Simba yaizima Yanga Zanzibar

Muktasari:

Simba sasa itacheza na Azam baada ya kuizima Yanga kwa mikwaju ya penalti katika mchezo mkali wa nusu fainali ya pili uliofanyika kwenye Uwanja wa Aman, Zanzibar.

Zanzibar. Penalti nne zimetosha kuifanya Timu ya Simba kuingia fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuicharaza Yanga iliyoambulia mbili.

Simba sasa itacheza na Azam baada ya kuizima Yanga kwa mikwaju ya penalti katika mchezo mkali wa nusu fainali ya pili uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Baada ya Simba kupata penalti tatu zilizofungwa na Jonas Mkude, kipa Daniel Agyey na Muzamir Yassin huku Yanga zikifungwa na Simon Msuva na Thaban Kamusoko ilibakia moja kila upande.

Ikawa sasa kila mmoja anamwangalia Janvier Bokungu, ambaye alikuwa anakwenda kupiga penalti ya tano kwa Simba hapo tayari Method Mwanjali (Simba) na Deo Munish na Haji Mwinyi walikuwa wameshakosa penalti zao.

Awali kabla ya mikwaju hiyo kila upande ulifanya mashambulizi ya kushtukiza na kutegeana, Simba ilicheza kwa kujihami zaidi ikitumia mfumo wa 4:5:1 huku Yanga ikitumia 3:5:2.

Yanga ilifanya badiliko moja pekee katika kikosi chake kilichopoteza mchezo uliopita dhidi ya Azam FC wakati Simba ilikuwa na mabadiliko ya wachezaji watatu katika kikosi kilichocheza mechi ya mwisho na Jang’ombe Boys.

Katika hatua nyingine, Azam imemtangaza Aristica Cioaba raia wa Romania kuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa mkataba wa miezi sita kuanzia sasa.

Cioaba ametokea katika klabu ya Aduana Stars iliyomaliza nafasi ya pili katika ligi ya Ghana na ataungana na mastaa wa zamani wa timu hiyo, Yahya Mohammed na Yakub Mohammed ambao wanacheza Azam.