Sheria za Tanzania kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk Adelardus Kilangi

Muktasari:

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk Kilangi amesema serikali ipo kwenye mchakato wa kuziandika kwa Kiswahili.


Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk Adelardus Kilangi amesema serikali iko katika mchakato wa kuziandika sheria zote za Tanzania ili zisomeke kwa lugha ya kiswahili.

Hata hivyo Dk Kilangi amesema kazi hiyo inakutana na vikwazo viwili ambavyo ni uhaba wa fedha na utaalam mzuri wa watafsiri wa lugha ili wasipotoshe maana katika sheria.

Mwanasheria Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni leo Septemba 05, 2018 wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu Faida Mohammed Bakari (CCM).

Katika swali la nyongeza mbunge huyo amehoji ni kwa nini serikali inapeleka miswada bungeni ambayo imeandikwa kwa lugha ya kingereza bila kujua elimu za wabunge zinatofautiana.

Amesema kutoandika miswada na sheria katika lugha ya kiswahili ni kushindwa kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kuhusu lugha ya kiswahili.

Mwanasheria Kilangi amesema tayari maandalizi ya kazi hiyo yameshaanza na mpango huo utakwenda kwa utaratibu mzuri na uangalifu.

Awali Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Antony Mavunde amesema mahakama za Tanzania zinaendesha kesi zao kwa lugha za kiswahili na kiingereza kulingana na uamuzi wa Jaji au hakimu isipokuwa mahakama za mwanzo pekee zinaendesha kesi kwa kiswahili tu.

Hata hivyo Mavunde amesema hukumu zote zinaandikwa kwa Kiingereza pekee na sababu ni kuwa Tanzania ipo katika mfumo wa common law hivyo ziko nchi hufanya rejea za hukumu za mahakama za nchini na hata mahakama.