Shein apunguza baraza, ampa ulaji Hamad

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein jana alitangaza Baraza la Mawaziri.

Muktasari:

Katika uteuzi huo, Dk Shein ameunganisha baadhi ya wizara na kuweka wizara tatu zenye mawaziri wanne chini yake.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein jana alitangaza Baraza la Mawaziri kwa kuziunganisha baadhi ya wizara na kufanya idadi yake kupungua kutoka 16 za awali hadi 13.

Katika uteuzi huo, Dk Shein ameunganisha baadhi ya wizara na kuweka wizara tatu zenye mawaziri wanne chini yake.

Wizara hizo ni Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ.

Wizara zingine ni Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Wizara ya Fedha na Mipango.

Wizara zingine ni Wizara ya Afya; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali; Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto; Wizara ya Biashara, Viwanda; Masoko; Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo.

Wizara nyingine ni Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.

Hamad Rashid aula

Baraza hilo la Dk Shein limewajumuisha wanasiasa mchanganyiko wakiwamo wakongwe, wanadiplomasia na Mlezi wa chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed ambaye pia aliwania urais kupitia chama hicho kuteuliwa kuongoza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Wengine walioteuliwa ni Issa Haji Ussi Gavu (Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), Haroun Ali Suleiman (Katiba, Sheria na Utawala Bora) na Haji Omar Kheir (Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu).

Wengine ni Mohamed Aboud Mohamed (Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais), Dk Khalid Salim Mohamed (Fedha na Mipango) na Mahmoud Thabit Kombo (Afya).

Mawaziri wengine ni Riziki Pembe Juma (Elimu), Amina Salum Ali (Biashara, Viwanda na Masoko), Ali Abeid Karume (Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi), Rashid Ali Juma (Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo).

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Moudline Castico, mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuvuliwa uraia wakati wa awamu ya tatu na baadaye kurejeshewa, ambaye sasa ataongoza wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto. Salama Aboud Talib ataongoza wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.

Dk Shein alitaja naibu mawaziri kuwa ni Harous Said Suleiman (Afya), Mmanga Mjengo Mjawiri (Elimu), Mohamed Ahmed Salum (Ujenzi), Lulu Msham Khamis (Kilimo), Chumu Kombo (Habari), Juma Makungu Juma (Ardhi) na Juma Khamis Maalim (Katiba).

Ateua wapinzani Baraza la Mapinduzi

Dk Shein pia aliwateua Juma Ali Khatib kutoka ADA-Tadea na Said Soud Said (AFP) kuwa Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar. Mawaziri hao walitarajiwa kuapishwa wakati wowote kuanzia sasa katika viwanja vya Ikulu ya Vuga, mjini hapa.

Akitoa hotuba yake kabla ya kutangaza baraza hilo, Dk Shein alisema akiwa kiongozi mkuu wa Serikali ya Zanzibar aliyepata ushindi mnono atahakikisha anaiongoza Serikali yake kwa uwazi na ukweli.

Alisema yeye na safu yake ya uongozi, watajitahidi kulinda haki na amani ya wananchi wa Zanzibar na kuwaomba wananchi wote bila kujali itikadi zao kumuunga mkono.

“Lengo la Serikali yangu ya awamu ya saba ni kuhakikisha kila Mzanzibari anapata fursa, analindwa yeye na mali zake, tunasisitiza amani wakati wote kwa kuwa ni jambo lililopo katika Katiba yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa uchaguzi umekwisha kwa amani na utulivu na kwamba kinachotazamwa sasa ni kuwafanyia kazi Wazanzibari na akaahidi kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu na umakini.

Maoni ya wachambuzi

Wachambuzi wa siasa za Zanzibar walisema timu hiyo ni mkusanyiko wa watoto wa vigogo na watawala wa zamani wa SMZ na pia zawadi ya kisiasa kutokana na mambo yaliyojitokeza kuelekea uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016.

“Nahisi kuna kikundi cha watoto wa wakuu wa mikoa, watoto wa wabunge na si vibaya kusema wamo wapigadebe wa uchaguzi wa marudio sambamba na wale wafuasi wa siasa za zamani za ‘Komandoo’ Dk Salmin Amour (Rais wa Awamu ya Tano ya Zanzibar),” alisema Hafidh Othman, mwanasheria wa kujitegemea na mchambuzi wa mambo ya utawala.

Mohamed Khamis, mwanahabari mwandamizi nchini alisema: “Sioni hali ya matumaini katika Baraza lililotangazwa ingawa pia sikubaini wapiga siasa walio mahiri zaidi ya watu waliopata fursa ili wazitumie.”