Simba afanyiwa upasuaji kwa saa tatu

Madaktari wa wanyama wakimfanyia upasuaji simba aliyekuwa na uvimbe mwilini mwake katika Hifadhi ya Ngorongoro, Arusha jana.Picha na (WMU).

Arusha. Madaktari wa mifugo wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Wanyamapori (Tawiri) wametumia saa tatu kumfanyia upasuaji simba aliyekuwa na uvimbe.

Simba huyo alikuwa eneo la Kreta Ngorongoro ambako muda mwingi alionekana akiwa amekaa peke yake na taarifa za awali zilieleza kuwa huenda alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa ngiri ambao ulimsababishia uvimbe.

Upasuaji huo ulianza saa saba mchana hadi saa 10 jioni kwa ufanisi mkubwa na mara baada ya kukamilika, madaktari walieleza kuwa watakapojiridhisha kuhusu afya yake, watamwachia ajiunge tena na wenzake.

Awali, ofisa wa idara ya uhusiano NCAA, Nickson Nyange alisema, “Muda huu madaktari na watafiti wanaendelea na upasuaji kuokoa maisha ya simba huyu, ambaye amekuwa ni mmoja wa vivutio vya utalii katika hifadhi yetu.”

Alisema madaktari na maofisa wa NCAA na Tawiri leo watatoa taarifa kamili za kitaalamu juu ya ugonjwa uliokuwa unamkabili simba huyo.