Simulizi ya mwanamke aliyepambana na mamba – 4

Abadallah Makamba ambaye ni dereva wa ngalawa akionyesha eneo ambalo walimwokoa Marita Malambi aliyeshambuliwa na mamba katika Kijiji cha Dakawa Ukutu, mkoani Morogoro. Picha na Herieth Makwetta

Muktasari:

  • Kutokana na wanakijiji wengi kuelekeza shutuma zao kwa uongozi, mwandishi alifunga safari hadi kwa mtendaji wa Kijiji cha Dakawa Ukutu, Salumu Lunyovi kusikia upande wa pili.

Jana tuliangalia mikasa mbalimbali ya watu waliopotea ikiaminika kuwa ni katika Mto Mgeta na Kituo cha Afya Duthumi kikisema watu 39 walitibiwa kwa kushambuliwa na mamba huku wakiituhumu serikali ya kijiji kwa kutoshughulikia tatizo hilo. Leo tunaangalia majibu ya Serikali hiyo hususan hatua ambazo imechukua kutatua kero ya maji na kiini cha mamba hao.

Tatizo ni Sh76 milioni

Kutokana na wanakijiji wengi kuelekeza shutuma zao kwa uongozi, mwandishi alifunga safari hadi kwa mtendaji wa Kijiji cha Dakawa Ukutu, Salumu Lunyovi kusikia upande wa pili.

Kwanza anajibu madai kwamba uongozi hauonekani kujishughulisha na masaibu hayo akisema wamewahi kuokota maiti ya Msinune Abdallah ambaye alipotea na kwa jitihada zao na wanakijiji waliuona mwili wake.

“Tumewahi kuokoa maisha ya vijana wawili wa kiume, Bashiri Jamlolo na Fidia Bakari wao walikoswakoswa kwenye Mto Kibwaya unaoumwaga maji yake Mto Mgeta,” anasema.

Anakubaliana na wanakijiji kwamba matatizo hayo yanatokea kwa kiwango kikubwa kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya maji jambo linalowalazimu kuyafuata mtoni.

Anasema licha ya Serikali kufanikiwa kutatua tatizo la umeme kupitia mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), tatizo la maji ni kilio cha muda mrefu kinachohitaji ufumbuzi wa haraka.

“Tunamuomba Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwele atutembelee. Tuliwahi kuzungumza na wenzetu wa Selou wakawaleta wataalamu wao kupima tukaelezwa kuwa bajeti ni Sh76 milioni, walisema mkiweza kutoa fedha hizi maji yataunganishwa kutoka Matambwe mpaka Dakawa.”

Lunyovi anasema kutokana na ufinyu wa fedha kijijini, wameshindwa kupata maji hivyo wanaiomba wizara iangalie suala hilo ili kunusuru maisha ya watu.

Alipoulizwa kuhusu kuwashirikisha wananchi masuala ya maendeleo anasema, “Huwa tunakutana kwa mwezi mara moja kile kinachostahili kuwaeleza tunawaeleza ili wafahamu nini kinachoendelea.”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Dakawa, Hassan Mwanga anasema kati ya vijiji vinne vya Kata ya Bwakilachini, cha kwake ndicho chenye changamoto nyingi, kubwa ikiwa ya maji inayosababisha madhara makubwa.

“Wananchi zaidi ya watano wamepambana na mamba na wakatoka wazima japokuwa wengi hufariki.”

Mwanga anasema wamekuwa wakitoa elimu ya namna ya kuchota maji kwa kifaa chenye mti mrefu badala ya kuingia ndani ya mto, lakini wengi hukaidi na uongozi wa kijiji hauwezi kuwazuia wasiende mtoni kwa kuwa kijiji hakina vyanzo vingine vya maji.

“Tuna chombo chetu kinaitwa Jukumu Society kwa ajili ya kufuga wanyama, huwa tunawasiliana na wenzetu wanakuja na kuwaondoa hawa wanyama lakini huu mwaka wa pili hawajaja,” anasema.

Anasema watu kadhaa wameshambuliwa na viboko, tembo na mamba, wengine wanakufa, lakini wapo wanaookolewa.

Mwanga anasema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwani zaidi ya 300 huvuka ng’ambo ya mto huo kila siku kutokana na shughuli za kilimo.

“Nimewaambia kupitia mikutano kwamba wanaokwenda kuchota maji wasiingie ndani ya mto, wasioge na wale wanaovuka ng’ambo wasivuke chini ya mto watumie mitumbwi iliyochongwa ili kunusuru maisha yao,” anasema Mwanga.

Kuhusu ushirikishwaji, Mwanga anasema kila tarehe 25 ya mwezi hufanya mkutano na hupokea mawazo ya wanakijiji na kuyafikisha juu, lakini anasema sauti yake inaishia kwenye Kata ya Bwakilachini.

“Namuomba Waziri wa Maji akiangalie hiki Kijiji cha Dakawa Ukutu, asikie kilio chetu cha maji, kama alivyokuja Waziri wa Nishati, aone kama haya yana usahihi. Hapa tuna milipuko ya magonjwa ya kipindupindu, kuhara, homa za matumbo kipindi hiki cha mvua maji yote yanakusanyika pamoja, unapotokea mlipuko kudhibiti kwake kunakuwa kugumu.”

