Siku saba bila Mo Dewji, wananachi watumia mitandao ya kijamii kuhoji alipo

Muktasari:

  • Leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 ni siku ya saba tangu alipotekwa mfanyabiashara maarufu Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’
  • Watu wa kada mbalimbali nchini Tanzania wanatumia mitandao ya kijamii kuhoji alipo mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ na kutaka waliomteka kumrejesha

Dar es Salaam. Leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 ni siku ya saba tangu alipotekwa mfanyabiashara maarufu Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo limewagusa maelfu ya Watanzania ambao leo kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wameandika ujumbe mbalimbali wakitaka juhudi zaidi zifanyike kumpata bilionea huyo, baadhi kushangazwa kupita siku saba bila Mo Dewji kupatikana.

Dewji alitekwa alfajiri ya Alhamisi ya Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi.

Juzi, familia ya mfanyabiashara huyo imetangaza donge nono la Sh1bilioni kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa bilionea huyo kijana.

Katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Carol Ndosi amesema, “ Tunaoendelea na shughuli kama kawaida kwa kuamini ‘na hili litapita’ ni kwamba halijatufikia bado mlangoni. Tunaona  jinsi linavyozidi kufika kwa jirani, ndugu, jamaa na marafiki. Kama nchi inabidi tuamue kwa pamoja. Enough is enough. Usisubiri libishe hodi mlangoni.”

Flaviana Matata ameandika, “Kila mtu ninayekutana naye anaulizia kuhusu Mo Dewji ,tumuombee jamani.”

Kwa upande wake Giddy amesema siku saba Mo Dewji bado hajapatikana na hakuna hata taarifa ya awali ya kueleweka iliyotolewa, “Mungu aendelee kukupigania huko uliko na urudi salama. Bring Back our Mo.”

Halima Mdee amesema “Siku Saba BringBackourmo”, huku Ismail Jussa akisema, “leo ni siku ya saba. Hatuwezi kukaa kimya Bringbackourmo.”

Naye Dk Joachim Mabula amesema, “natamani ingekuwa inawezekana kuamua kama nchi ila haiwezekani.

Watoa uamuzi  pengine hawana muda kabisa na kelele za watu. Nimesikia pia Wizara ya Mambo ya Ndani haihitaji msaada kutoka nje. Kama mwananchi wa kawaida nimekwamba kifikra naomba nisikie fikra za wengine.”

Maria Sarungi amesema, “wiki moja iliyopita (alhamisi iliyopita) asubuhi kama hii, nchi ilitikiswa kwa taarifa ya kushtua ya kutekwa kwa@moodewji siku saba!wiki moja bado hamna taarifa.”

Maxence Melo amesema, “ni vigumu kuendelea kunyamaza wakati @moodewji akiwa hajulikani alipo. Inasikitisha kuwa tumefikia hatua kama hii kama Taifa na inaogofya juu ya usalama wa kila Mtanzania.”