Siku 667 zawakutanisha Lipumba, Lowassa msiba wa Kitwana Kondo

Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof Ibrahim Lipumba walipokutana kwenye msiba wa Kitwana Kondo, Upanga jijini Dar es Salaam jana. Picha na Bakari Kiango

Muktasari:

Wawili hao walikutana kwa mara ya mwisho Julai 28, 2015, wakati Lowassa alipokuwa anatambulishwa kujiunga na Chadema kisha kuteuliwa kugombea urais kupitia Ukawa.

Dar es Salaam. Msiba wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Kitwana Kondo, umewakutanisha waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa na mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ikiwa ni siku 667 tangu wapeane mkono kwa mara ya mwisho.

Wawili hao walikutana kwa mara ya mwisho Julai 28, 2015, wakati Lowassa alipokuwa anatambulishwa kujiunga na Chadema kisha kuteuliwa kugombea urais kupitia Ukawa.

Hatua hiyo ya Lowassa kuteuliwa kugombea urais ndiyo sababu ya Profesa Lipumba kujiuzulu wadhifa wake CUF akidai dhamira ilikuwa inamsuta.

Baada ya mwaka mmoja, Profesa Lipumba aliandika barua ya kutengua uamuzi wake, lakini Mkutano Mkuu wa CUF uliridhia uamuzi wa kujiuzulu kwake.

Lakini miezi 21 baadaye, wawili hao wamejikuta wakikutanishwa katika mazishi ya Kitwana Kondo aliyefariki dunia juzi kwenye Hospitali ya Hindu Mandal. Alizikwa jana kwenye makaburi ya Tambaza.

Katika msiba huo, viongozi mbalimbali walihudhuria akiwamo Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru. Wengine waliofika kuhani msiba huo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Valentino Mlowola.

Lipumba aliwasili saa saba katika msiba huo uliofanyika nyumbani kwa marehemu Upanga na baada ya muda mfupi aliwasili Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Baada ya swala ya mchana ya kuuombea mwili wa marehemu, Profesa Lipumba alisalimiana na baadhi ya viongozi na watu mbalimbali wakati akirejea kwenye kiti chake alimfuata Lowassa ambaye naye aliinuka alipokuwa ameketi na kusalimiana kwa kupeana mikono kwa sekunde kadhaa.

Akimzungumzia marehemu, Profesa Lipumba alisema alimfahamu Kitwana Kondo wakati akiwa msaidizi wa Rais Mwinyi, na kwamba alikuwa mmoja wa Watanzania wenye mchango mkubwa katika Taifa.

“Mchango wake unatambulika tangu akiwa Inspekta wa Polisi, enzi za wakoloni. Ndiye aliyekisaidia Tanu kujua mambo mbalimbali yanayoendelea.

“Taifa limepoteza mtu mkubwa na mzito. Bahati mbaya Taifa hili halina historia ya kutambua michango ya watu wake kama alivyokuwa Kondo,” alisema Profesa Lipumba.

Kwa upande wake, Lowassa alimshauri Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuipa jina la Kitwana Kondo moja ya barabara za jijini hapa ili kumuenzi kiongozi huyo.

Lowassa alisema aliwahi kufanya kazi na Kitwana na kwamba waliweza kukubaliana au kutokukubaliana, lakini kazi zilikuwa zinakwenda. “Namuomba Meya Jiji la Dar es Salaam (Isaya Mwita) afanye utaratibu kwa kuipa jina la KK (Kitwana Kondo) mojawapo ya barabara,” alisema Lowassa.

Baada ya Lowassa kutoa wazo hilo baadhi ya watu msibani hapo walisikika wakisema ‘great idea’ wazo zuri ametoa.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu ombi hilo, Mwita alijibu kwa ufupi kuwa : “Nimelichukua,”

Rais mstaafu Mwinyi alisema Kitwana alikuwa mtu mkweli ambaye hakupenda kudanganya watu na akiwa na shida anakueleza ili umsaidie.

“Alikuwa mtu wa masihara, lakini ujumbe aliufikisha. Alikuwa pia ni mwalimu wa wengi nikiwamo mimi,” alisema Mwinyi.

Katibu Mkuu wa CCM, Kinana alisema msiba wa Kitwana ni wa wanaDar es Salaam na Watanzania wote kwa ujumla kwa sababu alikuwa ni kiongozi wa ngazi mbalimbali ikiwamo ya kijamii.

“Alikuwa na kipaji cha kusema, hasa methali zilizokuwa zikiendana na wakati,” alisema Kinana.

Mtoto wa kwanza wa Kitwana, Stara Kitwana alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza sehemu ya kichwa na alilazwa siku 10 katika hospitali ya Hindu Mandal kabla ya mauti kumfika.