Siasa, Lowassa, wanasiasa njiapanda

SIKILIZA ALICHOKISEMA MBOWE BAADA YA LOWASSA KWENDA IKULU

Muktasari:

Na si kukutana tu, bali sifa ambazo Lowassa, ambaye aliwahi kuelezewa na Tundu Lissu kama “tembo wa siasa za Tanzania” alimmwagia Rais Magufuli bila ya kueleza kasoro za utawala wake zinazolalamikiwa na wapinzani, zimefanya mjadala kuwa mzito zaidi.

Dar es Salaam. Edward Lowassa alikuwa kete ya Chadema na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, sasa amekuwa tena katikati ya mustakabali wa siasa za Tanzania baada ya kukutana faragha na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Na si kukutana tu, bali sifa ambazo Lowassa, ambaye aliwahi kuelezewa na Tundu Lissu kama “tembo wa siasa za Tanzania” alimmwagia Rais Magufuli bila ya kueleza kasoro za utawala wake zinazolalamikiwa na wapinzani, zimefanya mjadala kuwa mzito zaidi.

Na hiyo imejionyesha wazi baada ya viongozi wa Chadema kukosoa waziwazi kauli ya waziri mkuu huyo wa zamani wakisema pamoja na kusifu, alipaswa kueleza matatizo ya kidemokrasia yaliyopo nchini, kushambuliwa kwa wanasiasa, kupotea kwa watu kadhaa na kukamatwa mara kwa mara kwa wanasiasa.

Lowassa hajasema kama anarejea kwenye chama hicho kilichomlea, lakini tayari mjadala umeshaibuka kuhusu uwezekano wa kuchukua hatua hiyo, huku suala la mgombea urais wa Chadema mwaka 2020 likionekana kuanza kurudi katika utamaduni wake wa kawaida wa mwanachama kutopewa nafasi ya pili kujaribu.

Mvutano ulioibuka ndani ya Chadema baada ya mazungumzo hayo ya Ikulu umeibua hisia tofauti hasa kuhusu misukosuko, mikakati na matarajio ya Lowassa tangu akiwa CCM hadi alipohamia chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Wakati mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema maoni ya Lowassa ni yake binafsi na hayahusiani na chama, huku mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu akisema kumsifia Rais Magufuli ni vigumu kukubalika na kuna athari kubwa kisiasa.

Lowassa alikutana na Rais Magufuli juzi na kufanya mazungumzo kwa mara ya kwanza tangu mbunge huyo wa zamani wa Monduli alipojiengua CCM na tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliowapambananisha wawili hao uliokuwa na ushindani kuliko wakati mwingine wowote tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi.

Mkutano huo umezua misimamo tofauti baada ya Chadema kulaumu, huku baadhi ya wana-CCM wakisema hatapata kitu hata kama atarejea.

Vikao vya juu vya CCM vimekuwa vikimtaja Lowassa kila mara huku waliomfuata au kumuunga mkono wakionekana kuwa ni wasaliti na baadhi kuchukuliwa hatua na Chadema ikitumia vikao vyake kumtetea.

Na Rais Magufuli alitumia kikao cha juzi kueleza umahiri wa Lowassa katika siasa na kutaka aenziwe. CCM sasa itakuwa njiapanda kuacha kumponda au kumsifu kama mwenyekiti wao alivyofanya.

Maswali yamekuwa yakitawala katika mitandao ya kijamii na kuzidisha mjadala kama Lowassa akirejea CCM hali itakuwaje ndani ya chama hicho tawala kutokana na kutumia nguvu nyingi kumshambulia baada ya kujivua uanachama kwa kumtuhumu kwa kashfa mbalimbali, huku Chadema ikimtenga na kashfa hizo na hivyo kujiweka katika hali ngumu ya kupambana naye tena iwapo atarejea CCM.

Februari 6, 2016 katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake, Lowassa alisema kusakamwa na maneno, kejeli, vijembe na vitisho, kuitwa gamba na fisadi ndani ya CCM ndiko kulikomfanya kukihama chama hicho na kwenda upinzani.

Lowassa, ambaye kwa mara ya kwanza alikutana na Rais Magufuli Agosti 28, 2016 na ambaye alikuwa na nguvu na ushawishi ndani ya CCM, alihamia Chadema baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kumsaka Rais kwa tiketi ya chama hicho.

Katika mahojiano hayo alisema licha ya kuitumikia CCM kwa zaidi ya miaka 30 tangu mwaka 1977, chama hicho kiliamua kutumia watu kumsakama kwa kila aina ya maneno, jambo lililomfanya achoke. Uamuzi wa kujiunga na upinzani ulitafsiriwa na CCM kuwa Chadema inashindwa kuendeleza hoja yake ya kupinga ufisadi kwa kwa kumteua mtuhumiwa wa ufisadi kugombea urais.

Agosti 30, 2016 Lissu alinukuliwa na Mwananchi akisema Lowassa ni tembo aliyepo katikati ya uwanja wa siasa za Tanzania, hata ukifumba macho hapotei yuko palepale.

