Sheria ya kuwabana wote wanaojiita ‘madaktari’ yaja

Muktasari:

Watakaobaini kutozwa faini au kifungo kisichozidi miaka miwili

Dodoma. Serikali imekuja na Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi ambao utazuia watu kujiita madaktari bila kuwa na elimu ya kiwango cha shahada na kuendelea.

Jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliwasilisha maelezo ya muswada huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleoya Jamii mjini Dodoma ili kujadiliwa.

Akizungumza nje ya kikao cha kamati hiyo, Mjumbe wake, Dk Faustine Ndungulile (CCM- Kigamboni) alisema Muswada huo ni mzuri na kwamba utawabana na kuwaondoa watu wanaojiita madaktari bila kuwa na sifa.

Dk Ndungulile ambaye pia ni daktari kitaaluma, alisema Sheria iliyokuwa inatumika ya mwaka 1959 imepitwa na wakati na kada nyingi za kutoa huduma za matibabu zimeongezeka hivyo kusababisha changamoto kwenye sekta ya afya.

Alisema kupitwa na wakati kwa sheria hiyo kumesababisha pia taaluma nyingi kukosa usimamizi katika sekta ya afya.

Akisoma maelezo ya muswada huo, Ummy alisema unaainisha makosa na adhabu zitakazotolewa kwa watu wanaokwenda kinyume cha sheria.

Muswada huo umeainisha pia adhabu ya Sh5 milioni na isiyozidi Sh10 milioni ama kutumikia kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka miwili ama vyote kwa pamoja kwa mtu atakayebainika anafanya kazi bila kuwa na sifa za taaluma husika.

“Kuna changamoto nyingi katika kukidhi mabadiliko ya ongezeko la vyuo vya udaktari, ongezeko la wahitimu wa udaktari wa meno na teknolojia katika utoaji wa huduma za afya,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema kamati yake itaufanyia kazi muswada huo kwa kukutana na wadau ili kusikiliza maoni yao kabla haijatoa mapendekezo yake.