Shonza asema hawatarudi nyuma

Muktasari:

Shonza amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imejipanga vizuri kuhakikisha maadili ya Mtanzania yanadumishwa na kuzingatiwa hususani wasanii wanapofanya kazi zao za sanaa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania

Dodoma. Serikali imesema haitarudi nyuma katika suala la maadili kwa wasanii wote nchini licha ya kelele nyingi ambazo zinapigwa na watu wasioitakia mema tasnia ya muziki.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alipokutana na viongozi wa taasisi ya Malezi Bora Foundation ofisini kwake mjini Dodoma ambao walilenga kuzungumzia mpango  wa kuanzisha kampeni maalumu ya kuhamasisha maadili kwa wasanii hapa nchini.

Shonza amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imejipanga vizuri kuhakikisha maadili ya Mtanzania yanadumishwa na kuzingatiwa hususani wasanii wanapofanya kazi zao za sanaa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Wizara yetu imejipanga kuhakikisha maadili ya Mtanzania yanalindwa na kuheshimika na kila mtu, wito wangu kwa wasanii ni kuhakikisha wanazingatia maadili wanapotengeneza kazi zao za sanaa na kwenye maisha yao kwa ujumla kwani wasanii ni kioo cha jamii,” amesisitiza Shonza.

Akizungumzia suala la wasanii kuweka picha za nusu uchi kwenye mitandao ya kijamii Shonza amesema wanafuatilia kwa karibu wale wote wanaoweka picha zisizozingatia maadili kwenye mitandao ya kijamii na hatua za kinidhamu dhidi yao zitachukuliwa bila kumuonea mtu huruma.