Mkali wa Filamu wa India kupamba tuzo za SZIFF Aprili Mosi

Muktasari:

Amesema kuwa maandalizi ya usiku wa tuzo hizo yanaendelea na wasanii mbalimbali wa hapa nyumbani na kutakuwa na ugeni mkubwa siku hiyo.


Dar es Salaam. Mkali wa filamu kutoka India, Preetika Rao “Aaliya” anatapamba siku ya utoaji wa tuzo za SZIFF kwenye ukumbi wa Mlimani City Aprili Mosi mwaka huu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando amesema mbali ya kupamba siku ya tuzo hizo,  Aaliya ambaye anatamba katika tamthilia ya Beintehaa, pia atapata nafasi ya kuzungumza na wasanii wa filamu wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema kuwa maandalizi ya usiku wa tuzo hizo yanaendelea na wasanii mbalimbali wa hapa nyumbani na kutakuwa na ugeni mkubwa siku hiyo.

Mhando amesema siku hiyo watatoa tuzo kwa wasanii mbalimbali wa filamu katika vipengere 18 tofauti. Pia amesema kuwa watatoa tuzo kwa kipengere cha 19 ambacho ni cha Chaguo la mtazamaji," alisema Tido.

"Kwa sasa mashabiki wa filamu wapo katika zoezi la upigaji kura ya tuzo ya chaguo la mtazamaji kwenye filamu zilizochaguliwa kwa kuandika neno Ndiyo na kuandika namba (code) ya filamu ambayo ipo kwenye kava la filamu husika na kuituma kwenda namba 0757339567," amesema.

Kwa mujibu wa Mhando, jumla ya filamu 143 zilipambanishwa ili kupata zile za kuingia kwenye tuzo ambazo zilionyeshwa kwenye chaneli ya Cinema Zetu katika king'amuzi cha Azam Tv.

Amesema kuwa tuzo hizi ni kubwa na filamu kutoka nchi jirani nazo zimeshindanishwa.