Shivyawata yapata Sh24 mil za ujasiriamali

Muktasari:

  • Katibu wa Shivyawata Wilaya y Kisarawe, Ibrahim Tuli alisema fedha hizo ni ajili ya kutoa elimu kwa wajasiriamali kwa vitendo kata za Kurui na Kidugalo.

Kisarawe. Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, limepata Sh24 milioni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali.

Katibu wa Shivyawata Wilaya y Kisarawe, Ibrahim Tuli alisema fedha hizo ni ajili ya kutoa elimu kwa wajasiriamali kwa vitendo kata za Kurui na Kidugalo.

Tuli alisema fedha hizo zitatumika katika utoaji elimu namna ya kufuga kuku wa kienyeji kwa njia za kisasa sanjari na ujenzi wa mabanda, kabla hawajapewa vifaranga.

Alisema mradi huo utaendeshwa kama wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe, kwani mkulima atalazimika kulipa kuku kwa ajili ya kukopesha wengine ili uwe endelevu.

Katibu huyo alisema waliwahi kutoa kuku kwa wanachama wao ili wafuge, lakini walikula wote hivyo kusababisha mradi kufa.

Tuli alisema hawataki kurudia makosa ndiyo maana wanatoa elimu kwanza, kwani kufanikiwa kwa mradi huo kutawasaidia wanachama hao kumudu gharama za kusomesha watoto wao na kuondokana na utegemezi.

Wilaya ya Kisarawe ina watu wenye ulemavu mbalimbali 1,400 wakiwamo wa ngozi 71.

Mmoja wa wanufaika wa elimu, Ali Mkala alisema mradi huo utasadia kuwakwamua na umaskini na kuachana na utegemezi.

Mkalla alisema iwapo Serikali itakuwa ikiwawezesha watu wenye ulemavu kama Shivyawata wanavyofanya, walemavu wengi wataacha kuwa ombaomba kwani watapata fursa ya kushiriki maendeleo.