Shule ya Sekondari Bukoba yafungwa baada ya vyumba 15 kuezuliwa kwa upepo

Muktasari:

Wanafunzi 97 wamehamishiwa Sekondari ya Bweni ya Omumwani na 750 Ihungo baada ya baadhi ya vyumba vya madarasa na ofisi za walimu Shule ya Sekondari Bukoba kuezuliwa na upepo

Bukoba. Shule ya Sekondari Bukoba mkoani Kagera imefungwa baada ya vyumba 15 vya  madarasa na ofisi za walimu kuezuliwa kwa upepo usiku wa kuamkia leo Jumatano Oktoba 17, 2018

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi zaidi ya 800 wamehamishiwa shule za sekondari Ihungo na Omumwani zilizomo mkoani humo.

Shule hiyo ambayo ilikumbwa na tetemeko la ardhi Septemba 10, 2016, ilikuwa haijafanyiwa ukarabati kwa vyumba vya madarasa vilivyoathiriwa.

Ofisa elimu Mkoa wa Kagera, Aloyce Kamamba amesema wanafunzi 97 wa kidato cha tano na sita wamehamishiwa Shule ya Omumwani na 750 wa kidato cha kwanza hadi cha nne wamepelekwa Ihungo.

Amesema vyumba vinane vya madarasa vimeathiriwa na vingine vinane vya walimu pamoja na maabara ya fizikia na tathimini ya kiwango cha hasara inaendelea kufanyika.

Kamamba amesema mkurugenzi wa manispaa ameagizwa kufanya tathmini ya uharibifu na shule hiyo ilikuwa katika mpango wa kukarabatiwa tangu ilipoathiriwa na tetemeko la ardhi.

Amesema uhamisho huo hautakuwa na athari kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya kidato cha nne kwa kuwa wamehama na walimu wao na wale wa kidato cha tano na sita wataendelea kukaa bweni kama walivyokuwa shuleni kwao Bukoba.

Kuhusu idadi kubwa ya wanafunzi waliohamishiwa Ihungo amesema vyumba vilivyopo vinajitosheleza na kusema wanafunzi wanaodai shule hiyo iko mbali hilo ni suala la wanafunzi wachache.