Sheikh Mbonde aanza upya mchakato kumfunga Babu Tale

Babu Tale 

Muktasari:

Katika hukumu iliyotolewa na Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016 wakurugenzi wa kampuni ya Tip Top Connection Company Limited  waliamriwa kumlipa fidia ya Sh250 milioni, mhadhiri wa dini ya Kiislamu

Dar es Salaa. Zaidi ya mwezi mmoja na nusu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufuta amri yake ya kuwakamata na kuwafunga gerezani wakurugenzi wa kampuni ya Tip Top Connection Company Limited, mahakama hiyo imewaita tena mahakamani wakurugenzi hao.

Mahakama hiyo imewaamuru wakurugenzi wa kampuni hiyo, Hamis Shaban Taletale, maarufu kama Babu Tale na ndugu yake Idd Shaban Taletale, kufika mahakamani hapo Jumatatu Oktoba 22, 2018 kufuatia maombi mapya ya kuwakamata na kuwafunga jela, yaliyofunguliwa mahakamani hapo.

Maombi hayo yamefunguliwa na mhadhiri wa dini ya Kiislam, Sheikh Hashim Mbonde, baada ya mahakama hiyo kuifuta amri ya awali iliyoitoa dhidi yao, kuwakamata na kuwafunga jela kama wafungwa wa madai.

Katika maombi hayo namba 755 ya mwaka 2017, Sheikh Mbonde anaiomba mahakama hiyo kuwakamata na kuwafunga jela kama wafungwa wa madai ndugu hao wawili kwa nafasi yao ya wanahisa na wakurugenzi wa Tiptop Connection Company Limited.

Pia, anaiomba mahakama hiyo iwaamuru walipe Sh215 milioni zilizosalia kati ya Sh250 milioni ambazo kampuni yao ya Tiptop iliamriwa na mahakama kumlipa kama fidia kwa kosa la kukiuka Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kwa kutumia mawaidha yake kibiashara bila ridhaa yake.

Kufuatia maombi hayo, mahakama hiyo, katika hati ya wito imewaamuru wanandugu kufika mahakamani hapo Jumatatu, saa 3:00 asubuhi, wakati maombi hayo yatakaposikilizwa na Jaji Yose Mlyambina.

Februari 16, 2018 naibu msajili wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri, aliamuru Babu Tale na nduguye Idd wakamatwe na kuwapeleka kifungoni katika gereza la Ukonga kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama hiyo.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016, iliwaamuru ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Sheikh Hashim Mbonde, kama fidia ya hasara halisi na hasara ya jumla kwa kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.

April 4, 2018 akatoa na kusaini hati ya kuwakamata na Mei 22, 2018, Babu Tale alitiwa mbaroni na Polisi Mkoa wa Ilala na kuhifadhiwa kituoni hapo siku mbili akisubiri Naibu Msajili Mashauri kuidhinisha amri yake ya kumpeleka gerezani kuwa mfungwa wa madai.

Lakini Mei 24, Jaji Mkasimongwa akikaimu nafasi ya Jaji Mfawidhi alimuachia huru kwa muda baada ya kubaini kasoro katika amri hiyo ya kuwakamata na kuwafunga.

Kesho yake, Mei 25 aliwataka mawakili wa pande zote kutoa hoja zao kuhusu hoja iliyoiibua mahakama hiyo iwapo Msajili ana mamlaka ya kutoa na kusaini amri hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, katika uamuzi wake alioutoa Julai 2, 2018, Jaji Mkasimongwa aliifuta amri hiyo ya kuwakamata na kuwafunga, akisema ilikuwa ni batili.

Jaji Mkasimongwa alisema hiyo haikuwa halali kwa kuwa Msajili hana mamlaka ya kutoa na kusaini amri kama hiyo na kwamba alitenda kinyume cha mipaka ya mamlaka yake na kwamba amri kama hiyo inatolewa na kusainiwa na Jaji pekee na si Msajili.

Hata hivyo, licha ya kuifuta amri hiyo alitoa maelekezo kwa mwombaji kama akipenda awasilishe maombi upya ili yaweze kusikilizwa na kuamriwa na mamlaka husika.
Soma zaidi: