ili ahojiwe kuhusiana na kauli hiyo.

Spika alitoa maagizo hayo bungeni jana baada ya matangazo ya wageni.

“Kumekuwa na upotoshaji mkubwa unaofanywa na Kubenea mara kadhaa ambao unalifedhehesha Bunge na mimi. Naagiza Kamati ya Adadi (Adadi Rajabu- Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama) imuite na asaidie kamati yeye anafahamu Tundu Lissu alipigwa risasi ngapi,”alisema.

Alisema maelezo aliyoyatoa bungeni kuhusu tukio hilo na idadi ya risasi alizopigwa Lissu alimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma.

“Ukinituhumu nimedanganya unajua zaidi, huyu atawasaidia, muiteni haraka katika Kamati ya Adadi. Katibu atafutwe aletwe kesho (leo) kwa haraka kwa utaratibu wowote,” alisema.

Alisema pia Kubenea atatakiwa kwenda katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kumwita Spika muongo.

Mbali na Kubenea, Spika Ndugai aliagiza mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kupelekwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kutamka kuwa Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za kamati ya Bunge za almasi na Tanzanite.

“Apate nafasi ya kusikilizwa huko, akahojiwe kuhusiana na kauli yake kuwa Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani,” alisema.

Alisema ripoti za kamati ambazo huwasilishwa ndani ya Bunge ni zile zilizotokana na azimio la wabunge ndani ya Bunge.

“Ni lini imetolewa hoja ya kuundwa kwa kamati? Ni lini mlihojiwa hapa hadi nikazuia kuleta hapa ripoti? Anaitwa nani mbunge aliyeleta hoja? Spika niliona busara kuunda kamati ambazo zitaishauri Serikali,” alisema.

Ndugai aliwaambia wapiga kura wa Zitto wajue mbunge wao ambaye yupo hapa nchini hajafika bungeni kuwawakilisha.

“Mimi sina taarifa za kutokuwapo kwake bungeni. Mbunge wenu mtoro Spika sina taarifa ya kutokuwepo bungeni naawaambia mliomchagua,” alisema.

Mbowe azungumzia kuhusu Lissu

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema watu waliopanga na kutekeleza shambulio la risasi dhidi ya mwanasiasa machachari wa upinzani, Tundu Lissu watajulikana muda si mrefu.

Ameliambia Mwananchi kwa njia ya simu akiwa Nairobi, Kenya, kuwa shambulio hilo lilipangwa kwa muda mrefu na kwamba waliofanya hivyo hawawezi kujificha tena.

“Tukio hili lilipangwa na kuratibiwa kwa muda mrefu. Kuna magari mengi yamekuwa yakimfuatilia Lissu kwa muda mrefu na hili jambo halikupangwa na mtu mmoja, limepangwa na watu wengi na baada ya muda kila kitu kitajulikana,” alisema.

Dk Mashinji aeleza jinsi risasi zilivyomvunja Lissu

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema Lissu ameumizwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na kwamba alipigwa risasi nyingi tofauti na risasi tano zilizoelezwa.

Dk Mashinji amesema Lissu amevunjwa miguu yake, nyonga na mkono wa kushoto, jambo ambalo linawapa madaktari kazi kubwa kuimarisha afya yake.

Kiongozi huyo alisema Lissu alianza kusumbuliwa na kifua juzi asubuhi, jambo lililowalazimu madaktari kumwekea mashine za kumsaidia kupumua, hata hivyo alisema walizitoa baadaye na jana aliamka salama.

“Bado najisikia uzito kuelezea hali ya Tundu Lissu. Kwa namna alivyoumia inawezekana matibabu yakachukua muda mrefu, hivyo tuendelee kumwombea na kuchangia matibabu hayo,” alisema Dk Mashinji.

Alisema Lissu ameongezewa damu nyingi akiwa Dodoma na bado anaendelea kuongezewa huko Nairobi, hivyo madaktari wanajitahidi kuokoa maisha yake na ana imani watafanikiwa.

“Sasa hivi wamemtibu sehemu za ndani ambazo zingehatarisha uhai wake, hilo wamemaliza sasa wameanza sehemu za nje na mpaka sasa amefanyiwa operesheni tatu. Madaktari wamesitisha kumfanyia upasuaji kwanza ili apate muda wa kupumzika.”

“Tutatumia resource (rasilimali) zote tulizo nazo kama chama kuhakikisha tunaokoa uhai wake,” alisema Dk Mashinji mbele ya vyombo vya habari na wanachama waliohudhuria mkutano huo.

Polisi kachero wa Kenya

Jeshi la Polisi limekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazomtaja mmoja wa askari wake wa kitengo cha Interpol kuwapo jijini Nairobi.

Juzi, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliweka picha ya kachero huyo kwenye mitandao ya kijamii na kueleza kuwa yupo Nairobi.

Msemaji wa jeshi hilo ACP Barnabas Mwakalukwa alisema taarifa hizo hazina ukweli, kwani kachero huyo alikuwa Nairobi kwa mafunzo maalumu na tayari amesharejea nchini.

“Askari huyo alikuwa nchini Kenya kwa kozi ya kimafunzo kuanzia Septemba 4 hadi Septemba 8 wakati Lissu alijeruhiwa Septemba 7.

“Tunatoa onyo kwa wote wanaofikiri wanaweza kukaa na kupika habari ili waweze kuivuta jamii iwe upande wao na kuchafua upande wa Serikali.”

Mwakalukwa alisema polisi kupitia kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao, linachunguza kuwabaini wanaohusika kusambaza taarifa za uongo.

Aliwataka watu wote waliotuma au kutoa maoni kuhusu taarifa hiyo kupitia kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii kujisalimisha kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kwa ajili ya kutoa maelezo.

“Kama unajijua uli-comment chochote kuhusu taarifa hiyo njoo mwenyewe kabla hujatafutwa, tuna njia zetu tunaweza kuwafikia,” alisema.

Mashirika 100 yalaani

Mashirika 102 ya utetezi wa haki za binadamu yameorodhesha matukio 17 ya uvunjifu wa amani yaliyokea nchini tangu mwaka 2015 na kulaani kitendo cha kupigwa risasi Lissu.

Akizungumza kwa niaba ya mashirika hayo, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amependekeza Bunge liunde tume huru kuchunguza waliohusika na tukio hilo.

“Tunapendekeza Bunge liunde tume huru kuchunguza tukio la Lissu na matukio mengine ambayo taarifa zake hazijajulikana hadi leo ili wahusika wachukuliwe hatua,” alisema na kuongeza, “tunalaani Lissu kupigwa risasi, ni tukio la kinyama.”

Mbali na tukio la Lissu, Bisimba aliyataja baadhi ya matukio mengine yenye utata yanayohitaji kuchunguzwa na tume hiyo kuwa ni la kutishiwa kupigwa risasi kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Alisema tukio hilo liliwashangaza Watanzania kwa nini waziri huyo alitishiwa kupigwa bastola hadharani na kwamba suala hilo linatakiwa kutolewa majibu.

Bisimba alisema tukio jingine linalotakiwa kufanyiwa kazi na tume hiyo ni kupotea kwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane..

Bisimba alisema tukio jingine ni mkutano wa CUF kuvamiwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha katika hoteli ya Viva iliyopo Mabibo wilayani Kinondoni ambao waliwapiga waandishi wa habari na wafuasi wa chama hicho

Imeandikwa na Elizabeth Edward, Pascal Adrian, Peter Elias, Benard James, Herieth Makwetta na Raymond Kaminyog

-->