Simulizi ya msomi aliyerudia mtihani wa kidato cha nne mara nne

Muktasari:

Kila anapojikwaa, hujizoazoa na kuamka. Ujasiri wa kupambana na hali yake hadi kuzishinda changamoto zilizoelekea kuwa kikwazo katika maisha yake, umemfanya kuwa mmoja wa watu wa kupigiwa mfano.

Hebu pata picha ya mtu anayejikwaa barabarani tena sehemu ileile aliyoumia jana na juzi, lakini bado yumo; haoni shida wala kukata tamaa au kufikiria kuchepukia barabara nyingine.

Kila anapojikwaa, hujizoazoa na kuamka. Ujasiri wa kupambana na hali yake hadi kuzishinda changamoto zilizoelekea kuwa kikwazo katika maisha yake, umemfanya kuwa mmoja wa watu wa kupigiwa mfano.

Mtu aliyejikwaa mara kadhaa na hatimaye kupata ufumbuzi, ni Clement Fumbuka ambaye sasa ni mtaalamu wa ufugaji kwa ngazi ya elimu ya juu. Na ili watu wajue kukata tamaa katika maisha ni kosa kubwa, Fumbuka ametunga kitabu kiitwacho “Jijenge kimawazo: Anguka mara 7 simama mara 8”.

Kitabu hiki kinaakisi maisha yake; maisha ya kutokata tamaa maishani. Laiti angekuwa na aibu ya kusimulia yaliyomtokea miaka 13 iliyopita au angekuwa mchoyo, angeinyima jamii ya Kitanzania siri ya mafanikio ya kielimu aliyo nayo.

Fumbuka anatudhihirishia kuwa maisha ni mapambano, hakuna kukata tamaa maishani. Mikasa aliyokutana nayo katika safari yake kielimu leo inatumika kwa wengi kama funzo lenye kushibisha.

Kufikia kuwa mtu mwenye elimu ya chuo kikuu na kipaji cha uandishi wa vitabu, Fumbuka “alianguka chini mara nne, na akasimama”. Hapana, hakuanguka chini bali alishindwa mtihani wa kidato cha nne mara nne na bado alirudia kwa bidii hadi akafaulu.

Kitabu cha hamasa

Unaweza kukiita kitabu chenye mafundisho ya hamasa kuhusu harakati za kuzikabili changamoto za maisha. Ametumia saikolojia, mafundisho ya kidini, ufundi wa lugha na mifano kadhaa kuelezea kwa nini binadamu hapaswi kukata tamaa.

Mbali ya kitabu “Jijenge kimawazo: Anguka mara 7 simama mara 8” kinachosimulia harakati za maisha, pia ametunga vitabu vingine kama “Hujashindwa ndoto yako” (2015), “Mtunze kuku akutunze”(2016) kinachozungumzia ufugaji wa kuku.

Safari yake kielimu

Kitabu chake kinasadifu maisha binafsi. Hakuandika kitabu mithili ya riwaya za kufikrisha, bali kudhihirisha kwamba mtu anaweza kuanguka mara saba na akasimama mara nane kwa ujasiri na sasa ni mtaalamu wa mifugo, elimu aliyoyapata kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Mwaka 2004 kwa mara ya kwanza alifanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Geita na kujikuta akifutiwa matokeo kwa sababu anazosema hakuzifahamu.

“Sikujua kama nilifaulu au la. Kutokana na sababu za kiuchumi, sikuweza kufuatilia chanzo cha kufutiwa, kwani wazazi hawakuweza kugharimia ufuatiliaji,” anasema

Huu ukawa kama mwanzo wa kinachoweza kusemwa kama nuksi. Baada ya hapo alijaribu mara kadhaa kurudia mtihani huo lakini hakufanikiwa.

“Niliamua kujisajili katika kituo cha kujiendeleza watumishi walioko kazini na elimu ya watu wazima (Klasta)). Hapo nilifanya mtihani kama mtahiniwa binafsi. Mazingira hayakunipa nafasi nzuri kujisomea na kujiandaa vema kama ilivyo kwa mtahiniwa wa shule,” anasema.

