Steve Nyerere ajitosa sakata la Maua Sama, Soudy Brown

Muktasari:

  •  Ni baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya siku nne katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam

Mchekeshaji Steve Nyerere amejitosa kuwaombea radhi kwa vyombo vya ulinzi na usalama, mwanamuziki Maua Sama na mtangazaji wa Clouds FM, Soud Brown akisema anaamini hawakufanya makusudi kuweka mtandaoni video inayowaonyesha mashabiki wakikanyaga noti.

Katika waraka wake wa maneno 272 aliouweka kwenye mtandao wa Instagram amesema kupitia Soudy Brown na Maua Sama wanaoshikiliwa kwa zaidi ya siku tano wamejifunza lakini anaviasa vyombo vya dola kuwasamehe.

“Tumefundishwa kulinda na kuheshimu chochote kile chenye alama ya Taifa, sasa naimani kupitia wenzetu na jamii nyingine kuna la kujifunza hapa tena kubwa sana, ila najua mtoto akinyea mkono wa kulia huukati,” ameandika. 

Ameongeza kusema kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria maana sheria ni msumeno, “Kwa niaba ya wenzetu hawa tunaomba radhi sana tena sana kwa vyombo vyote husika. Imani yangu bado vijana hawa kazi ya kuelimisha jamii kupitia vipaji vyao inahitajika sana mimi kama kijana mwenzao naomba kuchukua nafasi hii kuwaombea radhi naamini hawatarudia na si wao tu hata kwa sisi wengine. Nitafurahi nikisikia wamepewa dhamana. Nitafurahi nikiona wapo huru na kuja kuomba radhi kwa Watanzania.”

Wengine waliojitosa kuwaombea radhi ni mshindi wa Big Brother Africa 2014, Idris Sultan ambaye amesema mamlaka zimtumie mwanamuziki Maua Sama kama balozi wa kuelimisha jamii kupitia makosa aliyofanya.

“Binafsi ningependa kumuombea msamaha Maua kwa kuwa lengo si kuivunjia heshima fedha yetu na Benki Kuu kwa ujumla. Katika harakati za kujitafutia ugali makosa yatafanyika tu ila muhimu ni tukae tukumbuke lengo. Lengo si kukomoana, lengo si kuonyeshana nani anajua zaidi, lengo si kuwekeana mabavu bali lengo ni kuelimisha jinsi ya kutunza vyetu wenyewe.”

Wanamuziki Dayna Nyange, Msami Baby na Shetta kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wamewapa pole Soud Brown, Maua Sama na wengine sita wanaoshikiliwa kwa makosa mbalimbali ya mtandao.

Baadhi ya wanaoshikiliwa ni mtangazaji Shaffi Dauda, Mc Luvada, Tumaini Makene na Michael Mlingwa.