Wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote nchini

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakipitia kabrasha la mapendekezo ya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya kanuni za Bunge hilo mjini Dodoma mwaka 2014. Kutoka kushoto ni Tundu Lissu, Ismail Jussa, Profesa Ibrahim Lipumba na Godbless Lema. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Ukifuata Katiba na mfumo wetu wa utawala, wananchi wanazungumza kupitia bungeni. Ili upate maagizo ya wananchi, ni lazima kusikiliza sauti kutoka bungeni.
  • Iko wazi kwenye Katiba kwamba, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, kama tunaifuata Katiba ya nchi hatuwezi kuziba masikio juu ya kilio cha wananchi cha kuitaka Katiba Mpya

Ni muhimu kukubaliana na kuelewana tumesimamia wapi? Kama tunaifuata Katiba ya nchi hatuwezi kuziba masikio juu ya kilio cha wananchi cha kuitaka Katiba Mpya.

Iko wazi kwenye Katiba kwamba, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote. Hivyo, wananchi wakiitaka Katiba hakuna wa kusema hapana. Upole wa Watanzania, utulivu na amani visichukuliwe kama njia ya kukwepa wajibu na ukweli.

Ukifuata Katiba na mfumo wetu wa utawala, wananchi wanazungumza kupitia bungeni. Ili upate maagizo ya wananchi, ni lazima kusikiliza sauti kutoka bungeni.

Bila sauti ya Bunge ni mapenzi ya watu binafsi na ni kwenda na kinyume na Katiba. Ingawa bado kuna kasoro za hapa na pale na wakati mwingine Bunge letu kuwa na wawakilishi wengi wa chama kimoja na kufanya maamuzi ya kukipendelea chama chao, lakini kwa asilimia kubwa maamuzi ya Bunge, kwa uzito yanachukua nafasi ya kwanza ukilinganisha na mapenzi ya mtu binafsi.

Fedha na rasilimali zote za nchi ni mali ya wananchi. Maamuzi ya kuzitumia fedha au kutozitumia ni maamuzi ya wananchi. Viongozi ni wasimamizi tu na wanafanyakazi ya uratibu kwa kuelekezwa na wananchi wenyewe. Hili wala halina mjadala wa kubishana. Liko waziwazi. Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote.

Inawezekana kabisa kwamba jambo hili limesahaulika au watu wanalifumbia macho. Inawezekana hata wasomi wetu hawatambui tena kwamba msingi wa mamlaka yote ni katiba na Katiba yenye imetamka hivyo katika ibara ya nane.

Masuala ya kujiuliza, ni je, kwa kiasi gani hii Serikali inawajibika kwa wananchi? Je, wananchi wanaelewa maana ya kifungu hiki katika Katiba yao? Je, wananchi wanajua kwamba wao ndio msingi wa mamlaka yote na madaraka katika nchi? Ni mipango mingapi ya Serikali imefanyika kwa kuzingatia ustawi wa wananchi wake? Ni kiasi gani wananchi wamekuwa wakishirikishwa shughuli za Serikali yao? Ni wananchi wangapi wanafahamu kwamba Serikali inawajibika kwao?

Wananchi wangejua Serikali inawajibika kwao ni kiasi cha kusema: ‘Tunataka Katiba Mpya na hakuna mtu wa kupinga.

Awamu za uongozi nchini Awamu ya kwanza ya uongozi wa taifa letu ilisaidia sana kuimarisha misingi ya taifa letu, maadili ya taifa letu, umoja wa taifa, mshikamano wa taifa, lakini pia kujaribu kuwafanya Watanzania wajione ni taifa huru. Pamoja na dosari zilizojitokeza wakati wa awamu ya kwanza, hakuna anayeweza kupinga mafanikio niliyoyataja hapo juu.

Awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi, ilifungua milango ya biashara. Kama hii ilisaidia kupambana na ulofa, kujenga moyo wa kutetea uhuru wetu na uzalendo.

Awamu ya tatu ya Benjamin Mpaka, ilishughulikia zaidi mambo ya uchumi na imefanya kazi nzuri katika ubinafsishaji.

Awamu ya nne ya Jakaya Kikwete, ilijenga uhusiano na nchi za nje, ilijenga miundombinu, vyuo vikuu viliongezeka, huduma za maji, umeme na afya viliboreshwa.

Awamu ya tano ya Rais John Magufuli, imetumbua majipu, imepambana na rushwa, ufisadi na imejikita katika sera ya viwanda. Kwa kiasi kikubwa kila Mtanzania mwenye nia njema na taifa letu ni lazima aisifie.