“Sikuwa na tatizo lolote niwapo kwenye chumba cha mtihani. Changamoto za kawaida wakati mwingine zilijitokeza lakini hazikuwa tatizo kubwa kunikatisha tamaa. Nakumbuka mara ya kwanza kufanya mtihani katika kituo cha Klasta, msimamizi wa mtihani alinipa mtihani wa Engineering Physics badala ya Basic physics. Baada ya saa moja na nusu tangu mtihani uanze, msimamizi alishtuka na kunifuata. Alifika na kunitaka radhi kuwa mtihani alionipa siyo wangu, bali amekosea kunipa mtihani wa mtu mwingine ambaye alikuwa anafanya mtihani wa somo hilo,” anasimulia.

Anasema wakati wote wa kurudia mitihani mwaka hadi mwaka, ndugu, jamaa na marafiki waliungana naye mwanzoni, lakini mwishowe walimchoka wakiamini ni sawa na mtu anayetwanga maji kwenye kinu au alikuwa fungu la kukosa.

“Marafiki wengi walianza kuniambia niachane na shule kwani maisha si lazima niwe nimesoma tu. Ndugu zangu walianza kunishauri nifanye biashara. Kaka yangu mmoja alijitokeza na kutaka kunipa mtaji nianze biashara. Wazo lake sikulikataa lakini nilimwambia anitunzie mtaji nikishindwa kabisa ndipo anipe mtaji huo. Niliendelea tena kulipia mtihani kila mwaka hadi nilipofaulu na kupata vigezo vya kuendelea na kidato cha tano,” anaeleza.

Fumbuka anakumbuka mtihani wake wa kwanza alipoanza kurudia matokeo yalikuwa; Kemia (B), Biolojia (D), Fizikia (D), Jiografia (D), Kiswahili (D), Uraia (D), Kiingereza (D), Hisabati (D) na Historia (F).

Ndoto yake anasema ilikuwa kusoma tahasusi za PCB au PCM, hivyo kwa matokeo hayo akawa na deni la kutafuta angalau alama C katika masomo ya Fizikia na Biolojia.

Mwaka 2006 akarudia masomo matatu: Fizikia, Hisabati na Biolojia. Matokeo yakawa Biolojia (C), Fizikia (D) na Hisabati (D) hivyo bado akawa anadaiwa angalau C moja ya kumpa sifa ya kujiunga na kidato cha tano.

“Baada ya matokeo hayo nilipata matumaini mengine, nikaamua kwenda kusoma ‘Pre-form five’ (masomo ya kujiandaa kwa kidato cha tano) katika sekondari ya Buluba iliyopo Shinyanga, huku najipanga kurudia tena kusafisha matokeo yangu.

‘’Shule niliyokwenda kusoma, haikuwa na tahasusi za PCB na PCM, badala yake kulikuwa na CBG (Kemia, Biolojia na Jiografia). Niliamua kusoma CBG mwaka 2007 na wakati huohuo nililipia tena mtihani wa kidato cha nne na kufanikiwa kupata C ya Jiografia. Alama hii ikanipa sifa ya kusomea CBG na hivyo nikawa na ruhusa ya kwenda kidato cha sita,” anaeleza.

Huo ukawa mwanzo wa safari ya kuelekea kuipata shahada ya kwanza aliyonayo sasa. Baada ya kuhitimu masomo ya kidato cha sita alijiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo mwaka 2009.

Fumbuka ambaye sasa ni mfanyakazi katika Chuo cha Kilimo na Mifugo cha Kilacha mkoani Kilimanjaro anasema, jinamizi la kufeli halikumwandama hadi alipofanikiwa kuhitimu masomo mwaka 2012.

