Wednesday, September 13, 2017

Siku 10 zilivyopoteza maisha ya Moureen na Ikram mikononi mwa watekaji Arusha

By Mussa Juma, Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz

Matukio ya utekeaji watoto yaliyotokea hivi karibuni jijini Arusha yameacha majonzi na maswali magumu kwa wakazi wa jiji hilo.

Tukio la kutekwa watoto wawili Moureen David (6) na Ikram Salim (3) na baadaye kupatikana wakiwa wamefariki dunia ndilo linaloendelea kugonga katika vichwa vya wananchi wengi.

Mauaji hayo yametonesha majonzi ya vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent vilivyotokea Mei 6 mwaka huu.

Tukio la kutekwa na kuuawa kwa watoto hao limekumbusha majonzi ya Mei 6 kwa sababu limemhusisha mwanafunzi mwingine la Lucky Vincent, Moureen ambaye alikuwa anasoma darasa la kwanza.

Hakuna aliyetarajia kuwa watekaji ambao walikuwa wakiongozwa na Petro Samson (18) wangeweza kukatisha maisha ya watoto Moureen na Ikram kwa kuwa walionyesha dalili za kuwarejesha wakiwa hai.

 

Wazazi wa watoto wazungumza

David Njau ni baba wa Moureen, anasema mtoto wake alitekwa Agosti 21 saa 11 jioni alipokuwa anacheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao Mtaa la Olkelian Olasiti mjini Arusha.

Anasema Moureen baada ya kutoka shuleni  alibadili nguo na baadaye kupata chakula.

“Baada ya chakula alitoka nje kucheza na wenzake, lakini ilipofika saa 12 jioni hakurudi nyumbani ndipo tulianza kumtafuta,” anasema.

Anasema watoto wenzake waliokuwa nawacheza naye walieleza kuwa alikuja kijana mmoja akamuita kwa jina na kumchukua na kuondoka naye.

“Siku iliyofuata tulipata ujumbe uliotupwa mlangoni kuwa Moureen yupo na watekaji, lakini tusitowe taarifa popote kwa majirani au polisi juu ya tukio hilo,” anasema.

Anafafanua kuwa watekaji hao waliandika namba ya simu 0625791236  na 0753131899 tutume fedha kiasi cha Sh4.5 milioni ndipo   wamuachie  Moureen.

“Baada ya huu ujumbe ambao ulitupwa nje ya nyumba tulichanganyikiwa na mama yake Moureen kwani kiasi hicho cha fedha tulikuwa hatuna, hivyo kwa kutumia namba ambazo walitumia tulituma ujumbe wapunguze,” anasema.

Anasema ujumbe huo, ulijibiwa kuwa watume Sh2 milioni   nao wakaomba wapunguziwe zaidi kwani hawakuwa na kiasi hicho ndipo wakasema wapewe Sh300, 000.

Hata hivyo, anasema baada ya majadiliano hayo wakati wanaanza kutafuta fedha hizo, wakashauriwa kutoa taarifa polisi nao wakafanya hivyo.

“Baada ya kuwapa taarifa polisi, waliomba tuwape namba za simu na tusitume fedha wanafuatilia suala letu na tukaondoka polisi,” anasema.

Anaongeza kuwa walikaa siku mbili bila kupata mrejesho kutoka polisi juu ya uchunguzi, wakati huohuo, watekaji waliwatumia ujumbe mwingine ulioandikwa nyuma ya kalenda ya zamani ukiwa na nguo alizokuwa amevaa Moureen.

“Ujumbe huu ulieleza kuwa wao watekaji walikuwa hawana nia kumpoteza mtoto wetu lakini tumetoa taarifa polisi na kwingineko, tusiwalaumu, ukasisitiza tutume fedha la sivyo tutaletewa maiti ya mtoto,” anasema.

Baada ya ujumbe huo tuliendelea kufuatilia kwa kushirikiana na polisi na viongozi wa mtaa bila mafanikio na baadaye simu iliyokuwa inatumika haikuweza kupokelewa tena wala ujumbe kujibiwa.

“Tulianza kuhangaika huku na kule kuwatafuta hatukufanikiwa ila tukasikia kuna watoto wengine watatu wametekwa,” anasema.

Anasema watoto hao walikuwa ni Ikram, Bakari Seleman na Ayoub Fred na kwamba waliamini kutekwa kwa watoto hao kungerahisisha kupatikana kwa mtoto wake.

“Ila jioni Agosti 31 tulipata taarifa    za kuachiwa watoto wawili tukawa na imani kuwa na mtoto wetu huenda wangeachiwa,” anasema.  

Hata hivyo, anasema Moureen hakuonekana  na jitihada za kumpata zilionekana kuanza kukwama.

“Tuliamua kuungana na mwenyekiti wetu wa mtaa, Daudi Safari kuwasaka watuhumiwa kupitia mtandao wa simu,” anasema.

 

Wakala wa fedha anaswa

Anasema walifanikiwa kumkamata wakala wa fedha wa mitandao ya simu aliyetoa Sh300, 000 ambazo zilitumwa na babu yake Ikram kwa Athuman Seleman ambaye simu yake ilitumika kuomba fedha.

