Sheikh Salum awaasa waislam

Muktasari:

Sheikh Alhad alitoa ushauri huo jana wakati akifungua Msikiti wa Imamu Ali, uliopo Mikwambe wilayani Kigamboni uliokwenda sambamba hafla ya futari.

Dar es Salaam. Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amewahimiza waislam nchini, kuutumia vyema mwezi wa Ramadhani kwa kuwa karibu na kuwasaidia watu wasiojiweza ikiwamo kula nao pamoja futari.

Sheikh Alhad alitoa ushauri huo jana wakati akifungua Msikiti wa Imamu Ali, uliopo Mikwambe wilayani Kigamboni uliokwenda sambamba hafla ya futari.

Alisema imezoeleka wakati wa futari watu wenye uwezo na nafasi za juu, hualikana wenyewe kwa wenyewe, huku watu wasijioweza wakihangaika.

“Tutumie fursa hii, kuwakumbuka watu wa namna hiyo. Asipatikana mtu akakosa futari au chakula tujitahidi watu wenye uwezo tuwakumbuke wenzetu,” amesema Sheikh Alhad.

Mbali na hilo, Sheikh Alhad aliwataka Waislam katika kipindi hiki kujenga tabia ya kuwatembelea yatima, wajane na wagonjwa mbalimbali waliopo hospitalini ili kuwafariji.

Aliwaasa pia Waislam kuutumia mwezi huo kusameheana pale walipokosana na kwamba mwezi ambao dua za waumini zinakubaliwa.