Wapinzani walipaswa kutoa Azimio la Zanzibar kabla ya Ukuta

Vyama sita vya upinzani, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD, Chaumma na ACT-Wazalendo, vimetoa tamko ambalo wameliita Azimio la Zanzibar. CUF iliyohusika na utilianaji saini ni ile ya upande wa Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad.

Azimio hilo, limesainiwa na Seif kwa upande wa CUF, Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi na Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe.

Hoja zote zilizozungumzwa kwenye Azimio la Zanzibar zinaweza kuwekwa kwenye kichwa kimoja cha utambulisho; demokrasia. Vyama hivyo vimeunda mshikamano wa kudai demokrasia na wameutangaza mwaka ujao, 2019 kuwa ni wa kudai demokrasia.

Uhuru wa vyama kufanya siasa na kubanwa kwa asasi za kiraia, Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, Sheria ya Takwimu na kadhalika, ni mambo ambayo yameguswa chini utambulisho wa kupigania demokrasia.

Tunapaswa kukubaliana hili; muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ndiyo kichocheo cha vyama hivyo kukutana na kusaini azimio la pamoja. Wameona sheria hiyo ikishapita itakula kwao.

Ni sahihi pia kusema kwamba kama kusingekuwa na muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, pengine viongozi wa vyama hivyo wasingekuwa na mawazo ya kukutana, kujadiliana na kuunda azimio la pamoja.

Azimio limechelewa

Julai 2016, Rais John Magufuli, alitangaza kufuta mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano. Chadema walitangaza kuwa Septemba Mosi, 2016, ingekuwa siku ya maandamano makubwa. Rais Magufuli aliwajibu kwamba hajaribiwi. Muda ulipofika, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kuahirisha Ukuta mpaka Oktoba Mosi, 2016 ambayo pia iliahirishwa na maandamano hayo hayakufanyika tena.

Utaona kuwa kosa la kiufundi ambalo Chadema walilifanya kupitia Ukuta ni kuanzisha vuguvugu la kudai demokrasia peke yao kisha wakaita ni umoja.

Kimatamshi, Chadema walitangaza kuwa Ukuta ni wito wa jumla wa kudai demokrasia. Walisema Ukuta ni zaidi ya mapambano ya kisiasa, kwamba viongozi wa dini, asasi za kiraia na makundi mengine, walipaswa kushiriki.

Walichosahau ni kuwa waungwana hawahudhurii harusi wasizochanga. Hukumwalika kwenye maandalizi wala hakuchanga, sherehe ikifika atajiongeza tu kwamba haimhusu. Chadema hawakualika makundi waliyoyakusudia kipindi cha maandalizi, matokeo yake walipotangaza Ukuta, waliowalenga wakajiona hawahusiki.

Hiyo ndiyo sababu Ukuta lilibaki kuwa vuguvugu la Chadema. Bungeni, Chadema wanaongoza Kambi ya Upinzani kwa kushirikiana na CUF pamoja na NCCR, chini ya mwavuli waUkawa, lakini kwenye Ukuta, waliwatenga katika kujenga mawazo na kuyapitisha.

Kwa vile vyama vingine vilijitenga na Ukuta, ikawa sababu ya kutofanikiwa. Na tangu Ukuta ulipofeli, hakujawahi kuwa na mawazo yenye nguvu kwa wapinzani mpaka Azimio la Zanzibar. Ukipima Ukuta ulivyoshindwa kuvuta wigo mkubwa wa wapinzani, unapata jibu kuwa Azimio la Zanzibar lilipaswa kusainiwa kabla ya Ukuta.

Chadema walitakiwa kuviita mezani vyama vingine mwaka 2016 na kuunda mawazo ya pamoja. Ama Ukuta wenyewe au azimio lolote ambalo lingesainiwa, ilitakiwa kuwe na nguvu ya pamoja. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

Nini kiliwachelewesha?

Seif ndiye aliwaita viongozi waandamizi wa vyama vya upinzani ili kuzungumza kisha kupitisha Azimio la Zanzibar. Imepita miaka miwili na miezi mitano tangu shughuli za kisiasa zipigwe marufuku. Vilevile ni miaka miwili na miezi tisa tangu Uchaguzi wa Zanzibar uliporudiwa Machi 20, 2016 na Dk Ali Mohamed Shein kuchaguliwa kuongoza muhula wa pili.

Swali linakuja; nini kimewachelewesha? Mkutano wa Zanzibar uliozaa Azimio la Zanzibar ulipaswa kufanyika miaka miwili iliyopita ili kuunda nguvu za pamoja. Tatizo kila chama kilitaka kupambana na hali yake. Matokeo yake ikawa rahisi kuwadhibiti.

Seif akajikuta yupo peke yake kupigania haki ya ushindi wa urais Zanzibar ambao anaamini aliupata katika Uchaguzi Mkuu 2015. CUF ilipoingia kwenye mgogoro wa uongozi, kwa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, aliyejiuzulu Agosti 2015, kurejea mwaka 2016 na kudai bado mwenyekiti halali, Seif akawa peke yake kwenye mapambano dhidi ya Lipumba.

Seif akawa na safari nyingi za nje, ikielezwa ni jitihada za kutaka jumuiya za kimataifa kutambua kuwa Shein ni kiongozi aliyeingia madarakani kwa uchaguzi batili. Rungwe na Chaumma yake naye akawa anapambana peke yake.

Chadema tangu Mwanasheria Mkuu wao, Tundu Lissu alipopigwa risasi nyingi Septemba 7, mwaka jana, ikawa kama wamepigwa na bumbuwazi. Na msemaji wa masuala ya nchi alikuwa Lissu. Ikawa kila mmoja anamtazama Mbowe.

Zitto naye akawa na harakati nyingi mitandaoni, vilevile mikutano na waandishi wa habari. Pengine harakati za Zitto zingepata ushirikiano na vyama vingine, hali isingekuwa iliyopo sasa.

Jinsi ambavyo wapinzani walivyopepesuka tangu mwaka juzi, Zanzibar iliporejewa uchaguzi na CUF walipoanza kugombea uongozi, kisha shughuli za kisiasa zilipopigwa marufuku, ndiyo maana swali linakuja, wapinzani walichelewa wapi kuungana na kutoa azimio la pamoja kama la Zanzibar? Hata hivyo, pongezi kwao kwa hatua waliyofikia.