“Baada ya hapo tuliendelea na msako na baada ya siku mbili tulipata taarifa za kukamatwa mtuhumiwa mkoani Geita ambaye siku inayofuata aliletwa Arusha.

“Baada ya kukamatwa tulipata amani kwani alikiri kuwateka watoto wetu na angekuja kuwaonyesha, lakini kwa masikitiko makubwa alionyesha maiti za watoto ambao alikwisha kuwaua,” anasema.

Kwa upande wake babu wa Ikram, Kassim Silim anasema mjukuu wake alitekwa Agosti 26 saa 12 jioni akiwa anacheza na wenzake.

Anasema watekaji walituma ujumbe wakitaka Sh4.5 milioni kumwachia, lakini baada ya majadiliano na kuwaomba sana walikubali kupokea Sh300, 000.

Kabla ya kutuma fedha hizo walikubaliana kuonana eneo jirani na uwanja wa Shule ya Msingi Lucky Vicent usiku ili kuwakabidhi fedha.

Hata hivyo, anasema alifanikiwa kwenda na gari na alipokaribia aliona vijana zaidi ya watano kwenye migomba, mmoja akimpigia simu ajitokeze kuonana nao.

“Nilivyowaona vijana wengi nikaona usalama wangu upo hatarini ndipo niliona nisiwaone nipige simu polisi ili waje lakini polisi hawakutokea,” anasema.

Anasema baada ya hapo alikwenda hadi njiapanda ya kuingia shuleni Lucky Vicent kwenye eneo ambalo huegeshwa pikipiki kisha aliwapigia tena simu.

“Niliongea nao na wakaniambia wananiona, kwanini nimewapita walipokuwa?  Kutokana na kuwa ni usiku na nilihisi usalama wangu kuwa hatarini sikurudi,” anasema.

Anasema badala yake, aliamua kuwatumia Sh300,000 kwenye simu ya  Samson Petro lakini hata hivyo, hawakumrudisha mtoto wakidai ametoa taarifa polisi.

“Baada ya hapo tuliendelea kuhangaika usiku na mchana kwenda polisi na kurudi hadi Septemba 7 tulipopata taarifa za kuonekana miili ya watoto wetu wakiwa wamefariki,”anasema.

 

Maisha ya mtekaji

Lina Kajuna ni mmiliki wa nyumba ambayo alikuwa anaishi mtuhumiwa wa utekaji nyara, Samson Petro ambaye alikuwa anaishi na kaka yake ambaye ni askari wa FFU, Masorogo Msibha eneo la Uzunguni Olasiti.

Kajuna anasema Petro alihamia Arusha, Juni mwaka huu na kukaa naye, lakini tangu alipohamia kwenye nyumba hiyo alikuwa akifanya matukio ya uhalifu.

“Tulianza kuibiwa ndani, mimi niliibiwa kuku na fedha, kwani tuligundua alikuwa ametoboa paa katika chumba chake,” anasema.

Anasema alikwenda kulalamika kwa balozi Daniel Kichau na walianza kumfuatilia, lakini baadaye yalipoanza matukio ya utekaji alitoweka.

“Tangu Agosti 25 sikuwahi kumuona hapa nyumbani hadi nilipomuona kwenye luninga akituhumiwa kuteka watoto,” anasema.

Petro Samson alikamatwa Katoro mkoani Geita ambako alifanya tukio jingine la utekaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulamba alisema mtuhumiwa alikamatwa katika nyumba ya wageni ya Shitungulu  saa mbili usiku.

Mtuhumiwa alikuwa amemteka mtoto mwingine, Justin Ombeni (2) Septemba Mosi nyumbani kwao na alikuwa amemficha chumba namba 103 katika nyumba hiyo ya kulala wageni.

Hata hivyo, baada ya kukamatwa ndipo alikiri kuhusika na matukio ya utekaji Arusha ambapo baadaye alisafirishwa hadi Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo anasema baada ya kufikishwa Arusha, jitihada kubwa zilifanywa kumshawishi mtuhumiwa kuonyesha watoto walipo.

“Tulimhoji na alituonyesha maeneo ya Njiro lakini baada ya kumbana zaidi ndipo alieleza aliwauwa watoto na kuwatumbukiza kwenye shimo la choo eneo la Olasiti,” anasema.

Baada ya kuonyesha eneo hilo miili ilipatikana, lakini siku iliyofuata aliahidi kuwapeleka polisi eneo la Mkonoo nje kidogo ya Jiji la Arusha, kuonyesha watuhumiwa wenzake.

Hata hivyo, anasema wakiwa katika eneo hilo, alitaka kutoroka na ndipo alipigwa risasi iliyomjeruhi na baadaye alifariki dunia akiwa hospitali.

 

Serikali ilivyopokea tukio hilo

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anasema Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo, ilipokea kwa mshtuko tukio hilo la utekaji.

Anasema waliagiza kufanyika msako mkali dhidi ya watuhumiwa wote ili kuvunja mtandao huo na ndipo baadaye mtuhumiwa mkuu alipatikana.

-->