Stanslaus Nyongo awa mwenyekiti wa Muda Kamati ya Viwanda

Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM), Stanslaus Nyongo

Muktasari:

Dk Dalaly Kafumu, mbunge wa Igunga (CCM) ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, na Vicky Kamata (viti maalumu, CCM) aliyekuwa makamu wake, walijiuzulu uongozi kwa kile walichoeleza kuwa ni kupata muda wa kutumikia wapiga kura na pia Serikali kutochukua ushauri wa kamati.

Dar\Dodoma. Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM), Stanslaus Nyongo ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa muda wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Dk Dalaly Kafumu, mbunge wa Igunga (CCM) ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, na Vicky Kamata (viti maalumu, CCM) aliyekuwa makamu wake, walijiuzulu uongozi kwa kile walichoeleza kuwa ni kupata muda wa kutumikia wapiga kura na pia Serikali kutochukua ushauri wa kamati.

Hata hivyo, wakati wabunge wa upinzani wakitoa maoni yao kuhusu kitendo hicho, wabunge wa CCM waliohojiwa na Mwananchi wamesema hawawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hawajapata nafasi ya kusikia vizuri jambo hilo kutoka mamlaka husika.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kamati hiyo ilipoteza urafiki na Serikali baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kutoa ripoti yake kuwa taasisi hiyo imeshindwa kujiendesha kibiashara.