Sita watajwa kufariki dunia kivuko cha MV Nyerere kilichozama

Muktasari:

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha amesema timu ya uokoaji bado inaendelea na uokozi na kuna uwezekano idadi ya waliofariki ikaongezeka

Mwanza. Watu sita wamefariki dunia na wengine 20 kuokolewa baada ya kivuko cha Mv Nyerere wilayani Ukerewe kuzama leo mchana katika ziwa Victoria.

Akizungumza na MCL Digital leo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha alisema timu ya uokoaji bado inaendelea na kazi ya uokozi na kuna uwezekano idadi ya waliofariki dunia ikaongezeka.

“Kuna maelezo kuwa katika kivuko hicho kulikuwa na abiria zaidi ya 100 baada ya kupinduka idadi kubwa ya watu wanahofiwa kufariki dunia,” alisema Nyamaha.

Kivuko hicho cha Mv Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.

Mwezi Julai kivuko hicho kilifungwa injini mpya baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma kwa watu wa Ukerewe tangu 2004.

Indelea kufuatilia MCL Digital kwa taarifa zaidi.