Simulizi ya mateso ya wajawazito yawaunganisha wanakijiji Geita

Muktasari:

Wajawazito 84 walipoteza maisha wakati wa kujifungua mkoani Geita 2017, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua.

Wajawazito wanne walifariki katika Wilaya ya Mbogwe mwaka huo.

Idadi ya watoto 37 waliozaliwa ama wamekufa au waliofariki dunia baada ya kuzaliwa wilayani humo katika kipindi hicho.

Mbogwe. “Nilipatwa na uchungu saa tisa alasiri, nikatafuta baiskeli ya kunipeleka Zahati ya Nyanulinga, nilianza safari saa 10 jioni nikafika saa mbili usiku nilihudumiwa na kujifungua mtoto wa kiume saa tano usiku,” hayo ni maneno ya Felista Francis.

Felista ni miongoni mwa wanawake wengi wa Kijiji cha Omolwa wilayani Mbogwe mkoani Geita wanaolazimika kusafiri kwa baiskeli umbali wa zaidi ya kilomita 25 kufuata huduma za afya katika Kituo cha Afya Masumbwe. Huko pia ndiko wanakojifungulia.

Kutokana na mateso hayo, wakazi wa kijiji hicho wameamua kujifunga mkanda na kuanza ujenzi wa kituo cha afya ili kuondokana na vifo vya mama na watoto vinavyosababishwa na umbali wa huduma za afya.

Wakizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ya kukagua miradi ya maendeleo, miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho akiwamo Felista, walisema wajawazito wengi hujifungulia nyumbani kwa kutegemea wakunga wa jadi na inaposhindikana hutumia usafiri wa baiskeli kwenda Masumbwe.

“Huku huwezi kupata gari wala pikipiki, usafiri wetu ni baiskeli, ni mateso makubwa, ndiyo maana tumeungana tujenge hospitali yetu wenyewe,” alisema Felista.

Pili Paulo ambaye ni mama wa nyumbani, alisema kutokana na huduma kuwa mbali wanawake wengi hushindwa kuhudhuria kliniki wakiwamo wajawazito na hata wakijifungua, watoto hawapelekwi kliniki kama inavyotakiwa. “Huku ni kama jangwani, hakuna huduma ya hospitali wala huduma ya maji, akinamama wanateseka sana jamani tusaidieni,” alisema Pili.

Joseph Pongano anayejishughulisha na kilimo, alisema wamechoshwa na adha wanayopata hasa wanawake wanapoumwa uchungu nyakati za usiku ndiyo maana wakaamua kuja na mpango wa kutatua suala hilo.

Alisema katika utekelezaji wa suala hilo wameamua kuanza ujenzi kwa kuchangia fedha na kusomba mawe pamoja na mchanga. “Tumechoka kuwazika watoto na wajawazito, unaweza kumuona mjamzito akiwa amezidiwa amebebwa kwa baiskeli anapelekwa hospitali, kutokana na umbali hafiki, anafia njiani. Hii ni kero lazima tuimalize,” alisema Pongano.

Viongozi waunga mkono

Diwani wa kata hiyo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Vicent Busiga alisema kutokana na adha ya kupata huduma za afya, wananchi wameamua kujenga kituo hicho cha afya kwa gharama zao.

“Kijiji kina kaya 350, tulikaa na kuona hatuwezi kutoka hapa kama hatutaanza wenyewe, tulifanya mkutano na tukakubaliana kila kaya ichange Sh50,000, tukakusanya Sh32.5 milioni, mimi nikachangia Sh19.3 milioni tukaanza ujenzi 2013 na hadi sasa tunaendelea,” alisema Busiga.

Alisema baada ya mwamko wa wananchi kuwa mkubwa, halmashauri imewasaidia kwa kuwapatia Sh46.2 milioni, fedha ambazo zimesaidia jengo la kituo cha afya kuezekwa bati.

Kutokana na kuguswa na kazi kubwa iliyofanywa na wananchi wa kijiji hicho, Mkuu wa Mkoa, Gabriel aliahidi kuwa Serikali itatoa Sh100 milioni zitakazotumika kumalizia ujenzi wa majengo hayo.

Mganga mkuu wa mkoa, Josephat Simeo alisema majengo hayo yaliyojengwa na wananchi kwa ukubwa wake yatasaidia kupatikana kwa wodi ya watoto, wajawazito na chumba cha upasuaji na kujifungulia.