Saturday, April 20, 2013

Mbunge atuhumiwa kuyumbisha sheria

By Habel Chidawali, Mwananchi

Dodoma. Wabunge wameendelea kushambuliana kwa maneno makali huku Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) akimtuhumu mbunge mwenzake wa Viti Maalumu bila ya kumtaja jina kuwa anatumia fedha zake kuyumbisha sheria.

Mbunge huyo alisema kuwa kigogo huyo amekuwa akitumia fedha nyingi kupindisha sheria ili nyumba yake iliyoko eneo la Kawe Dar es Salaam isivunjwe licha ya kuwa iko katika eneo la wazi.

Alitoa shutuma hizo wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano kwa mwaka wa Fedha 2013/14. “Nimejifunza mambo mengi jeshini, miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kusema ukweli kwa ajili ya nchi yangu na watu wake, na nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko,” alisema Bulaya na kuongeza:

“Yupo mtu hapa ambaye ni kigogo mkubwa na kiongozi mkubwa wa kisiasa ambaye yupo humu ndani, lakini amekuwa akitumia fedha zake kuiyumbisha sheria na kuzuia nyumba yake isivunjwe, hili ni jambo la hatari sana mheshimiwa spika naomba kutoa hoja kuwa nyumba hiyo ivunjwe ndani ya siku saba,”

Eneo hilo limekuwa na migogoro ya muda na baadhi ya nyumba zilivunjwa na Serikali lakini nyumba hiyo inayotuhumiwa kuwa ya mbunge aliyekwenda mahakamani kuzuia nyumba yake isivunjwe.

Bulaya aliitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kutoogopa kuvunja nyumba hiyo kwani bila ya kufanya hivyo jamii haitawaelewa.

“Kutokana na hilo, niko tayari kutoa shilingi ili kuzuia bajeti hiyo kama sitapata majibu ya kuridhisha juu ya nyumba hiyo, kwani hatutendi haki kama viongozi ambao tunatakiwa kuwa ni mfano kwa wengine juu ya mema lakini tunaongoza kufanya maovu,” alisisitiza Bulaya.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa ufafanuzi na kumtaka Bulaya kuwa mvumilivu kwani mahakama ndiyo chombo pekee kitakachotoa uamuzi wa mwisho juu ya haki ina nani na inafaa kutolewa lini.

-->