Spika Ndugai awapa pole wanajeshi

Muktasari:

Ametoa pole kufuatia vifo vya wanajeshi 14 wa Tanzania nchini Kongo

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi kufuatia kuuawa kwa askari  14 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Pia Ndugai ametumia salamu hizo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo kufuatia tukio la askari hao waliokuwa katika operesheni ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya  Demokrasia ya Kongo (DRC).

Tarifa iliyotolewa leo, Jumamosi  Desemba 9, 2017 kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Bunge ilieleza kuwa ; “Nimepokea kwa masikitiko makubwa  taarifa hizi za kuuawa kwa askari wetu waliokuwa wakilinda amani DRC, hakika hili ni pigo kwa Taifa zima naungana na Watanzania  wenzangu kuwa pole kwa msiba huu mzito. Nina muomba mwenyezi Muingu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” amesema Ndugai katika taarifa hiyo.

Na kuongeza kuwa ; “Natoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao. Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” amesema.

Mbali na hilo, Ndugai amewaombea askari 44 waliojeruhiwawapone haraka ili waweze kurejea katika majukumu yao na askari wawili waliopotea waweze kupatikana wakiwa salama.