Kauli ya DED

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili anasema mamba waliopo katika mto huo wanatokea eneo liitwalo Milengwelengwe.

Anasema mto huo umepita katika vijiji vya Sesenga, Milengwelengwe, Mngazi, Dakawa, Bwakilachini, Bonye na Mbwade ambako ndiko Kata ya Bwakilachini ilipo.

“Mto huu umeenda Magogoni, Kongwa hadi ukagusa mbuga ya Selou na kidogo ukaingia Kidunda, ambako ndipo ulipoungana na Mto Ruvu kule chini ikitokea Kibaha, kwa hiyo ni mto mkubwa,” anasema.

Mpili anasema katika kila kijiji kuna makao manne hadi matano ya mamba na kwamba linapotokea tatizo la kujeruhi au kuua, hutoa silaha kwa askari wa maliasili ili kumsaka mnyama aliye msumbufu lakini si kuwaua mamba wote kwenye mto.

“Mamba anayefanya fujo anakuwa anatembea sana kwenye maji tofauti na wengine, hawezi kukaa kutulia kama wengine wanaoota jua, anakuwa anazunguka kwenye maji na ndivyo tunavyowagundua.”

Anasema wamekuwa wakiwataka wananchi wanaolima ng’ambo ya mto au kufuata maji kuchukua tahadhari, lakini imekuwa vigumu, “Mto una mamba lakini bado unakwenda kukaa pembeni unaoga au unafua, ule mto hata kuvuka wanabahatisha tu, hata wanaovuka wakifanikiwa ni kwa bahati tu kwa sababu mamba wanaishi kwenye maji yale.”

Anasema kuna tahadhari za uvukaji kwa kutumia mitumbwi au kuteka maji kwa machoteo maalumu kwa umbali na umakini lakini hilo limekuwa gumu kutekelezwa huku akisisitiza kwamba Serikali haiwezi kuua mamba wote.

“Tayari mamba wawili wameuawa lakini siyo kwamba wameisha, tunasisitiza tahadhari lakini pia tumejaribu kutengeneza mifumo ya maji, kuna mradi wa maji mkubwa pale karibu na kituo cha afya, lakini wananchi wanaona vigumu kuyafuata wanakwenda mtoni,” anasema Mpili.

Hata hivyo, kituo hicho cha afya kinahudumia vijiji 18 vilivyopo katika kata mbili za Bwakilachini na Mvuha.

Alipoulizwa kuhusu mradi wa maji Dakawa unaohitaji Sh76 milioni, Mpili anasema awali, Serikali ilijitahidi kuchimba visima vya maji ya kuvuta kwa kamba lakini kwa kuwa kamba hazidumu zilipokatika wananchi hawakufanya juhudi ya kununua nyingine.

“Halmashauri imetenga fedha na tumeiombea Dakawa mradi mkubwa wa maji kwenye bajeti ya mwaka huu kwa hiyo mambo yao yatabadilika tu, lakini pia nitawakumbusha Tanesco kuhusu ahadi yao kupitia mradi wa Stiglers Gorge, basi watekeleze ahadi zao,” anasema Mpili.

Akizungumzia madhara ya mamba katika eneo hilo, Mpili anasema takwimu zinaonyesha watu 39 walifikishwa hospitali baada ya kushambuliwa, lakini hakuna takwimu sahihi za wanaopotea au kutofikishwa hospitali. Anasema pia kwamba si mamba pekee wanaodhuru watu, bali wanyama na wadudu waumao katika eneo hilo ni wengi.

“Vifo vya majini vipo vya aina tofauti, kuna mtu anaweza kung’atwa na viboko, mara nyingi wanajeruhi, wapo wengi wameshashambuliwa kwa kupita maeneo yao. Akikuuma kichwani au kifuani unaweza kufa lakini akimuuma maeneo mengine anakujeruhi. Kiboko anaweza kukuondoa sehemu ya kiungo ukabaki mlemavu.

“Mtu anayefariki kwa kushambuliwa na kiboko mwili wake ni rahisi kupatikana, lakini akishambuliwa na mamba katika mazingira ambayo hayana usumbufu huwa anaanza kumla hapohapo, habakizi kitu. Kwa hiyo kuna mazingira ambayo unakuta labda mtu amevuka mtoni peke yake, akikamatwa na mamba anaweza asionekane tena akapotea kabisa, kama hakuna mwenye taarifa zake.”

Hata hivyo, Mpili anasema kuna vifo vingi katika hayo maeneo, ikiwamo mbugani kwani kuna wanyama wakali kama simba, chui, nyoka na huko kuna watu wanaokwenda kutafuta mawindo au chakula licha ya sehemu hizo kuwa ni hatari.

“Kuna watu wanaondoka peke yao wanaingia msituni kutafuta asali, huyu anaweza kuliwa hata na simba. Wengine wanaweza kugongwa na nyoka wakali huko porini na kufa akiwa peke yake.”

Alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa zahanati katika kijiji cha Dakawa Ukutu, Mpili anasema jengo lililojengwa na wananchi lilitakiwa kuzinduliwa Februari 28 na kwamba tayari wameshapeleka wataalamu ambao wanasubiri kutimiza siku 14 kisheria waende kuripoti akiwamo mganga, wauguzi wawili wazoefu na mwingine mmoja na baadhi ya vifaa vimeshapelekwa.