Simanjiro yapata Sh27.9 milioni mnada wa Tanzanite

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi amesema pia, wamepanga kukusanya kodi ya huduma kupitia madini ya Tanzanite ili kuongeza mapato ambayo kwa kiwango kikubwa yanategemea mchanga na kuni.

Mirerani. Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, imepata Sh27.9 milioni kwenye mnada wa Tanzanite uliofanyika jijini Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi amesema pia, wamepanga kukusanya kodi ya huduma kupitia madini ya Tanzanite ili kuongeza mapato ambayo kwa kiwango kikubwa yanategemea mchanga na kuni.

Myenzi amesema kwa muda mrefu halmashauri hiyo ilikuwa haipati kodi ya huduma kutoka kwa wachimbaji madini hayo, ila baada ya kukutana na kuzungumza nao anatarajia hali itabadilika.

“Haiwezekani tuwe na madini ya Tanzanite halafu tuwe tunategemea kupata fedha kupitia mchanga na kuni tu, tunaendelea kuzungumza nao ili wamiliki wa migodi watupe ushirikiano,” amesema.

Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya amesema ingawa madini hayo yapo sehemu hiyo pekee, jamii ya eneo hilo haijanufaika nayo ipasavyo kwa sababu kuna changamoto ya huduma za jamii.