Shehena ya bangi yawapeleka rumande maofisa watano wa polisi

Muktasari:

Taarifa za uhakika zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa wanaoshikiliwa na polisi ni ofisa mwandamizi wa Kituo cha Polisi Sanyajuu na maofisa wengine wanne.

Moshi. Maofisa watano wa Polisi wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, wametiwa mbaroni wakidaiwa kuachia shehena ya bangi na watuhumiwa waliowakamata.

Taarifa za uhakika zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa wanaoshikiliwa na polisi ni ofisa mwandamizi wa Kituo cha Polisi Sanyajuu na maofisa wengine wanne.

Mkuu wa Wilaya ya Siha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo, Onesmo Buswelu alilithibitishia gazeti la Mwananchi kuhusu kushikiliwa kwa maofisa hao wa polisi.

"Ni kweli wewe andika nimethibitisha kuwa wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa kwa kuachia watuhumiwa wa bangi. Tumeelekeza wakamatwe. Hapa Kazi Tu," alisema Buswelu.

Alipotakiwa na gazeti hili kufafanua undani wa tuhuma zinazowakabili mkuu huyo wa wilaya alisema taarifa alizonazo mezani kwake ni kuwa waliachia bangi na watuhumiwa.

Taarifa zimedai juzi usiku polisi hao walikamata magunia ya bangi kati ya manane na 10 lakini katika mazingira yasiyoeleweka waliwaachia watuhumiwa na bangi hiyo.