Shonza azungumzia sheria ya huduma za habari

Muktasari:

Asema sheria hiyo lengo lake ni kuwasaidia waandishi wa habari kutambulika kama wanataaluma wengine.


Dodoma. Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema Serikali haikutunga Sheria ya Huduma za Habari kwa lengo la kuwakomesha waandishi wa habari nchini, bali kuwasaidia waweze kutambulika kama wanataaluma wengine.

Akizungumza leo Februari 13, 2018 katika maadhimisho ya siku ya redio duniani, Shonza amewataka waandishi wa habari nchini kuangalia pia mazuri yaliyomo katika sheria hiyo kuliko yanayolalamikiwa.

“Ninaamini sheria hii ina mazuri mengi ambayo kama tukiyafuatilia na kuyatumia vizuri yanaweza kutusaidia. Mojawapo ni kuifanya taaluma ya waandishi wa habari iwe kama taaluma nyingine,” amesema.

“Hatukuleta sheria kuja kuwakomesha waandishi wa habari, hapana. Tumeleta hii sheria na kutoa muda ili kupitia muda huo basi muweze kusoma na kutambulika kama wanahabari kwelikweli.”

Aidha, Shonza amewataka waandishi kuzingatia maadili ya uandishi wa habari ikiwemo kuhakikisha habari wanazoziandika zinakuwa na mizania na kuhakikisha hawapindishi habari yoyote ile hata kama hawaipendi.

“Ni vyema mkajiweka mbali na masuala ya kisiasa kwa sababu unapokuwa mwandishi wa habari halafu ukaingiza U-CCM, ukaingiza U-Chadema, ukaangiza U-CUF ni vigumu kuhakikisha habari inatoka ikiwa na taarifa kutoka pande zote,” amesema.