Tuesday, March 21, 2017

Sheria ya uvuvi kufanyiwa marekebisho kuongezwa makali

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba 

By Rehema Matowo, Mwananchi

Chato. Katika kupambana na uvuvi haramu na kulinda masalia ya samaki, Serikali imesema inakusudia kuifanyia marekebisho Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 ili kuipa makali zaidi.

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la kimataifa la samaki na dagaa, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema sheria hiyo inatakiwa kurekebishwa kwa kuwa haina nguvu.

Pia, wizara hiyo inakusudia kuwasilisha bungeni marekebisho ya vifungu vya sheria namba 22 na kanuni zake za mwaka 2009 ya kuongeza adhabu kwa wavuvi wanaovunja sheria kutoka Sh200, 000 za sasa hadi Sh5 milioni pamoja na kifungo cha miezi sita.

 “Sheria hizi zilikuwepo lakini sasa hazina nguvu na watu wanatuchezea wanavua kwa zana haramu wakikamatwa hakimu anamwambia alipe faini ya Sh200, 000 akitoka nje analipa anamzomea aliyemkamata sasa tunazibadili ukikamatwa na kokoro tunakuweka ndani na makosa ya uhujumu uchumi hayana dhamana,”alisema Dk Tizeba.

Dk Tizeba alisema marekebisho ya sheria hiyo yatawagusa wavuvi haramu, wanaosafirisha samaki kinyume cha sheria, wanaobanika samaki wasio halali na wenye duka wanaouza nyavu zisizoruhusiwa.

Mbunge wa Chato, Dk Merdad Kalemani alisema ujenzi wa soko hilo ni ahadi aliyoitoa mwaka 2010 wakati wa kampeni kwa lengo la kuona uchumi wa watu wa Chato unakua.

-->