Shindano kampuni 100 bora lazinduliwa

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakati wa NMB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa kutambulisha wajasiriamali bora 100. Kulia ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu na Mshauri wa Masoko wa KPMG, Ketan Shah

Muktasari:

MCL kwa kushirikiana na kampuni ya ukaguzi wa hesabu za kampuni na ushauri ya KPMG wanaratibu mashindano hayo


Dar es Salaam. Mchakato wa kuzisaka kampuni 100 bora zenye mitaji ya kati kwa awamu ya nane umezinduliwa.

Benki ya NMB na Hoteli ya Hyatt Regency watakuwa wadhamini wakuu wa shindano hilo linalolenga kuwainua wajasiriamali wadogo na kati kushindana kitaifa na kimataifa.

Akizungumza leo Julai 10, wakati wa hafla ya uzinduzi, mhariri mtendaji mkuu wa kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Bakari Machumu amesema lengo ni kuwaweka wafanyabiashara wenye mitaji ya kati katika mfumo rasmi wa kuendesha biashara.

MCL kwa kushirikiana na kampuni ya ukaguzi wa hesabu za kampuni na ushauri ya KPMG wanaratibu mashindano hayo

Ambayo pamoja na mambo mengine yanahamasisha washiriki kuorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

"Msukumo mkubwa ni kuangalia sekta ya kilimo, kuongeza thamani ya biashara zao na namna ambavyo watatengeneza ajira.Hawawezi kufanya hivyo bila kufuata wengine wanafanyaje kimataifa ndiyo sababu ya kufanya utafiti huu,"amesema Machumu.

Amesema kwa sasa Serikali imeweka msukumo mkubwa wa kuhamasisha uanzishaji wa viwanda ili kuongeza mchango wa sekt ahiyo kwenye Pato la Taifa hivyo wafanyabishara wanapaswa kuangalia watakavyoshiriki kwenye mkakati huo.

Mshauri wa masoko wa KPMG, Ketan Shan amesema kampuni zinazopaswa kushiriki mchakato huo ni zenye mtaji kati ya Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni.

Kampuni hizo zinatakiwa kukaguliwa hesabu zake kwa walau miaka mitatu mfulilizo na kuonyesha ongezeko la faida kila mwaka.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo na kati wa Benki ya NMB, Abdulmajid Nsekela amesema ushiriki wao utaipa fursa benki hiyo kupiga hatua na kutanua wigo wa huduma kwa wananchi.

“Kupitia mchakato huu NMB itatoa fursa kwa wateja hao kunufaika na huduma za kibenki hususan mikopo kwa ajili ya wafanyabiashara ili kupanua wigo wa biashara zao," amesema.

Licha ya NMB na Hoteli ya Hyatt Regency, wadhamini wengine wa shindano hilo ni Azam Media na Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).