Lissu amekuwa akimtetea kuwa kashfa ya Richmond ni ya kimfumo na hivyo wote waliohusika wafikishwe mahakamani. Pamoja na tuhuma hizo, Lowassa aliibuka kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi tangu uchaguzi wa vyama vingi uanze tena nchini. Alipata kura milioni 6.07, huku mshindi Rais Magufuli akikusanya kura milioni 8.8.

Lakini kauli zake za juzi kuhusu Rais Magufuli na mazungumzo yake ya kirefu, vitafanya ndoto yake ya kugombea tena urais kwa tiketi ya Chadema kuwa njiapanda kutokana na jinsi chama hicho kilivyoipokea.

Na uwezekano wa kutimiza ndoto hiyo kupitia CCM pia itakuwa ngumu kutokana na utamaduni wa chama hicho, lakini Chadema na CCM zitakuwa kwenye wakati mgumu kukabiliana na sakata kutokana na ukweli kwamba Lowassa ni “tembo wa siasa za Tanzania.

Wanasiasa walonga

Watu waliongea na Mwananchi au waliotoa taarifa za maoni yao pia walikuwa na maoni tofauti kuhusu kikao cha wawili hao.

“Inaelekea Lowassa hakumshirikisha mwenyekiti (wa Chadema) kabla ya kukubali au kuamua kwenda Ikulu kukutana na Rais Magufuli,” alisema Lissu, ambaye yuko Ubelgiji akitibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma, tukio ambalo mwanasiasa huyo amelielezea kuwa ni “jaribio la mauaji ya kisiasa.”

“Na juzi tu wakubwa wetu hawa wawili (Lowassa na Mbowe) walikuwa pamoja hospitalini kumsalimia Mzee Ngombale Mwiru. Je, inawezekana Lowassa hakuwa anajua tayari kwamba ana appointment Ikulu? Kama alikuwa anajua, kutokumshirikisha mwenyekiti wake kuna tafsiri gani hasa?”

Alisema katika mazingira ya sasa nchini, uamuzi wowote wa kufanya mazungumzo na Rais hata kama ni kwa nia njema, bila kushauriana au kushirikisha viongozi wa juu wa Chadema ni uamuzi usio sahihi na mgumu kukubalika.

“Kauli za aina ambayo tumeisikia kutoka kwa Lowassa, zina athari kubwa kisiasa. Sio tu zinachanganya wanachama na wafuasi wetu, lakini pia zinawapa mtaji wa kisiasa maadui zetu,” alisema.

Alisema kuanzia sasa Chadema wategemee kuwasikia CCM wakishangilia kile alichokiita busara za Lowassa.

Naye katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju alisema Lowassa aliwahi kuwa kiongozi mkubwa wa Serikali na Rais Magufuli alikuwa chini yake, hivyo si dhambi kwa wawili hao kukutana.

Alisema Lowassa kwenda Ikulu kusichukuliwe kuwa ni msaliti au anataka kuhama Chadema, bali kiongozi bora anatakiwa kuwa hivyo akisisitiza mtu anaweza kuhama chama bila kwenda Ikulu.

“Kuna dhana iliyojengeka kuwa ukiwa mpinzani huwezi kusifia kazi zinazofanywa na Serikali, lakini kumbe mambo hayaendi hivyo na ni jambo la kawaida kutoa pongezi kama alivyofanya Lowassa,” alisema.

Alisema huenda kuna zaidi yaliyozungumzwa na viongozi hao, ukiacha yale yaliyowekwa katika taarifa ya Ikulu.

Naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema, “Siwezi kujua kwa sasa lakini huenda wamejadili mambo mbalimbali, hasa ukizingatia upinzani umekuwa ukilalamika kwa muda mrefu suala la uminywaji wa demokrasia.”

“Kama wamejadili masuala ya kitaifa kutokana na hali halisi ilivyo Lowassa atafikisha ujumbe kwa viongozi wa chama vinavyounda Ukawa na baadaye kutoa taarifa kwa umma kuhusu suala hilo, lakini kama mambo mengine itakuwa ni siri yao,” alisema.

Kwa upande wake, Hashim Rungwe wa Chaumma alisema: “Lowassa aliomba siku nyingi kuonana na Rais na kila mtu ana mazungumzo yake. Kila mtu ana mawazo yake binafsi. Sijaona kibaya alichokifanya.”

Mmoja wa manaibu katibu mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema: “Kwa hali hii, Lowassa hawezi kukaa Chadema, ujue kilichompeleka Lowassa Chadema ni upepo tu, aliangalia fursa ya kugombea urais lakini bado ana mapenzi na CCM.

“Si Lowassa pekee atarudi CCM, bali wote waliotoka watarudi. Ipo siku mtakumbuka maneno yangu. Kitendo cha yeye binafsi kwenda kumuona Rais Ikulu kinaonyesha alivyo na mapenzi na CCM.”

Maoni ya Sakaya yanatofautiana na mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovuta.

“Sioni kama kuna tatizo hapo, kusifia si kwamba kwenda CCM ni mtazamo wake lakini kama Chadema walikuwa wanasubiri ateleze wamchukulie hatua haya ila mimi naona hakuna tatizo,” alisema.

Nyongeza na Ibrahim Yamola