Standard Gauge, Stiglers Gorge tupo vizuri au tutajuta baadaye?

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania na Misri jana zimesaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa umeme utakaozalishwa Mto Rufiji katika bonde la Stiegler Gorge.

Jumatano iliyopita, Kampuni ya Arab Contractors ya Misri na Shirika la Umeme nchini (Tanesco), walisaini mkataba wa ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme kwenye Mto Rufiji, maarufu kama Stiegler’s Gorge. Utilianaji huo wa saini ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly, walikuwa mashuhuda wa utilianaji huo wa saini. Kukamilika kwa Stiegler’s Gorge kutaifanya Tanzania kuwa na umeme mkubwa, wenye kutosheleza nchi na zaidi tena kwa bei nafuu.

Mradi wa Kinyerezi ulipokamilika mwaka juzi, taarifa ya Tanesco ilieleza kuwa mahitaji ya umeme yalitimia kwa asimilia 100. Ilielezwa kwamba Kinyerezi inazalisha megawati 150, hivyo kufikisha megawati 1,500 ambazo ndizo mahitaji ya nchi kwa sasa.

Hata hivyo, hali halisi ya umeme kwa sasa, jinsi umeme unavyokatika mara kwa mara, huku nishati hiyo ikionekana kuwa si ya uhakika, ni dhahiri kuwa kiwango cha umeme kilichopo hakitoshelezi. Ama uwezo wa mitambo ya ufuaji ni mdogo au njia za upitishaji wa umeme zimezidiwa.

Stiegler’s Gorge ikikamilika, itaweza kuzalisha umeme zaidi ya megawati 2,100. Kwa hesabu ya Tanesco mwaka juzi kuwa mahitaji ya nchi ni megawatt 1,500, maana yake, mradi huo ukikamilika, itawezekana hata kuzima mitambo mingine yote na kutumia umeme wa Stiegler’s Gorge na mwingine utabaki.

Mantiki hapo ni kwamba nchi itakuwa na umeme mwingi wa ziada. Itaweza kuuza hata nje umeme mwingine. Ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), unaendelea awamu ya kwanza kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro. Matarajio ni kupitisha treni za umeme. Stiegler’s Gorge inaielekeza nchi kwenye umeme unaokidhi mahitaji.

Tuuhoji uhakika

Pongezi kwa Rais Magufuli kwa nia yake njema pamoja na uthubutu wa kuhakikisha nchi inakuwa na umeme mwingi na wa bei nafuu, ukizingatia kuwa Stiegler’s Gorge ni mradi ambao upo kwenye mipango ya Serikali tangu miongo minne iliyopita.

Novemba mwaka jana, wakati Bunge lilipokuwa kwenye mjadala wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017-2018, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliikosoa Serikali kwa uamuzi wake wa kutoishirikisha sekta binafsi katika miradi inayoweza kujiendesha kibiashara.

Alikosoa utaratibu wa Serikali kujenga miradi mikubwa kwa fedha za ndani, wakati kiuhalisia inakopa na kuipa nchi mzigo mkubwa wa madeni. Nape alisema, kuishirikisha sekta binafsi kuna nafuu kubwa kuliko kuendelea kukopa, kitu ambacho alionya kwamba kitakuja kusababisha athari kubwa kwa nchi.

Jambo la kwanza Nape alisema kuwa Serikali inakopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mikubwa ambayo ukamilikaji wake unachukua muda mrefu, wakati mikopo husika marejesho yake yanafanyika ndani ya muda mfupi. Kutokana na hali hiyo, alitahadharisha kwamba marejesho yataathiri miradi mingine.

Nape alisema kwa vile miradi itachelewa kukamilika, wakati wa marejesho ya mikopo, itabidi kuchukua fedha kwenye miradi ya huduma kama elimu, afya na kadhalika ili kuwalipa wadeni wa nchi. Katika hili Nape alisema anatilia shaka uzalendo wa wachumi ambao wanamshauri Rais Magufuli.

Tahadhari ya Nape

Upande wa pili, Nape alionya kuwa nchi inapiga hatua kwenda kuwa isiyokopesheka ikiwa itakopa kwa ajili ya miradi miwili tu; wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) dola 15 bilioni (Sh33.8 trilioni) na wa ufuaji umeme wa Stiegler’s Gorge megawati 2,100 dola 5 bilioni (Sh11.27 trilioni), jumla dola 20 bilioni (Sh45 trilioni).

Nape alisema taarifa za mpango zinaeleza Deni la Taifa lilifikia dola 26 bilioni (Sh58.6 bilioni) sawa na asilimia 32 ya uhimilivu wa deni. Kwamba ili Tanzania ifikie kikomo cha kukopeshwa, deni lake linapaswa kufikia dola 45 bilioni (Sh101.4 trilioni).

Kutokana na hoja hiyo ya Nape, endapo Serikali itaongeza mkopo kwa miradi miwili tu ya Standard Gauge na Stiegler’s Gorge, deni lingefikia dola 46 bilioni (Sh103.7 trilioni), yaani ongezeko la Sh2.3 trilioni kutoka kwenye kiwango chake cha mwisho cha kukopa.

Hata hivyo, hesabu ya Nape kuwa Stiegler’s Gorge ingegharimu Shi11 Trilioni haipo sawa, kwani wakati wa utiliaji saini kati ya Tanesco na Arab Contractors, Waziri wa Nishati, Medadi Kalemani, alisema kuwa mradi gharama yake jumla ni Sh8 Trilioni.

Nape pia alikosoa kutelekezwa kwa mradi wa gesi ambao uligharimu maisha ya watu kuhamishwa makazi. Mipango ya awali ilikuwa nchi ije kuwa umeme wa gesi. Hata hivyo, Rais Magufuli mwaka huu alizungumzia sababu ya kupuuza mradi wa gesi, kwamba ulishaandaliwa mazingira ya kifisadi.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, amekuwa akipigia kelele mkataba wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge, kuwa unaminya fursa zilizopo nchi. Nchi ina chuma, makaa ya mawe na kila kitu chenye kutumika kujenga reli, lakini mkataba uliopo unafanya Waturuki waliopewa zabuni watoe malighafi nje ya nchi, badala ya kuwabana kutumia zilizopo nchini.

Wadau wa mazingira wanadai Stiegler’s Gorge ni hatari kwa mazingira, lakini wanapuuzwa. Haya ndiyo mambo ya kutazama kipindi hiki furaha ikiwa imetanda. Je, kila kitu kinakwenda safi au upo wakati majuto yataibuka. Hoja za akina Nape na Zitto hazina maana au utafika wakati itakuwa majuto mjukuu? Watu wa mazingira je? Vema kusikiliza hoja za kila upande, kwani hiyo ndiyo mantiki ya kujenga nchi moja.