Simulizi za kusikitisha ajali ya kivuko cha Mv Nyerere

Muktasari:

  • Wakati Ochori Burana na Ruben Pande wakisimulia jinsi walivyonusurika na kifo baada ya kuruka majini na kushikilia tairi la gari hadi walipookolewa, Mitamba Sendeni ameeleza alivyotumia boya kuwaokoa wenzake watatu akiwemo mjamzito.

Ukerewe/Dar. Kuzama kwa Kivuko cha Mv Nyerere kumeacha simulizi za kusikitisha kutoka kwa manusura wa ajali hiyo iliyotokea siku tatu zilizopita na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200.

Wakati Ochori Burana na Ruben Pande wakisimulia jinsi walivyonusurika na kifo baada ya kuruka majini na kushikilia tairi la gari hadi walipookolewa, Mitamba Sendeni ameeleza alivyotumia boya kuwaokoa wenzake watatu akiwemo mjamzito.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kilizama Alhamisi iliyopita saa 8:05 mchana, umbali wa mita 50 kabla ya kutia nanga katika ghati la bandari ndogo ya Ukara.

Mpaka jana saa mbili usiku, miili ya watu 218 iliopolewa huku mhandisi wa kivuko hicho, Alphonce Charahani akipatikana akiwa hai baada ya wazamiaji kumkuta katika chumba cha injini ya kivuko hicho.

Akizungumza jana, Burana alisema walianza safari kuelekea Ukara huku kivuko hicho kikiwa na idadi kubwa ya watu na mizigo, yakiwemo magunia ya mahindi na kwamba walimuonya nahodha wa kivuko kutoongeza mizigo mingine.

“Tulimueleza nahodha kutojaza mizigo, lakini hakutusikiliza, ila hilo halikutufanya tusipande kivuko. Tuliingia na safari ikaanza,” alisema Burana.

Alisema wakati kivuko kikikaribia kutia nanga pwani ya Ukara, hali ilibadilika na kwamba, wakati huo nahodha alikuwa akizungumza na simu yake ya mkononi.

“Kumbe wakati anazungumza na simu aliachia ghati, ghafla meli ikaanza kuelemea upande mmoja na magunia ya mahindi yakaanza kutumbukia kwenye maji,” alisema.

Alisema baada ya kuona hali hiyo, alirukia majini na kushikilia tairi la gari lililokuwepo katika kivuko hicho na alikaa majini kwa takribani robo saa kabla ya watu kumuokoa.

“Nilipoona ajali niliruka kwa sababu nilijua tu kuwa kivuko kinazama kwa kuwa kilielemea upande mmoja na maji yalikuwa yameshaanza kuingia ndani. Tairi limenisaidia kuokoa maisha yangu,” alisema Burana.

Alisema katika ajali hiyo amepoteza ndugu zake sita na hadi jana mchana walikuwa wamepata miili mitatu.

Akisimulia tukio hilo manusura mwingine, Pande alisema tairi liliokoa uhai wake kwa sababu meli ilipoanza kuzama, aliruka majini na kuanza kuogelea kulifuata tairi hilo na kulishikilia.

“Tulitoka vizuri, lakini hali ilikuja kubadilika ghafla baada ya magunia ya mahindi kuanza kuporomoka, nilijirusha na kuogelea hadi kwenye tairi lililokuwa linaelea upande wangu wa kushoto,” alisema.

Katika ajali hiyo, Pande alisema amepoteza ndugu zake 10 na hadi jana jioni hakuwa akijua idadi ya miili ya ndugu zake iliyopatikana.

“Kwa sasa (jana mchana) bado akili yangu haijakaa sawa. Ninawaza nilipata wapi ujasiri wa kuruka na kushikilia tairi, yaani siamini kama nipo hai, lakini pia nawaza ndugu zangu ambao wamepoteza maisha,” alisema.

Aeleza alivyojiokoa, kumuokoa mjamzito

Manusura mwingine, Sendeni alisema kivuko kilipozama alibahatika kupata boya ambalo alilitumia kuwaokoa wenzake watatu, akiwemo mjamzito.

Alisema wakati tukio hilo linatokea, tayari alikuwa akimuona mjamzito akitapatapa majini kwa kurusha mikono juu kuomba msaada. “Niliporuka majini niliona boya nikalikamata. Niliposogea mbele kidogo nilimuona mwanamke akinyoosha mikono juu akiomba msaada, nikamsogezea boya na hapo ndio nikabaini kuwa alikuwa mjamzito,” alisema Sendeni.

Alisema aliendelea kuwasaidia wenzake kwa kutumia boya hilo na watu wengine wawili ambao hawafahamu.

Mazingira ya ajali

Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, Sendeni alisema kivuko hicho kilipakia magari mengi kiasi kwamba hata sehemu waliyokuwa wamekaa waliambiwa wasogee ili yapangwe magari.

“Tuliwabishia wafanyakazi wa kivuko na tuliwauliza kwanini wanaruhusu magari kuingia wakati kivuko kimejaa, wakatujibu kuwa tusiwapangie. Kuona hivyo tukatii na kusogea na tukapanda juu. Huo ndio utaratibu wao maana hata siku ilipotokea ajali, asubuhi nilipanda kivuko hicho kilikuwa kimejaa pia. Halafu nilishangaa kuona siku hiyo kilikuwa kimewahi kufika zaidi tofauti na siku zote ambazo hutembea taratibu.”

Alisema wakati akijiuliza maswali hayo, kivuko kilianza kuyumba na kupinduka, “kuona hivyo niliweka chini simu na bahasha ambayo ilikuwa na fedha maana nilikuwa nimetoka benki nikaanza kutafuta namna ya kujiokoa.”

Kwa upande wake, Alice John mama wa watoto wanne, wa mwisho akiwa na umri wa miezi tisa, amesimulia jinsi alivyompoteza mume wake katika ajali hiyo.

“Nilijulishwa na wifi yangu tukio la kuzama kwa kivuko, ila kwa kuwa mume wangu si mtu wa safari, sikuwaza kama atakuwa katika kivuko. Mwili wake umeshapatikana na hapa ninawaza nitaanzaje maisha bila yeye kwa kuwa alikuwa kila kitu kwangu,” alisema Alice.

Chadema wapata pigo

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Ukerewe kimepata pigo baada ya viongozi wake kufariki dunia katika ajali hiyo.

Katibu wa Chadema wilayani humo, Deodatus Makalanga alisema viongozi waliopoteza maisha ni wa ngazi ya shina, vitongoji, vijiji na kata.

“Viongozi hawa wanatoka katika kata nne za Bwisya, Nyamanga, Bukiko zinazounda tarafa ya Ukara,” alisema Makalanga.

Tarafa ya Ukara ni kati ya ngome muhimu za Chadema wilayani Ukerewe. Chama hicho kinaongoza kata tatu kati ya nne zinazounda tarafa hiyo tangu 2015.

Jimbo la Ukerewe pia linaongozwa na Chadema tangu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Imeandikwa na Asna Kaniki (Dar), Jovither Kaijage na Jonathan Musa (Ukerewe)