Tena chuoni alikuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wenzake. “Kutokana na uwezo wa kueleza kitu mpaka mtu akaelewa haraka, wanafunzi wenzangu walipenda niwafundishe na pengine waliniomba niende chuoni kuwasaidia kipindi cha likizo, walipokuwa wakirudia mitihani,” anasema

Moyo wa kutokata tamaa

Siku zote anasema aliamini kuwa angefanikiwa kufikia kiwango cha elimu alichokitamani ndiyo maana matokeo mabaya katika mitihani hayakuwa sababu ya kumkatisha malengo yake.

“Kila matokeo ya mtihani yalipotoka yalinipa akili mpya kurudi tena darasani kuendelea na mapambano, huku akilini nikiwa na msemo; ‘Mapambano ni sehemu ya maisha, kushindwa au kushinda kupo kwenye mikono ya Mungu),” anaeleza.

Moja ya vitu vilivyomsukuma kutokata tamaa katika safari yake ya elimu ni kuchukia maisha duni na kutaka kutafuta suluhisho la kuwa na maisha bora nyumbani. Sababu nyingine anasema ni nguvu iliyomvuta kutimiza malengo yake kama vile kuona watu waliofanikiwa kupitia ndoto yake na kumtia moyo kuwa atafanikiwa kama wao.

Sababu ya tatu anaeleza ni; “Nguvu ya ndani ya nafsi. Nguvu hii ilikuwa kubwa kuliko sababu zote zilizonifanya kuendelea kurudia mitihani. Nguvu hii haikukauka moyoni, kila mara nilisikia mahojiano ya nafsi mbili moyoni.”

Anasema nafsi moja aliisikia ikilalamika kwa mateso mengi na kutaka kukata tamaa na nafsi nyingine ilikuwa inahoji kama ataamua kukata tamaa kusoma, je hatakuja kujutia maamuzi hayo hapo baadae? Na kama anaamini tangu mwanzo kuwa elimu ndiyo silaha muhimu kuliko chochote katika maisha yake, je atatumia silaha gani kuyakabili maisha?

“Watu wengi walitokea kunikejeli na kunibeza lakini sikuona majibu ya maswali haya tofauti na kuhakikisha nimefikia elimu ninayoitaka.’’

Mazingira ya nyumbani

Kama ilivyo kwa jamii nyingi za Kitanzania mazingira ya nyumbani kwao katika kijiji cha Nkungulu wilayani Kwimba hayakuwa rafiki kwake.

Kila siku alikwenda shambani lakini alihakikisha kila ifikapo jioni anakwenda kulala Kwimba mjini ambako ni umbali wa kilomita nane kutoka kijijini. Alifanya hivyo kutunza akili ya kutobadili fikra za kusoma.

Changamoto nyingine iliyomkabili ni ya kukosa fedha za kugharimia masomo yake, hali iliyomlazimisha kufanya shughuli kama kuchoma mkaa na kukata kuni.

Wito wake kwa Watanzania

Fumbuka anawasihi Watanzania kufanya maamuzi na kusimamia ndoto ya malengo wanayojiwekea.

“Binafsi pamoja na kupanga kufanya mambo mengi, mengi yalichelewa kufanikiwa, lakini hakuna jambo ambalo nilipanga na kulisimamia likaja tofauti. Nimekuwa mtu wa kumshukuru Mungu kwa kutimiza ndoto zangu na malengo mbalimbali ambayo nilijiwekea. Subira, uvumilivu na kujituma katika mipango ni mambo matatu ambayo kwangu yamenifanya nifikie malengo,” anasema.

Wasifu na familia

Anasema, “Nyumbani tulizaliwa watoto 14 tukiwa wote ni watoto wa baba mmoja na mama mmoja. Hadi sasa tulio hai ni watoto 13, mimi ni mtoto wa 12. Katika watoto wote, mimi pekee nimefanikiwa kufika elimu ya juu. Wawili walifanikiwa kuhitimu kidato cha nne lakini hawakuendelea, wengine 10 waliishia darasa la saba.”