Sheria, kanuni za uwekezaji kigezo muhimu uchumi wa viwanda

Muktasari:

Baada ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuandaa jukwaa la kwanza la fikra lililofanyika Juni likijadili magonjwa yasiyoambukiza, MCL inakuletea jukwaa la pili la fikra litakalofanyika katika ukumbi wa Kisenga, Kijitonyama, Oktoba 4, kujadili fursa na changamoto kuelekea Tanzania ya viwanda.

Wakati tukijiandaa kwa tukio hilo la kihistoria, tunakuletea mfululizo wa makala zinazobainisha fursa na changamoto zilizopo. Leo tunazungumzia mchango wa sheria na kanuni za uwekezaji kufanyika kufanikisha ndoto hiyo.

Safari ya Tanzania kuelekea kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda inavutia licha ya changamoto na ugumu uliopo.

Changamoto zilizopo hazitokani na kukosa sera au kanuni maridhawa zinazoongoza sekta ya viwanda kwani kwa muda mrefu, zimekuwapo na watunga sera wamekuwa makini kutengeneza miongozo itakayowasaidia wananchi kutimiza lengo hilo.

Tangu uhuru, sheria mbalimbali zimetungwa chini ya sera zinazobadilika kila inapobidi. Lakini, inaelezwa baadhi ya sheria, sera na kanuni hizi zilikuwa dhaifu ilhali baadhi zikiwa imara zaidi ikichangiwa na usimamizi usio makini katika utekelezaji.

Kutokana na ukweli huo, upo msemo maarufukwamba: “Sera hutungwa Tanzania kisha kuboreshwa Uganda na kutekelezwa Kenya.”

Baada ya uhuru lilitungwa Azimio la Arusha mwaka 1967 ambalo licha ya kuwahamasisha wananchi kujituma ili kujitosheleza kwa kila kitu, lilihimiza Serikali kujenga misingi ya kujitegemea.

Azimio hilo liliwazuia viongozi wa umma kuanzisha, kuendesha au kuwa wanahisa au wakurugenzi wa kampuni au mashirika msimamo ambao ni tofauti na sera inayotumika sasa kuhamasisha ujenzi wa viwanda.

Chini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Endelevu Tanzania (SIDP) 2020 na Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025) Serikali inasimamia utekelezaji wa azma ya kuwa na uchumi imara.

Dira ya maendeleo

Baada ya kutungwa mwaka 1999, dira inakusudia kuhamasisha maeneleo ya uchumi ili kuihamisha Tanzania kutoka miongoni mwa nchi masikini hadi uchumi wa kati msisitizo ukiwa kuboresha maisha ya wananchi.

Wachambuzi wa mambo wanasema hii inahitaji kipaumbele kuelekezwa kwenye ubunifu wa sayansi na teknolojia ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha ufanisi hasa sekta ya kilimo kwa kuhamasisha uongezaji thamani wa mazao yanayovunwa.

Wataalamu wa masuala ya uchumi na maendeleo wanasema Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 imeweka msingi imara kuindoa Tanzania kutoka kwenye uchumi wa kilimo mpaka wa viwanda.

Kosa ambalio hufanywa mara nyingi hivyo kukwamisha nia njema iliyopo, inaelezwa kuwa ni kukosekana kwa mpango mkakati wa utekelezaji wa sera husika kuanzia mwanzo wa kutungwa kwake.

Sera ya viwanda

Sera ya Maendeleo ya Viwanda Endelevu 2020 inakusudia kuondoa uchumi kutoka serikalini kwenda sekta binafsi. Awali, Serikali ilikuwa inaendesha na kusimamia uchumi suala ambalo sasa linafanywa kinyume chake kupitia sera hii.

Sera hiyo iliyotungwa mwaka 1996 inahamasisha uwekezaji wa sekta ya viwanda ikiwa ni muongo mmoja wa Tanzania kutegemea program za taasisi na mashirika ya kimataifa.

Pamoja na mambo mengine, lengo la sera hiyo ni inakusudia kujenga uwezo wa ndani utakaoiruhusu Tanzania kushindana kwenye soko la kimataifa kwa kuipa sekta nafasi ya kuongoza uwekezaji wa viwanda huku Serikali ikibaki na jukumu la kutunga sera rafiki na kuboresha mazingira ya uanzishaji na ufanyaji biashara.

Changamoto

Licha ya malengo mazuri yaliyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo, yapo mambo mbalimbali ambayo ni kikwazo katika uwekezaji nchini jambo linaloweza kufifisha jitihada za kujenga uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya urahisi wa kufanya biashara mwaka huu inaonyesha Tanzania imeporomoka kutoka nafasi ya 132 mwaka 2016 mpaka 137 mwaka 2017 kati ya nchi 190 zilizotathminiwa.

Mfumo wa sheria na kanuni ni miongoni mwa vikwazo vinavyobainishwa kuwachelewesha wawekezaji kuanzisha viwanda au miradi mingine nchini licha ya kampeni kubwa inayofanywa na Serikali.

Kati ya changamoto zinazobainishwa na ripoti hiyo ni kwamba huchukua siku 30 kupata cheti cha tathmini ya athari za mazingira (EIA) kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc) hivyo kuchelewesha utekelezaji.

Mapema Julai, Rais John Magufuli alisema vibali vya Nemc huchelewesha uanzishaji wa miradi na kuwataka wahusika walifanyie kazi suala hilo ili kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda.

Kikwazo kingine ni mabadiliko ya mara kwa mara kwenye sheria za kodi pamoja na kiwango kikubwa na wingi wa kodi husika.

Mabadiliko ya sera ya fedha ambayo hubadili mfumo wa kodi unaelezwa kuwayumbisha wawekezaji hasa waliopo. Viwango vikubwa vya kodi hupunguza faida ya uwekezaji na zinapokuwa nyingi tatizo hilo huwa kubwa zaidi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.

Mkakati

Pamoja na changamoto zilizopo, sekt abinafsi inaon aupo uwezekano wa kuongeza mchango wake nchini. Hili linatokana na kufanyiwa kazi kwa maoni yao yaliyojumuishwa kwenye muongozo wa ufanyaji biashara na uwekezaji nchini (Blueprint) ambao tayari umekabidhiwa kwenye baraza la mawaziri.

Licha ya kuanisha mapungufu ya kanuni na sera, muongozo huo umebainisha mkanganyiko wa kisheria uliopo hasa kwenye utekelezaji wa majukumu ya mamlaka za usimamizi zilizopo.

Utekelezaji wa muongozo huo, ambao pamoja na kubainisha mapungufu yaliyopo, umeweka mapendekezo ya namna ya kushughulika na changamoto zilizoainishwa ili kuboresha mazingira yaliyopo.

Yakifanyiwa kazi kwa wakati, mapendekezo hayo yatatoa unafuu kwa wawekezaji nchini kwa kupunguza muda wa kushughulikia ukamilishaji wa utaratibu uliopo pamoja na kuokoa fedha zinazolipwa kwa mamlaka nyingi zinazoingiliana kwenye kimajukumu.