Pamoja na hayo, si kazi ya viongozi kufanya yale wanayoyataka wao, hata kama ni mazuri kwa ustawi wa wananchi; kazi ya viongozi ni kufanya yale waliyoagizwa na wananchi.

Maana yake ni kwamba, kama wananchi wanaitaka Katiba, hakuna wa kupinga. Viongozi wote wanaajiliwa na wananchi na hawa ndio mabosi.

Watu mbalimbali katika taifa letu wamekuwa wakililia ushirikishaji wa wananchi katika mipango mbalimbali ya maendeleo. Jukwaa la majadiliano katika ngazi ya kijiji hadi taifa. Jitihada nyingi zimefanyika kulijenga jambo hili lakini, bado limeshindikana na uamuzi unafanyika kwenye ngazi za juu na kuletwa chini.

Taifa huru, lenye watu huru ni muhimu na ni lazima wananchi wakafahamu Serikali inawajibika kwao. Ni muhimu watu wakaushinda ulofa. Mfano usiku wa kuamkia Desemba 9, 1961, Mwalimu alitamka hivi: “Mtalala malofa na mtaamka malofa. Mtalala kama watawaliwa lakini mtaamka kama watu huru na mnaojitawala. Msikubali mtu yeyote awanyang’anye uhuru wenu.”

Kama alivyosema Mwalimu, uhuru ulipatikana na yeye alitumia nguvu zake zote kuulinda. Na si kuulinda uhuru wetu tu, alihakikisha nchi nyingine za Afrika zinapata uhuru kama wa kwetu.

Tunakumbuka alivyotufundisha kwamba kama jirani yako si uhuru, uhuru wako na wewe pia uko mashakani.

Uhuru ulipatikana, lakini ulofa, ulibaki palepale. Watu wengi hawakuwa na elimu, ajira, umasikini ulikuwa ni wa kutisha na maradhi yaliwashambulia watu kwa kasi.

Kwa kupambana na ulofa, kitu ambacho pia alikifanya kwa nguvu zake zote. Mwalimu aliwatangaza maadui watatu: Ujinga, maradhi na umasikini. Vitu hivi aliviona kama kizingiti kikubwa kwa Mtanzania kufikia maendeleo.

Ili kupambana na maadui hawa watatu, na kuutokomeza ulofa na kuyakaribisha maendeleo, mwalimu alizitangaza silaha za kutumia ardhi, siasa safi, watu na uongozi bora.

Maisha yote mwalimu, alipambana na ulofa na kuulinda uhuru wa Tanzania. Aliyafanya haya kwa uaminifu mkubwa.

Ni bahati mbaya kwamba wale waliokuwa wamemzunguka na watekelezaji wake hawakuyaelewa vizuri malengo yake.

Ndiyo maana badala ya kuuboresha mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea, wameamua kuuzika.

Awamu ya kwanza ya uongozi wa taifa letu ilisaidia sana kuimarisha misingi ya taifa letu, maadili ya taifa letu, umoja wa taifa, mshikamano wa taifa, lakini pia kujaribu kuwafanya watanzania wajione kwamba ni taifa huru. Pamoja na dosari zilizojitokeza wakati wa awamu ya kwanza, hakuna anayeweza kupinga mafanikio niliyoyataja hapo juu.

Awamu ya pili ya mzee mwinyi, ilifungua milango ya biashara. Kama hii ilisaidia kupambana na ulofa, kujenga moyo wa kutetea uhuru wetu na uzalendo.

Awamu ya tatu ilishughulikia zaidi mambo ya uchumi na imefanya kazi nzuri katika ubinafsishaji.

Awamu ya nne ilijenga uhusiano mkubwa na nchi za nje, ilijenga miundombinu, vyuo vikuu viliongezeka, huduma muhimu kama maji, umeme na afya viliboreshwa.

Awamu ya tano, imetumbua majipu, imepambana na rushwa, ufisadi na imejikita katika sera ya viwanda. Kwa kiasi kikubwa kila Mtanzania mwenye nia njema na taifa letu ni lazima aisifie.

Pamoja na hayo, si kazi ya viongozi kufanya yale wanayoyataka wao, hata kama ni mazuri kwa ustawi wa wananchi; kazi ya viongozi ni kufanya yale waliyoagizwa na wananchi.

Maana yake ni kwamba, kama wananchi wanaitaka Katiba, hakuna wa kupinga. Viongozi wote wanaajiliwa na wananchi na hawa ndio mabosi.

Utility

Nukuu

Ibara 8(1): Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo:-

(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii;

(b) Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;

(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;

(d) Wananchi watashiriki katika shughuli za serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.”