Spika, Zitto hapatoshi bungeni

Muktasari:

  • Spika Ndugai ameelekeza Zitto apelekwe kwa mara ya pili kwenye kamati ya maadili kwa kulidharau Bunge

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuwa anaweza kumpiga marufuku Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe kuongea bungeni kwa kipindi chote cha Bunge la 11 na hana cha kumfanya.

Jana Ndugai alimpeleka Zitto Katika Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa kulidharau Bunge.

Akizungumza leo Jumatano mara baada ya kipindi cha maswali na majibu Spika Ndugai amesema anaweza kulichambua Bunge kwa sababu alikuwepo katika vipindi hivyo na Anne Makinda na marehemu Samwel Sitta ni walimu wake.

"Hawa ni watu nawaheshimu sana na wamenilea sana na ni  sehemu nilipofika hapa leo. Utanilinganishaje mimi na milima mikubwa kama Kilimanjaro? Hata siku moja sikio haliwezi kuzidi sikio," amesema.

Amesema katika Bunge la 9 Zitto aliwahi kupeleka hoja ya Mgodi wa Buzwagi ambayo ilikataliwa na Bunge lakini ikazuka hoja ya kimaadili ambapo alihukumiwa hapo hapo.

"Alihukumiwa hapo hapo akapigwa miezi mitatu. Mnataka niende mkuku mkuku kama lile la Bunge la tisa nifanane na mzee Sitta? Hilo pia naliweza kwa nini mnaalika matatizo nashangaa unapambana na Spika," amesema.

"Ninauwezo wa kupiga marufuku kuzungumza hadi miaka yote mitano iishe hauna pa kwenda, hakuna cha swali, nyongeza wala kuzungumza utanifanya nini?

Amemtaka kupambana na mtu mwingine lakini sio yeye.

"Kwa haya ya Spika sina sababu nayo lakini ya kulidharau Bunge hayo sitaweza kuyavumilia nitalinda mihimili huu kwa nguvu zangu zote," amesema.

Amesema hawawezi kuacha wabunge kulidhalilisha Bunge na kuhoji kwamba watachukuliaje Watanzania wengine watakapolidhalilisha Bunge.

Amesema hilo kosa la pili kwa Zitto na kuagiza liende katika kamati ya maadili.

"Tutaenda sambamba mguu kwa mguu hadi kieleweke," amesema