VIDEO:Sheria kuruhusu watu kujipima Ukimwi nyumbani

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akijibu swali bungeni katika kikao cha 41 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Maambukizi yameongezeka kwa mkoa wa Dodoma kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 5 sawa  na mkoa wa Tanga na Mwanza.


Dodoma. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Wizara imemwandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kubadili sheria na kila mtu aweze kujipima Ukimwi nyumbani.

 Waziri Ummy ameyasema hayo leo Mei 31 bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambulie (CUF), Masoud Abdalla Salim ambaye ameuliza mkakati  wa ziada wa  Serikali kutambua wanaopata athari za Ukimwi.

 “Nchi nyingine wanatumia mate kutambua waathirika wa VVU (Virusi vya Ukimwi), Serikali ina mkakati gani wa ziada kutambua wale wanaopata athari za VVU hasa tukianza na Mkoa wa Dodoma.”ameuliza Salim

Akijibu swali hilo, Waziri Ummy ambaye pia ana dhamana ya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto amesema sheria imekuwa kikwazo kwa wananchi kujipima maambukizi ya Ukimwi.

Waziri Mwalimu amesema, ni kweli maambukizi yameongezeka kwa mkoa wa Dodoma kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 5 sawa sawa na mkoa wa Tanga na Mwanza.

“Tunafanya utafiti maalumu kubaini kwa nini maambukizi yamepanda. Tumekuwa na changamoto ya kuwapata wanaume kupima na njia ya   mtu kujipima mwenyewe,” amesema Waziri Mwalimu

Kuhusu dawa za VVU, Waziri Mwalimu amesema, zipo kwa asilimia 100.

“Ukimwi si sentensi ya kifo, ukibainika tunakuingiza katika mpango wa  kupata dawa.” amesema