Sintofahamu yagubika mradi wa nyumba za NSSF Kigamboni

Muktasari:

  • Taarifa za kuuzwa kwa mradi huo ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii mwanzoni mwa wiki hii na hazikukanushwa na NSSF wala Serikali.

Utata umegubika mradi wa ujenzi wa mji wa Kisasa Kigamboni jijini Dar es Salaam uliokuwa ukitekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Azimio Housing Estates baada ya kuibuka taarifa za kuuzwa.

Taarifa za kuuzwa kwa mradi huo ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii mwanzoni mwa wiki hii na hazikukanushwa na NSSF wala Serikali.

Lakini alipoulizwa jana kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe alikanusha kuuzwa kwa mradi huo akisema wanataka kuingia ubia na kampuni nyingine ili wauendeleze.

“Ule mradi tunajaribu ‘kuu-scale down’ (kurahisisha) na kufanya uwe ‘profitable’ (faida), siyo kuuza ila kutafuta ‘partner’ (mbia) ili achukue ule mradi. Kwa hiyo ni ‘joint venture’ (ubia). Bado hatujapata, ‘tuna-negotiate’ (tunajadiliana),” alisema Profesa Wangwe.

Licha ya NSSF kukanusha kuuza mradi huo maarufu kwa jina la Dege Eco Village, kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart imesema kuna mchakato unaendelea na taarifa itatolewa baadaye.

“Bado kuna mambo tunayafanyia kazi tutawapa taarifa baadaye. Nenda Hifadhi House ukawaulize,” alisema mmoja wa maofisa wa Yono ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Mradi huo ulioanzishwa mwaka 2014 kwa gharama ya Dola za Marekani 653.44 milioni (Sh1.3 trilioni) ulitarajiwa kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwani kutakuwa na nyumba za kifahari, majengo ya hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.

Hata hivyo, mradi huo uliokuwa ukisimamiwa na kampuni ya Hifadhi Builders Limited iliyoanzishwa na Bodi ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (Ahel), huku wajenzi wakiwa kampuni ya M/s Mutluhan Construction Industry Company Limited kutoka Uturuki, ulisitishwa Januari, 2016 baada ya kudaiwa kuwapo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh179 bilioni.

Julai 18, 2016 NSSF ilitangaza kuwasimamisha kazi wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja ili kupisha uchunguzi katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

Wakurugenzi waliosimamishwa ni pamoja na Yacoub Kidula (Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Fedha), Chiku Matessa (Rasilimali Watu na Utawala), Said Shemliwa (Udhibiti na Majanga), Paulina Mtunda (Ukaguzi wa Hesabu za Ndani) na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji, Cresentius Magori.

Mameneja waliosimamishwa ni pamoja na Amina Abdallah (Utawala), Abdallah Mseli (Miradi), Mhandisi John Msemo (Meneja wa Mradi), Davis Kalanje aliyekuwa Mhasibu Mkuu na aliyekuwa meneja kiongozi Mkoa wa Temeke, Wakili Chedrick Komba na Mhandisi John Ndazi.

Alipoulizwa kuhusu hatua za kisheria zilizochukuliwa kwa viongozi hao, Profesa Wangwe alisema wameviachia vyombo vya dola kufanya kazi yake.

“Kwa ‘level’ ya bodi tuliwasimamisha kazi, sasa siyo kazi yake ya kutafuta details, ni vyombo vya dola, sisi tumemaliza kazi yetu,” alisema Profesa Wangwe.

Meneja Uhusiano wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mussa Misalaba alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema bado wanalichunguza.

“Hilo suala lipo kwetu tunalifahamu, lakini kwamba limefikia wapi, tuachie sisi,” alisema Misalaba.

Kabla ya kuondolewa kwa wakurugenzi na mameneja hao, Machi 19, Rais John Magufuli alimteua Profesa Godius Kahyarara kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa NSSF Ramadhani Dau ambaye aliteuliwa kuwa Balozi.

Katika ubia wa mradi huo, kampuni ya Azimio Housing Estates ilitakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni ambapo kwa hatua ya awali ilitakiwa kuanza na ekari 300.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilionyesha katika mradi huo NSSF ilikuwa ikimiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estates inamiliki asilimia 55 ya hisa.

CAG alielezwa kwamba Azimio walikuwa wanamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 20,000 Kigamboni, ekari 655.3 Arumeru, ekari 7,832.7 Pwani, ekari 200 Mwanza, ekari 5,723.6 Mtwara, na kwamba maeneo hayo yanafaa kwa ujenzi wa miji ya kisasa.

Taratibu ziliitaka NSSF kujiridhisha kuhusu uwepo wa ardhi hiyo, uhalali wa kisheria wa Azimio kumiliki eneo hilo pamoja na thamani halisi ya ardhi hiyo kutoka mamlaka zinazohusika. Ripoti hiyo ilisema NSSF hawakufanya hivyo na wala hawakumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tatizo jingine kubwa ni kuhusu umiliki wa mradi. Mkataba wa mradi huo uliitaka Azimio kuchangia asilimia 55 zikiwamo ekari 300 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya mradi, huku NSSF ikichangia asilimia 45. Uchambuzi unaonyesha Azimio ilithaminisha ekari 300 za Kigamboni kwa Dola 108,906,113, na ekari 655.3 za Arumeru kwa Dola 556,764,924.

Kwa hiyo kwa miradi miwili hiyo, NSSF ‘imenunua’ ardhi yenye thamani ya Dola 665,671,037 (Sh1.33 trilioni) kutoka Azimio.

Taarifa ya CAG

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 ilisema mkataba wa ubia huo ulionyesha jumla ya gharama za mradi zilikuwa Dola 653.44 milioni na NSSF ilichangia asilimia 45 huku Azimio nayo ikichangia asilimia 35 ya gharama za mradi pamoja na ardhi ambayo itathaminishwa kuwa asilimia 20 ya gharama za mradi.

Hata hivyo ukaguzi wa hatimiliki uliofanywa na CAG ilionyesha kuwa Azimio Housing Estates ilikuwa ikimiliki viwanja viwili; kimoja chenye hatimiliki Na. 81828 cha ukubwa wa hekta 1.98, na kingine chenye hatimiliki Na. 105091 cha ukubwa wa hekta 114.11.

“Kwa kutumia kizio cha ekari 2.47 kwa hekta, hatimiliki hizi zitakuwa na ukubwa wa jumla ya ekari 286.74, pungufu ya ekari 13.26 kutoka kwenye ekari 300 ambazo zilipangwa kwa ajili ya Awamu ya Kwanza ya mradi,” inasema ripoti ya CAG.

“Sijaweza kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio aliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji. Hivyo imekuwa vigumu kwangu kuthibitisha uwepo wa viwanja hivyo,” imeongeza ripoti hiyo.

CAG pia alisema kwa kukosekana kwa hatimiliki, umiliki wa ekari 19,700 za ardhi ambazo sehemu ya mtaji wa Azimio Housing Estates kwa asilimia 20, fedha za NSSF zinakuwa kwenye hatari ya kupotea.

“Menejimenti inashauriwa kuwasiliana na Wizara ya Ardhi ili kuhakiki umiliki wa ekari 19,700 za Azimio Housing Estates katika eneo la mradi. Pia, hatimiliki za ekari 13.26 zilizokuwa pungufu kwenye Awamu ya Kwanza ya mradi zinahitajika kuonekana,” ilisema taarifa hiyo.